-->

Sababu za Mastaa wa Bongo Movie Kugeuza Usiku Kuwa Mchana

STAILI ya maisha ya mastaa wengi ulimwenguni inafanana lakini zaidi ni ile tabia yao ya kubadilisha usiku kuwa mchana kwa sababu mbalimbali, Juma3tata linakuondolea utata.

HEMMED

Siyo jambo la ajabu kwa mastaa kufanya kazi zao mpaka usiku mwingi kisha alfajiri kulala hadi mchana wa jua kali, muda ambao watu wengine huwa makazini wakitafuta riziki zao.

Ukiacha wanaofanya kazi nyakati za usiku, wapo wengine wanaokuwa kwenye majumba ya starehe, wakila bata usiku mzima, kisha kutumia mchana kupumzika.

Juma3tata lina ripoti iliyoshiba baada ya kuzungumza na mastaa wa fani mbalimbali Bongo na kueleza sababu za wao kubadili usiku kuwa mchana.

Hemed Suleiman 

Kutokana na namna kazi ya muziki ilivyo, wasanii wa muziki hulazimika kukesha usiku kucha wakipiga shoo katika kumbi mbalimbali na kurudi majumbani alfajiri na hivyo kupumzika mchana.

Hilo linawekwa sawa na msanii wa filamu ambaye pia ni mwanamuziki, Hemed Suleiman ‘PhD’ aliyesema kwamba, muda wake wa kulala huwa kati ya 10 – 11 alfajiri.

“Kazi inasababisha iwe hivyo. Kuna wakati labda nina scene za kucheza usiku, kama ni nyingi basi nalazimika kulala mchana mzima ili usiku niweze kwenda kufanya kazi nzuri.

“Usisahau kuwa mimi pia ni mwanamuziki, wakati mwingine huwa natakiwa kwenye shoo, kama unavyojua tena shoo nyingi ni za usiku kuliko mchana. Hiyo ndiyo husababisha nishindwe kufuata utaratibu wa kawaida wa maisha ya binadamu unavyopaswa,” anasema Hemed.

Snura Mushi 

Sababu nyingine inayowafanya mastaa kubadilisha usiku kuwa mchana, inaelezwa kuwa ni kutafuta utulivu wa akili wakati wa kutunga kazi zao.

Hoja hii inaungwa mkono na msanii wa filamu na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Snura Mushi ambaye anasema: “Huwa natunga nyimbo zangu usiku. Ni muda ambao umetulia na kichwa kinaweza kufanya kazi na kufikiri vizuri. Usiku ni mzuri kwa kutunga maana hata vurugu za watoto nyumbani zinakuwa zimeshapungua kabisa.”

Snura anasema mara nyingi muda wa kulala huwa kati ya saa 9 – 11 alfajiri kulingana na namna atakavyokuwa amechoka, huku akiamka kati ya saa 6 – 7 mchana.

Yusuph Mlela 

Staa wa filamu za Kibongo, Yusuph Mlela anasema yeye huamua kulala mchana na kufanya kazi zake usiku kwa sababu ya kutafuta utulivu kama walivyotangulia kueleza Snura na Tuwa.

“Kwa kawaida huwa nalala saa 11 alfajiri na kama ikitokea nikawahi sana basi ni saa 9, kuamka ni kati ya saa 8 – 9 mchana ili kujiepusha na uzee wa wa usinginzi. Napenda kufanya shughuli zangu usiku, mchana inabidi tuwaachie watu walioajiriwa, usiku ni muda wa sisi tuliojiajiri,” anasema Mlela na kuongeza:

“Lakini pia kuna wakati mtu unataka kwenda kula bata, huwezi kufanya kazi muda wote, kama staa lazima upate muda wa kutoka ili kupanua mawazo na kukutana na watu tofauti.”

IRENE UWOYA 

Uwoya anasema yeye huchelewa kulala kwa sababu ya mizunguko yake (mitoko) au kazi zake za kisanii zinazofanyika usiku wakati mwingine.

“Sina ratiba maalum, lakini kwa kawaida huwa nalala kati ya saa 10 – 11 alfajiri na kuamka kati ya saa 7 – 9 mchana. Sasa itategemea kama labda nilikuwa location kwa ajili ya kurekodi filamu au nimetoka na mambo mengine lakini usiku ni muda wangu wa kufanya mambo yangu na mchana ni muda wa kulala,” anasema Uwoya.

Mtanzania

 

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364