-->

Gabo, Miaka 12 Kwenye Ndoa

MASTAA wengi ulimwenguni wamekuwa wakishindwa kudumu kwa muda mrefu kwenye ndoa zao. Ni wachache walioweza kukaa na wenzi wao kwa zaidi ya miaka mitano kabla ya kuvunjika.

Hapa Bongo, miongoni mwa mastaa walio kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka kumi ni Salim Ahmed ‘Gabo’ ambaye amefanya vizuri kwenye sinema nyingi zikiwemo Bado Natafuta, Safari ya Gwalu, Big Surprise na Kona.

Gabo mwenye miaka 12 sasa kwenye ndoa yake na mkewe Fatma, wakiwa na watoto wawili – Salha na Athuman, amefunguka mengi kwenye exclusive interview na Swaggaz ambapo aliweka wazi mambo mengi kuhusu maisha yake ya kiuhusiano na uhusiano kwa ujumla.

Swali la kwanza kumuuliza lilikuwa ni tukio gani lililowahi kutokea kwenye maisha yake ya kiuhusiano, ambalo hawezi kulisahau.

Huyu hapa Gabo anajibu: “Lipo jambo moja siwezi kulisahau kabisa… kuna binti aliwahi kuwa mpenzi wangu, mapenzi yalikuwa motomoto na sote tulikuwa na matarajio makubwa ya kuishi pamoja.

“Matarajio yalikuwa makubwa sana, na tulizama mapenzini hasa, lakini haikuwa hivyo. Nikaja kuoa mwanamke mwingine kabisa. Kwa namna mapenzi yetu yalivyokuwa ilikuwa vigumu sana kufikiri labda tusingeoana.

“Nilitegemea angekuwa mke wangu, lakini haikuwa hivyo. Hivi ninavyoongea na wewe, yeye anaishi Ujerumani na ameolewa na mwanamume mwingine. Mimi nina mke wangu na yeye ana mume wake, maisha yanaendelea.”

Alipoulizwa iwapo anaumizwa na tukio hilo na kwamba alitamani mwanamke huyo awe mkewe, alijibu: “Hapana! Ipo tu kwenye kumbukumbu kwa sababu kwa namna ilivyokuwa haikuwa rahisi kuamini kilichopo sasa hivi, lakini nafurahia ndoa yangu.”

ANATUMIA MKWANJA KIASI GANI KWA MTOKO MMOJA NA MKEWE?

“Ni vigumu kupanga na kwakweli Kibongobongo wengi huwa hawapangi, nikisema huwa napanga nitakuwa nadanganya. Matumizi hutokana na mahali tunapokwenda na vitu tutakavyotumia.

“Naweza kumchukua wife kwa lengo la kwenda naye Kilimanjaro Kempiski kupata dinner, bei haitakuwa sawa na kwenda sehemu kama Coco Beach kwa mfano. Lakini inawezekana wakati wa kurudi, wife akashauri tuwachukulie watoto koni na vitu kama hivyo.

“Muhimu ninapotoka na wife, huwa nahakikisha ninakuwa na pesa kwenye waleti yangu angalau laki nne (Tsh. 400,000), kwenye gari pia nakuwa na pesa kidogo na hata kwenye simu. Kifupi sina bajeti maalumu ninapokuwa na mtoko na mke wangu,” anasema Gabo.

KWANINI NDOA NYINGI ZA VIJANA WA SIKU HIZI HUVUNJIKA MAPEMA?

“Waswahili wanasema, asiyefunzwa na mama atafunzwa na ulimwengu. Hii ndiyo sababu kubwa zaidi ya tatizo hili. Vijana wetu hawapati mafunzo kutoka kwa wazazi tena, matokeo yake dunia ndiyo inawafunza.

“Dunia ni pamoja na huu utandawazi ambao naona umewachizisha vijana wengi. Wapo vijana ambao hata ukimwuliza ngariba wake ni nani, hajui. Pengine hatajua hata maana ya ngariba.

“Yale mafunzo ya jando na unyago kwa sasa yamepungua na sehemu nyingine hakuna kabisa. Hilo ndiyo tatizo letu kubwa. Unakuta mtu anampeleka mke wake disko, anategemea nini?

“Siku akimwambia twende, baba akawa na dharura, mama akitaka kwenda peke yake itakuwaje? Tumesahau mila zetu kaka. Mimi ndoa yangu ina miaka 12 sasa na ipo imara, ni kwa sababu nimepata mafunzo hayo, najivunia kwa kweli.”

KOSA GANI AKIFANYIWA NA MKEWE ATAMUACHA?

“Dharau ndiyo kosa kubwa zaidi kwangu. Ujue dharau huzalisha mambo mengi, mfano usaliti. Mwanamke akishakudharau ni rahisi kuwa na mwanaume mwingine. Siku nitakayokugundua mke wangu wa ndoa ana mwanaume mwingine ndiyo utakuwa mwisho wetu.

“Mwanamke akishakuwa na mtu mwingine maana yake heshima hakuna tena, heshima ikitoweka ni dhahiri hata upendo nao utakuwa umetoweka moyoni mwake. Basi nasitisha tu ili kumpa nafasi aendelee na yake.”

AKIMKUTA MKE WAKE AMENUNA NA HAJAMUUDHI, ATACHUKUA HATUA GANI?

“Matatizo ni sawa na dharura. Jukumu la kwanza ni kuhakikisha namrudisha mwenzangu katika hali ya kawaida, akishakuwa sawa nitamkabili. Nitazungumza naye kwa upole, nijue tatizo ni nini.

“Nikishajua nitamfundisha njia bora za kukabiliana na matatizo badala ya kununa. Lakini kutokea hapo nitafuatilia kwa karibu zaidi nyendo zake ili kubaini kama kuna la zaidi linalomsumbua. Ni jukumu langu kama baba kuhakikisha mke wangu anakuwa mwenye furaha.”

AKIPEWA OFA YA KWENDA KUPUMZIKA MJI WOWOTE DUNIANI NA MKE WAKE, ATACHAGUA WAPI?

“Dubai. Nimechagua huko kwa sababu ule mji bwana nadhani umejengwa maalumu kwa ajili ya watu kustarehe. Kuna vitu vingi sana ambavyo havipo mahali popote zaidi ya Dubai.

“Zipo starehe ambazo hazipo mahali pengine popote duniani, lakini pale unazikuta. Aisee lazima nichague Dubai na siku nikienda kwa mapumziko, nitaitendea haki Dubai,” anasema akitabasamu.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364