Dj Mark: Tamthilia za Nje Zinaipiku Mno Bongo Movie
‘WANAKUJAAA hao!’ Msemo huu si mgeni masikioni mwa wafuatiliaji wa tamthilia za kikorea, kifilipino, kizungu, kichina na filamu mbalimbali ambazo zimewekwa vionjo vya lugha ya kiswahili.
Maneno hayo hutumiwa zaidi na Ahmada Abdulrahman maarufu Dj Mark, G Mashine, Jogoo kutoka lebo ya Acheche Production.
Licha ya biashara hiyo kupingwa na Serikali kwa kukiuka sheria za hakimiliki na kulalamikiwa kukiuka maadili ya Watanzania, lakini ni kimbilio kubwa la vijana katika kujipatia ajira zisizo rasmi.
Miaka ya 80, Kapten Lufufu Mkandala (marehemu) ndiye aliyeingiza mfumo huo nchini baada ya kupata mafunzo nchi za Vietnum. Kazi hiyo iliwavutia wengi kwani miaka ya 90 vijana wengi akiwemo Dj Mark ambaye katika makala haya anaeleza mengi, naye alikuwa mmojawapo kama anavyoeleza katika mahojiano haya.
MTANZANIA: Uliingiaje katika kazi hii?
Dj Mark: Nilikuwa nikimfuatilia sana mzee Lufufu, nilipofikisha miaka 18 nikiwa naishi Tandika nilitamani sana kufanya kazi aliyokuwa akiifanya mzee Lufufu ya kuweka maneno katika filamu mbalimbali za nje.
Hivyo mama yangu alivyoanza kuugua wakamuhamishia Zanzibar na baba yangu alihamia Arusha kwa shughuli zake, mimi nikabaki na kaka ambaye hata hivyo hakukuwa na uangalizi mzuri, nikaamua kuacha shule nikiwa kidato cha pili, nilipomweleza baba kwamba sitaki tena shule aliniuliza ninachotaka, nikamwambia nataka kazi anayofanya mzee Lufufu.
MTANZANIA: Vipi baba yako alikuelewa?
Dj Mark: Alielewa baada ya kumueleza mahitaji yangu, alirudi Dar es salaam akauza kiwanja chake Sh 400,000, akanunua TV ambayo nayo ilikuwa ikiuzwa Sh 400,000, aliongeza fedha nyingine Sh 180,000 akanunua deki akanikabidhi, aliniambia kwamba hayo ndiyo maisha yako uliyoyataka.
Hapo nikashukuru ingawa maneno yale yaliniingia akilini nikaamua kwenda kuanza maisha Arusha, huko nikafungua kibanda cha kuonyesha filamu za nje huku nikijitahidi kufikiria mzee Lufufu jinsi anavyoingiza sauti katika filamu, bila ya kujua alivyokuwa akifanya, nikawa kila ikifika saa 12 jioni naweka CD ya filamu za kizungu kisha nakaa pembeni na TV nawasimulia kinachojiri katika filamu hiyo, wakapenda watu wengi zaidi wakawa wanakuja katika banda langu, lakini baadaye kuna mzee alikubali kazi yangu aliamua kunipa redio yake ya kizamani iliyokuwa na spika mbili, nikawa naongea kwenye mic sauti inasikika kwenye spika za redio.
Kipindi hicho nilikuwa eneo la mgodi lakini baada ya kutokea ugomvi mkubwa kwa wachimba mgodi, wafanyabiashara wote tukafukuzwa huko, nikaamua kurudi Ungalimited nikafungua mabanda matatu ya kuonyesha video na duka moja la kawaida.
MTANZANIA: Ulifanikiwaje kuingiza sauti moja kwa moja katika filamu.
Dj Mark: Baadaye ulikuja utaalamu wa kurekodi kwa deki la mikanda VHS kwa VHS, nikaanza kurekodi kwa kutumia deki mbili, lakini sikuwa na soko la kuuzia filamu hizo, hivyo nikaja Dar ambapo niliona kazi za mtu mwingine anayefanya kazi kama yangu anaitwa Juma Kan filamu zake zilikuwa na picha ya Kava.
Katika tafuta tafuta ya mteja, nikapelekwa kwa mhindi anaitwa Ajey akaniambia yeye anafanya kazi kama yangu lakini anatafsiri za kihindi ila aliniambia kwamba soko la filamu za kizungu lilishikwa na mzee Lufufu, nikajua nimekosa kazi lakini baadhi ya watu walimshauri mhindi huyo akachukua na kazi zangu kwa kuwa Lufufu alikuwa peke yake anaishi Bukoba na umri ulikuwa umekwenda na hakuweza kutoa filamu nyingi zaidi.
MTANZANIA: Malipo yako ya mara ya kwanza yalikuwaje baada ya kupata soko?
Dj Mark: Mwaka huo ulikuwa 2007, yule mhindi alianza kunilipa Sh 6500 kwa mkanda mmoja lakini baada ya muda mfupi wa kufanya kazi na yule mhindi nikaona anazidi kuvunja na kutanua duka lake, kumbe alikuwa anaingiza fedha nyingi sana kutokana na kazi yangu, nikakataa kuendelea na malipo yele akaniongezea ikawa Sh 8500, baadaye ikawa Sh 15,000 kwa mkanda mmoja. Nikawa kwa siku najitahidi naingiza maneno ya Kiswahili mikanda minne ili nipate fedha nyingi.
