-->

Diamond, Giggy Money na Wema Sepetu…

Maisha yetu yapo kuligana na mawazo yetu. Furaha yako maishani inategemea na ubora wa mawazo yako.

Huwezi kumuweka kwenye kundi la vijana mabishoo. Ni mtoto wa kihuni. Hajali. Na kutokujali kwake ndiko kulikomfikisha pale alipo. Kifupi hasikilizi wala hana hofu na watu watasema nini. Ogopa sana mtu wa hivyo.

Ndiyo Diamond Platinumz. Kuna wakati unajiuliza ana moyo kama sisi wengine kweli? Yeye hana habari. Kijana fulani aliyekuwa na hasira na maisha halafu maisha yamepotea maboya yakatuama kwa mbavu zake. Ogopa.

Katika dunia ya sasa ukiogopa macho ya watu utabaki gizani wengine wakipasua anga. Ili utusue inabidi mishipa kadhaa ya soni aibu na hofu uitoe kwenye kichwa na moyoni.

Kuna wanamuziki wakali kuliko Diamond, ila yeye anawazidi kwenye kujiongeza. Kupita sehemu isiyopitika na kumvaa mtu asiyevalika.

Watu wenye mioyo kama hii ni rahisi sana kukutana na mtoto mzuri kwenye ndege halafu baada ya miezi miwili kummiliki mazima na mimba juu.

Ndivyo walivyokutana na Zari. Wenye tabia hii huishi kwenye yale aliyokuwa anayaota kabla. Kamata sana watoto wazuri. Changanya bongo za masista duu. Simamisha shughuli mitandaoni.

Kifupi dogo anaishi maisha ambayo vijana wengi wanayaota kila siku mpaka vitanda vinaoza. Wengine wako Keko na Segerea kwa kosa la kutaka kile anachokipata Diamond wa sasa hivi.

Alianza kama mwanamuziki. Hivi sasa ni mwanamuziki anayetengeneza habari kila siku. Usipomsikia kwenye muziki na kumtazama kwenye video. Utamsoma kwenye magazeti na mitandaoni. Anatumia fursa.

Tatizo ni njia. Upenyo. Kwa kifupi ni ‘koneksheni’ ya watu ili uweze kutoka. Hili tatizo siyo Bongo tu ni dunia nzima. Tena Bongo inaweza kuwa rahisi sana kuliko nchi za wenzetu.

Nigeria kuna watu wengi sana. Kila mtu anataka kutoka, na asilimia kubwa ya wananchi wa Naijeria elimu ya kawaida kwao ni ya chuo kikuu. Wakati sisi wengi wetu ni kidato cha nne wao ni wenye digrii.

Kupata nafasi ya kutoka kwa nchi kama Nigeria ni kazi kubwa sana. Na ukitoboa ujue wewe ni balaa. Ndiyo maana wengi wanakuwa matapeli kwa sababu njia zote zimebana, kila mtu anataka unachotaka na wako wengi.

Ni kama ajira kwa hapa Bongo. Wakihitajika watu kumi wanakuja elfu kumi kwenye usaili. Sasa ndani ya Amerika nchi yenye watu zaidi milioni 300 na zaidi unategemea kutoka kirahisi? Vipi China na India?

Sasa Kibongo Bongo kuna mwanadada mmoja aitwaye Giggy Money. Jina lake halisi ngumu sana kulijua. Inatosha tu kumjua kwa jina hilo la Giggy Money. Kwa kumtazama au kumsikia unaweza kudhani kituko hivi.

Lakini asikudanganye mtu msichana yule akili kubwa. Njia aliyopitia kutangaza uwepo wake katika uso wa burudani hapa Bongo ni njia ngumu sana kwa mtu mwenye utashi wa aibu na soni zenye haya ndani yake.

Giggy Money alifumba macho. Akajichetua. Akaziba masikio kisha akaamua kama mbwai na iwe mbwai, kwani hatari kitu gani bana. Akili hii inapatikana kwa watu wachache sana ili kutoboa.

Kwa nyakati hizi ukiwa na akili kama za Giggy utasikika. Ukiwa na akili kama za Enika utapotea. Enika mwanamuziki mwenye kiwango cha juu kabisa ukitaja jina lake watu wa dunia hii hawawezi kukuelewa unaongea kitu gani.

Hata siasa za nchi hii ili utoke inabidi ujifyatue akili kidogo, bila hivyo utaendelea kuwa shabiki tu na mfuasi usiyekuwa na faida wala hasara kwenye macho ya watu.

Diamond baada ya kutoka kimuziki, ili aendelee kuwa juu kila siku akapita njia kama za Giggy. Matokeo yake katikati ya sakata la maumivu ya Tundu Lissu dogo anasimamisha shughuli za watu anaongelewa yeye tu.

Kwa wiki nzima watu wakaweka pozi matatizo ya Lissu, wakasahau kama kuna kitu kinaitwa ‘Mara Paaap. Tumekusoma’ Fiesta. Watu wako ‘bize’ na Diamond. Siyo kwa muziki wala video mpya. Ni vurugu zake za kwenye chaga za kitanda.

