Bodi ya Filamu Yasitisha Usambazaji wa “Imebuma”
Bodi ya Filamu Tanzania imesitisha usambazaji wa filamu ya “Imebuma” mpaka pale maudhui yake yatakapofanyiwa marekebisho.
Akisitisha usambazaji wa filamu hiyo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso amesema mtengenezaji wa filamu hiyo hana kibali cha kutengenza filamu kutoka Bodi ya Filamu na hajazingatia Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu.
Bi Joyce Fisso amesema filamu hiyo imesitishwa kwenda sokoni kutokana na kukiuka vifungu vya kanuni za sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya mwaka 2011 ambayo inakataza kuonesha namna yoyote ya udhalilishaji wa kibinadamu katika filamu na maigizo.
“Baada ya kuangalia kwa makini filamu hii na kuona mapungufu ambayo yanakinzana na Kanuni za Sheria ya filamu na Michezo ya kuigiza nimeamua kuisitisha usambazaji wake mpaka pale wahusika watakaporekebisha maudhi yake” Alisema Bi Joyce.
Bi Joyce amefafanua kuwa filamu hiyo imeonesha baadhi ya matukio ya udhalilishaji wa kibinadamu, ushawishi wa matendo ya ngono na ushoga ambayo ni kinyume na madili ya mtanzania.
Aidha kwa upande wake Afisa Utamaduni kutoka Bodi ya Filamu Tanzania Bw. Julius Tairo amewataka waandaaji na waigizaji wa filamu nchini kufanya utafiti wa kutosha kuhusu maudhui ya filamu kabla ya kutengeneza ili kuondokana na utengenezaji wa filamu zisizofata Sheria na kanuni za utengenezaji wa filamu Tanzania.
JF