Mwaka 2009, Steps wanaofanya kazi na Bongo Movie waliniita walitaka niingize sauti kwa kufuata sauti za wahusika kulingana na jinsia zao, tukashindwana lakini wakakubali niendelee na aina yangu ya kuingiza sauti kwa filamu zao walizonipa wakawa wananilipa kwa mkanda mmoja Sh 50,000 lakini baada ya miezi takribani sita, yule mhindi wa awali alikamatwa na polisi hivyo Steps wakasitisha kuendelea na kazi hiyo.
MTANZANIA: Baada ya kukamatwa huyo mnunuaji wa kazi zako, maisha yaliendeleaje?
Dj Mark: Baada ya hali hiyo, ilinibidi niingie mwenyewe sokoni kwa kutumia namba za simu katika kila mkanda nilioutoa, niliweka namba nikawa nawapelekea watu mtaani hadi nikazoeleka.
Na sasa nafanyia kazi zangu Kariakoo kwa kuwa kodi ni kubwa hadi milioni moja inafika, hivyo tumeamua watu watatu tunaofanya kazi za aina moja tumechangishana tumekodisha lakini kila mtu anafanya shughuli yake.
Tunajua kazi hii si rasmi kwetu lakini imesaidia ajira watu wengi kama mimi nina miaka 20, kuna ugumu mkubwa wa kupata hakimiliki za watu tunaotumia kazi zao mfano inawezekanaje kupata hakimiliki za kutumia kazi za Rambo, naanzia wapi kuzipata na gharama yake kama ataniambia milioni 100 nitawezaje kujilipa wakati katika CD moja napata faida 300.
MTANZANIA: Sasa una ujumbe gani kwa Serikali kuhusu kazi yenu?
Dj Mark: Mimi naiomba Serikali ijenge mazingira mazuri kwa kazi zote za sanaa ikiwemo yetu, watusaidie hakuna asiyetaka kulipa kodi lakini tutengenezewe mazingira mazuri, mfano mdogo waende kwenye vituo vyote vya daladala ama masoko nchini lazima kazi zetu zipo au waende Kariakoo kwenye maduka ya CD kuanzia asubuhi hadi jioni waangalie wanaonunua CD zile kwa ajili ya wao nao kwenda kuziuza wataona watu wa kila aina wazee, vijana na wanawake, hii inaonyesha ni kazi inayotoa ajira, inatakiwa iwekewe mazingira mazuri si kutukataza kuifanya.
MTANZANIA: Hivi mna chama cha kuwasaidia kufikisha malalamiko yenu kwa Serikali?
Dj Mark: Chama kipo lakini tumejiunga na watu wa library ila huwa tunakutana kama kuna jambo kubwa la kugusa masilahi yetu linatokea ndipo tunakutana tunazungumza tofauti na hapo kila mtu anajijua mwenyewe.
MTANZANIA: Mwaka 2016 mmeliteka sana soko la Bongo Movie kwanini?
Dj Mark: Bongo Movie hawajajitambua hadi leo wanatafuta mchawi wakati wachawi ni wao wenyewe, wanatakiwa kumwangalia mlaji wao ni nani? Anapenda nini? Je, malalamiko yake yanafanyiwa kazi? Wao hawayafanyi kazi hayo ndiyo maana wanafeli.
Sisi si washindani wa Bongo Movie kwa maana CD zetu ni chafu katika sauti, tunakata tunaweka sauti nyingi za Kiswahili wakati mwingine tunakosea kutafsiri lakini cha ajabu wananchi wanazipenda zaidi zetu kuliko filamu za Bongo Movie, lazima hapo kuna tatizo.
Na tatizo kubwa ni kwamba wananchi wamewachoka waigizaji wale wale, mfano Ray Kigosi, JB na wengine uigizaji wao ni ule ule hadi leo na bado wanaendelea kutoa filamu zile zile zenye sehemu mbili hadi tatu na bei ni zaidi ya 3000, halafu kama wanaigiza kuhusu polisi kuanzia mavazi ni uongo hayana uhalisia wa nguo za polisi wa Tanzania, kituo cha polisi hatujawahi kuonyeshwa kituo cha polisi cha kweli wala gari la polisi la kweli, location zao hadi uigizaji wa ovyo unategemea watu waendelee kununua kazi mbovu.
MTANZANIA: Nini wafanye Bongo Movie ili warudi katika ushawishi wao?
Dj Mark: Wawekeze tu, tena haihitaji akili nyingi waige kwa Diamond, video yake ya dakika mbili na sekunde kadhaa ya ‘My Namber One’ ametumia zaidi ya milioni 50 kwa sasa ni msanii wa kimataifa, anapata shoo nyingi za fedha nyingi zaidi ya uwekezaji wake, inakuwaje Bongo movie wanawekeza milioni 10 kwa filamu za zaidi ya dakika 90 wahusika kibao, location za kuungaunga, hiyo filamu kweli ama utani ndiyo maana nasema hawajielewi.
Wazungumze vizuri na Serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya sanaa awasaidie wapate vifaa kama magari ya polisi, sare na vitu vingine ili waendane na uhalisia maana sanaa kwa sasa imekuwa kubwa mno hakuna wa kumdanganya, kila mtu anataka kitu bora lakini jingine wawekeze waache utani katika kazi.
Mtanzania