Futari Zao Mbona Freshi Tu
WAUMINI wa dini ya Kiislam kwa sasa wapo kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, moja ya nguzo muhimu katika imani ya dini hiyo.
Hiyo ni nguzo ya nne kati ya nguzo tano ambapo waumini hujizuia kula na kunywa nyakati za mchana, sambamba na kujipinda kufanya ibada ili kufanya toba na kumwomba Mungu kuwafutia madhambi waliyotenda.
Ibada hii ni masharti yake ikiwamo suala la mtu kula futari au mlo wenye chumo la halali na mojawapo ni muumini aliyefunga awe wa kike ama wa kiume kushirikiana kihalali na mume au mke aliyeoana naye na sio vimada.
Mwanaspoti linakuletea orodha ya mastaa kadhaa nchini ambao kwa sasa wanaitafuna futari yao kiroho safi kutokana na kuingia kwenye ulimwengu wa ndoa kwa kuikacha klabu ya ukapera;
Mr Blue
Mr Blue, mkali wa R&B nchini kwa sasa bwana anakula futari halali kabisa isiyo na shaka, kwani ni mume wa mtu. Mwimbaji huyo alioana na Waheeda, aliyezaa naye watoto wawili. Ndoa yao ndiyo kwanza imevuka mwaka mmoja kwani walifunga Aprili 14, 2016, hivyo ndani ya mwezi huu wawili hao… wanapeta kiulaini.
Mwana FA
Mwanahipop, MwanaFA naye hana noma wala nini kipindi hiki, kwani jamaa aliwahi mapema kubeba jiko kwa kufunga ndoa iliyoshtukiza wengi hasa ikizingatiwa kuwa aliwaaminishia mashabiki wake kuwa; ‘Bado yupo yupo sana’. MwanaFA alioana na Helga aliyezaa naye mtoto mmoja, ndoa yao ikifungwa Juni 5, 2016. Kutokana na kuaga kambili ya ukapera, MwanaFA ndani ya Mfungo huu wa Ramadhani naye mikaangizo kwa raha zake.
Luteni Karama
Unalikumbuka kundi la Gangwe Mob? Basi yule jamaa aliyekuwa akiimba na Inspekta Haruna, Luteni Karama bwana kipindi hiki wala hana presha wala kuhaha kusaka wa kumpikia futari. Karama bwana alifunga ndoa na Aisha Yasin, Mei 15, 2016 pale Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam. Hivyo katika kipindi hiki uji na futari kwake unashuka taratibu kooni bila hofu yoyote kwani, anakula cha halali kabisa.
Tundaman
Jamaa anatokea Tip Top Connections, anafahamika zaidi kwa ukali wa wimbo wake wa ‘Mama Kijacho’. Tundaman alifunga ndoa October 15, 2016 na mrembo aitwaye Sabrah, hivyo kipindi kama hiki jamaa anapeta kiulaini akila na kupakua futari na mamsap wake wa ndani. Imetulia hii.
Shamsa Ford
Malkia wa filamu, Shamsa Ford alifunga ndoa September 2, 2016 na mfanyabiashara wa maduka ya nguo Rashid Said ‘Chid Mapenzi’.
Ingawa hivi karibuni mumewe alipata matatizo, lakini kisheria bibie huyo anakula futari yake kihalali kabisa na hana presha yoyote maana yuko na wake ati.
Riyama Ally
Mtayarishaji na msanii wa filamu, Riyama Ally naye kipindi hiki hana hofu yoyote katika kuipata riziki yake kihalali, kwani bibie huyo alifunga ndoa Juni 16, 2016 na mume wake ambaye pia ni msanii chipukizi wa muziki, Leo Mysterio. Wawili hao waliamua kukata mzizi wa fitina kwa kuchoka kutengana kila ifikapo mfungo wa Ramadhani, lakini sasa wakielekea ndani ya mwaka mmoja wa ndoa yao, wapo freshi wanapika na kupakua futari zao freshi kabisa bila mchecheto.
Nuhu Mziwanda
Jamaa ni kama alishtuka fulani hivi, kwani mwimbaji huyo wa Bongofleva na mkali wa ‘Msondo Ngoma’ na ‘Jike Shupa’, Nuh Mziwanda aliamua kutuliza akili baada ya kutemana na Shilole na fasta akaoana na Nawal.
Ndoa yao ilifungwa Novemba 10, 2016 yaani ndio kwanza inaingia nusu mwaka sasa, hivyo ile presha aliyokuwa nayo zamani imetoweka katika Mfungo wa Ramadhani wa mwaka huu.
Mkono Mkonole
Mchekeshaji huyo naye mjanja kwelikweli, kwani baada ya kuona kila mfungo wa Ramadhani ukifika anawekwa roho juu, aliamua kukata mzizi wa fitina kwa kufunga ndoa. Ndoa yake aliifunga Mei 15, 2016 akimuoa bibie Sabrina Ally, hivyo kipindi hiki kwao kila kitu kipo poa sana, mapochopocho ya halali kabisa.