Hii akili inapatikana kwenye vichwa kama hivi vya kina Diamond, Giggy na Wema. Haya huwezi kuyakuta kwenye akili na mtazamo wa kina Kiba na Jokate.

Giggy Money ulichokitaka umekipata. Hata kama hujakipata kuna mwanga mzuri wa kukipata. Nampa Papa bonge la wimbo kwa nyimbo za kizazi hiki.

Pamoja na uwepo wa ukuta mrefu wa wasanii ambao wameshikilia kila kitu cha muziki wa kizazi kipya bado Giggy Money na upweke wake kaweza kutoboa.

Giggy Money. Tulia sasa kisha shikilia hapo hapo, huo ndiyo mwanzo wako mzuri na bora kabisa ukiachia kitu kingine zaidi ya hiki ‘Nampa Papa’ utakuwa katika dunia nyingine ya muziki.

Kama masihara vile Giggy Money huyu hapa. Umepitia nyakati ngumu na hatarishi kwa mustakabali wa maisha yako. Ungeweza kuonekana takataka tu lakini kwa huu wimbo wako tunaona kabisa unaelekea kwenye neema ya heshima na kitu adimu mbeleni.

Sasa jipange sana, fanya kama kugeuza bluu kuwa njano. Komaa kama ulivyokomaa kwenye kutengeneza jina sasa komaa kwenye kuuonesha umma kuwa una kipaji cha muziki.

Kilichotokea ni kwamba umeanzia pale alipo Diamond wa sasa kisha unarudi kwa Diamond wa mwanzoni. Yaani Diamond alifanya muziki ili atengeneza habari. Wewe umetengeneza habari ili ufanye muziki.

Tuliza mizuka sasa na shirikisha akili kubwa kwenye burudani ya muziki ili utoboe. Unajua maisha ya mjini. Unawajua wanamuziki. Unawafahamu wadau wakubwa wa muziki. Mungu akupe nini? Komaa.

Wakati Diamond alifanya kweli kwenye muziki ili akutane na magwiji wa biashara ya muziki. Wewe umejenga ukaribu na magwiji wa biashara ya muziki kwanza ili ufanye muziki. Ukitulia utachomoka.

Njia uliyopitia ni ya giza totoro lakini umepenya na kuwa mmoja wa wanadada wanaofanya watu watizame mitandaoni vituko vyako.

Sasa geuza akili zao uwe miongoni mwa wasichana wanaopanua masikio ya watu ili usikilizwe kwenye muziki. Punguza mitoko isiyo na msingi. Muziki unahitaji utulivu sana na ubunifu mkubwa ili utoke.

Wema yeye ni toafuti kidogo na Diamond na Giggy. Mazingira ya jina la Wema kwa kipindi kirefu limejijenga kwenye mahusiano zaidi ya kimapenzi kuliko kazi yake. Anapata tabu sana hivi sasa kuliko wengi wanavyofikiria.

Katika mazingira ya kawaida, Wema anahitaji kutumia guvu sana kuwaaminisha mashabiki wake katika kazi kwanza. Ili waachane na matazamo wao wa sasa wa kumuhusisha na mambo ya kiuhusiano wa mapenzi zaidi.

Kinachotokea ni kwamba mamilioni ya mashabiki wa Wema wanataka kusikia ‘drama’ zake tu na siyo kingine. Katika mazingira haya anapata wakati mgumu sana wa kutangaza biashara yake.

Yaani Wema ananoga kwenye masikio ya mashabiki wake akiongelewa kwa mambo ya mapenzi. Yaani wanatamani hivi sasa Wema angekuwa ndiye Hamisa Mobeto ili apambane na Zari.

Wanasahau kuwa ana filamu mpya anayohangaika kuiuza mitandaoni.

Tangu alipotwaa taji la Miss Tanzania, usiku ule wa 2006 pale Diamond Jubilee, akaanza kuvuma kwa habari za mapenzi tu. Kila habari yake ilihusu mapenzi.

Mashabiki wake wameganda kwenye ‘ishu’ hizo na kusahau kuwa ni msanii wa filamu ambaye anahitaji ‘sapoti’ yao ili aendelee kuishi. Mashabiki wake wameganda na mapenzi.

Hata wale wanaomuunga mkono Hamisa kwa wakati huu. Ni wale ambao waliumizwa na uwepo wa Zari kule Madale badala ya kipenzi chao Wema. Kifupi wanapunguza machungu ya hasira zao kwa kipenzi chao Wema.

Wanaacha kumalizia hasira zao kwa kumuunga mkono kwenye biashara yake ya filamu, wameganda kwenye matukio yake ya mapenzi. Mashabiki wa Wema Mungu anawaona. Msaidieni kwa kununua kazi yake kwanza.

Mtu haogopi yasiotambulika, huogopa yanayojulikana kufikia

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364