Mwanamitindo Flaviana Matata Aiburuza Mahakamani PSPF
MFUKO wa Pensheni wa PSPF umeshtakiwa mahakamani ukitakiwa kumlipa mwanamitindo wa Tanzania anayefanya kazi za mitindo nchini Marekani, Flaviana Matata, Sh milioni 165.
Mfuko huo umeshtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kukiuka mkataba wa mwanamitindo huyo anayewakilishwa na Wakili Edward Lisso wa Law Associates Advocates.
Mfuko huo unadaiwa kukiuka mkataba walioingia Januari, mwaka jana unaohusisha ‘fashion modeling services’ kwa ajili ya mfuko huo.
Inadaiwa mkataba huo unamhusisha mwanamitindo huyo kuitangaza PSPF katika shughuli zake kwa lengo la kuvutia wateja kwa mwaka mmoja.
Flaviana anaiomba mahakama iiamuru PSPF imlipe Sh milioni 100 kama fidia ya jumla kwa kupata hasara kwa kutopata fursa za kibiashara na mifuko mingine na kampuni nyingine za kibiashara kwa vile bado ana biashara na mlalamikiwa (PSPF) na kwa kupoteza muda na fedha wakati akifanya mawasiliano na mlalamikiwa na ugumu alioupata wakati akifuatilia suala hilo.
Kutokana na hilo, Flaviana anadai anakula hasara ya kiuchumi kwa vile picha zake zinaendelea kutumika kinyume na mkataba.
Shauri hilo lipo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Magreth Bankika na litatajwa Septemba 22, mwaka huu.
Mtanzania