-->

Faraja Nyalandu na Hoyce Temu Walitumia Uchawi Gani?

Na RAMADHANI MASENGA

KWANZA huanza kwa kupita jukwaani. Kisha yanafuata ni mambo ya ubunifu. Baadaye ndipo huanza kuulizwa maswali.

Hoyce Temu na Faraja Nyarandu

Moja kati ya maswali wanayoulizwa mamisi wetu ni pamoja wapi ulipo Mlima Kilimanjaro, Baba wa Taifa alizaliwa mwaka gani na Ziwa Tanganyika linapatikana mkoa gani.

Baada ya hapo mambo mengine hufuata. Kisha jina la mshindi hutajwa. Mara nyingi mshindi atatembelea vivutio vya  utalii. Atatembelea kambi wanayoishi wazee na mwisho atapita katika vituo vya watoto yatima kula na kupiga nao picha.

Hapo mrembo anakuwa kafanya kazi yake kwa kiwango cha juu sana. Halafu huwa kimya. Ukianza kumsikia tena basi atakuwa kawa msanii wa filamu ama kapora bwana wa mtu. Ukweli huu unauma ila bahati mbaya hauna mbadala.

Kama sivyo tuambiane ukweli baada ya Wema Sepetu kushinda alifanya nini cha maana zaidi ya nilivyotaja? Baada ya Siti Mtemvu kutangazwa mshindi kabla hajavua taji, ni jambo gani jipya alifanya?

Mwezi mmoja baada ya mshindi wa mashindano ya umisi kutangazwa, umaarufu wake katika mambo ya maana hufika kikomo.

Baada ya hapo ni kashfa na vituko. Mara ataonekana kavaa nguo ya usiku mchana ama ataonekana akifanya mambo ya chumbani hadharani.

Kwa uwekezaji huu wa mamisi ndiyo maana mpaka leo wazazi wengi wanaona tasnia hiyo ni uhuni. Toka haya mashindano ya urembo yameanza mpaka sasa, ni wasichana wachache mno walionyakua taji na bado wamekuwa lulu kwa wananchi.

Wengi hapana. Matendo na tabia zao zinanuka. Faraja Nyalandu (Kotta) ni miongoni wa wasichana wachache mno wanaoweza kupunguza sehemu kubwa ya kashfa ya mashindano hayo.

Kwanza toka mwaka 2004 aliponyakua taji hajawahi kukumbwa na kashfa yoyote ya ajabu. Sio madawa ya kulevya wala kupora mume wa mtu.

Amekuwa kimya, mwerevu na mwenye heshima siku zote. Kutokana na tabia hiyo ndio maana kijana mtanashati kutoka Singida, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni mbunge, alipiga goti na kuomba kumchumbia.

Sasa ni mke wa mtu huku pia akiwa mama wa familia. Mafanikio ya Faraja hayako tu katika ndoa na kutulia. Amefanikiwa kuwa mbunifu na kuja na project kabambe iitwayo Shule Direct.

Mradi huu umekuwa mkombozi kwa wanafunzi wengi kutokana na muundo wake kufanana na mitaala ya shule zetu huku akiwa kaupangilia kwa weledi na akili ya hali ya juu.

Ubunifu huu abadani huwezi kuletwa na mtu anayewaza kila siku kutoka na bwana mpya. Ubunifu huu abadani asilani hauwezi kuletwa na mtu anayetumia vinywaji na sigara zilizopigwa marufuku.

Faraja ni mfano wa mwanamke mrembo mwilini na kichwani. Bila shaka yale maswali ya Mlima Kilimanjaro uko wapi ama Ziwa Victoria linapatikana mkoa gani, alikuwa akiyachukia sana.

Bila shaka alihitaji maswali mazito mazito ya kuonesha ubunifu na ukubwa akili yake. Baada ya kuyakosa kule, sasa kaona aoneshe ukubwa na uimara wa akili yake kupitia ubunifu wenye faida.

Hapa sasa ndipo unapoweza kusifu shindano la mamisi kama lingekuwa linatoa watu sampuli ya Faraja ama Hoyce Temu mara nyingi.

Ila mashindano haya ya kutuletea watovu wa maadili na waruwaru hayawezi kumshawishi mzazi amruhusu bintiye ashiriki. Sura ya mashindano haya imebadlika na kuwa kama sehemu ya kukusanya mabinti wasiojielewa na kuwapa umaarufu ambao umaarufu huo utafanya jamii izidi kuwachukia badala ya kuwapenda.

Hongera sana dada Faraja. Mradi wako wa Shule Direct sio tu ukombozi kwa wanafunzi walio wengi ila pia umeonesha ni kwa namna gani mwanamke makini aliyepata nafasi anavyotakiwa kuwa.

Ni vile tu ndege wasiofanana hawawezi kuruka pamoja ila vinginevyo ningeomba uwapige msasa hawa mamisi skendo. Yaani raha, kule Faraja anafanya yake, huku Hoyce anasaidia jamii yake kupitia kipindi chake cha runinga.

Mjifunze basi kupitia kwao.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364