-->

Ethiopia Kuleta Umeme wa Bei nafuu, Asema Rais Magufuli

Dar es Salaam. Tanzania itapata umeme a megawatt 400 kutoka Ethiopia baada ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hailemariam Desagen kukubaliana kushirikiana katika mambo 13.

Rais Magufuli akisalimiana na kumpokea mgeni wake Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Dessalegn mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal One jijini Dar es Salaam.

Mbali na umeme, masuala mengine ni usafirishaji wa anga, bandari, matumizi ya Mto Nile, vibali vya kufanya kazi ndani ya nchi hizi mbili, utalii, kilimo, uboreshaji mfumo wa kodi, elimu, viwanda, madini na mazoezi ya riadha.

Ethiopia ilikubali kutoa kiasi hicho cha umeme kwa Tanzania katika mradi wake mkubwa wa umeme wa Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha MW 6400.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana wakati wa mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mawaziri kutoka pande zote.

“Wamejenga dam (bwawa) linaloitwa Gibe Dam inayoweza kutoa megawatts 1,870. Na wanajenga sasa hiviu dam, moja kubwa kuliko dam yoyote katika Afrika inaitwa GERD inayoweza ku-produce megawatts zaidi ya 6,400 za umeme,” alisema Rais Magufuli.

“Ukitaka kujenga uchumi wa viwanda, lazima uwe na umeme. Wenzetu Ethiopia wametuonyesha njia. Na mimi nimemuomba.”

Alisema Desagen amekubali maombi hayo ya umeme huo ambao utakuwa wa bei nafuu na hivyo kulipa Shirika la Umeme (Tanesco) changamoto.

Mazungumzo hayo yaliambatana na utiaji saini wa mikataba mitatu ambayo ni wa mkakati wa ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia ambao unalenga kupambana na tatizo la wahamiaji haramu, biashara na uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya afya.

Mkataba mwingine ni kuanzisha kamisheni ya pamoja ya kudumu baina ya serikali ya Tanznia na Ethiopia ambayo itahusisha wizara za mambo ya nje za Tanzania na Ethiopia na kushirikisha sekta nyingine. Mikataba hiyo ilisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Dk Workneh Gabeyehu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Suzan Kolimba.

Pia, serikali hizo mbili zilitiliana saini hati ya makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya utalii ambao utatoa fursa ya za uwekezaji wa pamoja na mafunzo kwa wadau wa sekta ya utalii. Mkataba huo ulisainiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Utamaduni na Utalii wa Ethiopia, Dk Hirut Teketel.

Rais Magufuli pia alizungumzia makubaliano baina ya mashirika ya ndege ya Ethiopian Airways na ATCL, akisema shirika hilo la Ethiopia sasa litageuza Tanzania kuwa kituo chake kikuu cha mizigo.

Alisema uamuzi huo utasaidia nchi zote mbili, ikiwa ni pamoja na Ethiopia kuanza kutumia Bandari ya dar es Salaam kupitishia mizigo yake kwa kuwa nchi hiyo haijapakana na bahari.

“Shirika la Ndege la Ethiopia ni kubwa sana, lina ndege 96 na wameagiza nyingine 42. Ndege zao zinatua katika viwanja zaidi ya 92 duniani kote. Hii ni nafasi kwetu kujifunza kutoka kwao ili tuongeze mapato yetu,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Desalegn alisema Tanzania na Ethiopia zina uzoefu tofauti katika kukabiliana na changamoto, hivyo wana wajibu wa kubadilishana uzoefu huo ili kujiletea maendeleo.

Alisisitiza kwamba ni muhimu kuboresha kilimo kwa sababu wananchi wengi wanategemea kilimo. Alisema endapo serikali zitafanyia kazi suala hilo, zitakusanya mapato mengi kupitia wakulima hao.

“Asilimia 70 ya nguvu kazi katika nchi zetu ni vijana chini ya miaka 35, tukiwatumia hawa tutapiga hatua kubwa kwa sababu ndiyo nguvu kazi ya ujenzi wa Taifa lolote,” alisema Desalegn na kusisitiza kwamba Tanzania na Ethiopia zimekuwa na historia inayofanana.

Lugha ya Kiswahili

Kuhusu kuendeleza lugha ya Kiswahili Rais Magufuli alisema amejitolea kutoa maprofesa na walimu kwenda kufundisha lugha hiyo nchini Ethiopia.

Alisema amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na Dessalegn kuwa akifika Ethiopia atachagua chuo kimoja cha kufundisha lugha hiyo.

“Kiswahili ni lugha ya Afrika, na kwa sababu makao makuu ya Umoja wa Afrika hayataondoka Ethiopia na yeye ni mtawala, pale Addis Ababa si vibaya akichagua chuo kimoja kwa ajili ya kukuza Kiswahili,” alisema.

Alisema miongoni mwa makubaliano yao pia ni katika kilimo, kwa sababu uchumi wa viwanda unaendana na kilimo endelevu kwa ajili ya kupata malighafi za viwandani.

Pia alisema Ethiopia pia itaisaidia Tanzania katika kupata njia za kunufaika na mashirika ya mawasiliano ya simu kutokana na mafanikio iliyoyapata kwao.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364