Dogo Janja: Nakua na Mziki Wangu
Msanii Dogo Janja ametoa sababu inayomfanya azidi kuwa bora kwenye kazi zake, kadri siku zinavyokwenda, tofauti na wasanii wengi ambao wakitoa hit song, hushindwa kuendelea nazo.
Akizungumza kwenye FNL ya East Africa Television na East Africa Radio, Dogo Janja amesema kwa sasa yeye anakua kiumri, hivyo hata uwezo wa kuandika mashairi yake unakua.
“Mimi ninakua sasa hivi, kwa hiyo hata uandishi wa mashairi yangu unabadilika, ukiangalia kuanzia anajua, siri zao, ya moyoni, mtoto wa uswazi, my life mpaka kidebe, utagundua kuna tofauti, kwa hiyo ninapokua nakua na muziki wangu”, alisema Dogo Janja.
Pia Dogo Janja ambaye kwa sasa ameachia video yake mpya ya ‘kidebe’ iliyofanywa hapa bongo, alizungumzia suala la kufanya show nyumbani kwao Arusha, na kusema kwa sasa yeye ni msanii mkubwa, hivyo show anayotaka kufanya lazima iandaliwe vya kutosha, lakini ni lazima akafanye show Arusha kwani ndio nyumbani (home boy), na wanamkubali kama familia na sio mashabiki tu.
“Unajua ukizungumzia show sasa hivi, inabidi nikafanye kama pale uwanjani, kwa hiyo inabidi iandaliwe, na Arusha mi ni nyumbani lazima niende, kwanza home boy wananikubali, ukiniongelea vibaya kule utarudi unavuja damu”, alisema Dogo Janja.
eatv.tv