-->

Diamond Endelea Kuwaamsha Wasanii Waliolala

NYOTA wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ akisema leo hafanyi tena muziki basi ataweza kuishi kwenye hadhi aliyonayo sasa kwa muda mrefu sana.

Jeuri hiyo anaipata kutokana na kufanya uwekezaji mkubwa kwenye kiwanda cha muziki nchini. Anamiliki lebo yenye wasanii wakali kama Rich Mavoko, Harmozine na Ray Vann.

Tunafahamu ukubwa wa wasanii hao waliopo chini yake, atalia vipi njaa wakati kila msanii anamwingizia fedha kwenye akaunti yake ndiyo maana nimesema hata akiacha muziki ana uwezo wa kuendelea kuishi kistaa.

Hivi karibuni amefungua tovuti yake ya wasafi.com ambayo inauza nyimbo za wasanii wenzake. Ule ni uwekezaji ambao hata asipokuwepo basi vizazi vyake vitafaidi matunda ya tovuti hiyo.

Wasanii wengi wanauza nyimbo zao Wasafi.com, ameingia nao mikataba ambayo ina mpa faida, kwa hiyo unaweza kuona hata asipofanya muziki anaweza kuendelea kujiingizia kipato.

Itafika kipindi hatategemea sana shoo kama chanzo kikuu cha mapato yake, ataanza kutegemea vitega uchumi vyake alivyovitega kwenye muziki wa Bongo Fleva. Hata asipotoa nyimbo jina lake litaendelea kutajwa hivyo umaarufu alionao utadumu kwenye tasnia.

Ndiye aliyeongeza hamasa ya wasanii wa Bongo Fleva kuwekeza fedha nyingi kwenye kazi zao za muziki ndiyo maana leo Bongo Fleva inastawi. Hili ni darasa tosha kwa wasanii wa filamu kuwekeza kwenye kazi zao na kuacha kumtafuta mchawi.

Jana ameweka rekodi nyingine ya kuzindua manukato yake, Chibu Perfume. Ni unyunyu wa kwanza kumilikiwa na msanii wa kitanzania, hii ni biashara ambayo itakamuweka kwenye ramani ya dunia hata akiacha muziki.

Anasema jina la Chibu ni la utoto kwani enzi hizo alishindwa kutaka jina Naseeb na badala yake akiulizwa anaitwa nani anajibu aitwa Chibu. Ni kumbukumbu nzuri kwake.

Lakini pia amewashtua wasanii hasa wa filamu ambao upande wao hali si shwari kuwa ukiwekeza unakuwa na uhakika wa maisha yake hata utakapoacha kufanya sanaa.

Mastaa fanyeni kazi wa weledi, kidogo mkipata fedha wekezeni nje ya sanaa kwa sababu kuna maisha nje ya ukubwa wa majina yenu.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364