-->

Gigy Money, Lulu Diva, Amber Lulu… Bongo Fleva Kunani?

MFUMO dume uliminya vipaji vya watoto wa kike kuchanua kwenye Bongo Fleva na kufanya wawe bidhaa adimu licha ya kuwa na uwezo wa kufanya kile wasanii wa kiume wanafanya.

Lakini mwaka 2016 tulishuhudia hali hiyo ikitoweka na wasanii wa kike wakiongezeka kwa kasi na wengine wakitoka kwenye tasnia za filamu na utangazaji na kuingia kwenye muziki.

Mifano ipo mingi, lakini Shilole, Snura na Feza Kessy wanaweza kuwawakilisha wengine. Kila mmoja ana sababu zake za kutupa karata zake kwenye Bongo Fleva ila leo Swaggaz tumeona tuwatazame warembo watatu wanaozungumzwa zaidi kutokana na uamuzi wao wa kujiingiza kwenye muziki.

Hawa ni Gigy Money, Lulu Diva na Amber Lulu.

KWANINI WAO?

Lulu Diva, Amber Lulu na Gigy Money ni warembo wanaozipendezesha video za muziki wa Bongo Fleva (Video Vixen). Kila mmoja amejizolea umaarufu kutokana na kazi za video alizozifanya.

Japo kazi ya kuuza sura kwenye video hawajaacha lakini hivi sasa wamewekeza nguvu zao kwenye muziki, jambo linaloibua mjadala kitaa.

Kuna kundi la watu wanaosema warembo hawa wamebugi kuingia kwenye muziki huku wengine wakiwapongeza kwa kucheza vizuri na fursa ili wajiongezee mkwanja.

Gigy Money

Kati ya warembo hawa watatu, Gift Stanford ‘Gigy Money’ ndiye aliyeanza kufanya muziki. Ngoma yake ya kwanza iliyotoka mwaka 2015 iliitwa Alela.

Mwanzoni mwa mwaka jana akaachia wimbo unaoitwa Majojorijo na akafunga mwaka 2016 kwa Supu, ngoma aliyomshirikisha Matonya.

Mrembo huyu aliyejizolea umaarufu kwa kunogesha video za muziki wa Hip Hop, Gigy Money amewahi kuuza sura kwenye video za wasanii kama Ney wa Mitego (Shika Adabu Yako), Darassa (Too Much) Dully Sykes (Inde) na Godzilah (I Get High).

Lulu Diva

Anaitwa Lulu Abbas ‘Lulu Diva’, amewahi kuonekana kwenye video kadhaa za wasanii wa muziki Tanzania ikiwemo ile ya msanii aliyewahi kusimamiwa na Wema Sepetu – Mirror wimbo unaoitwa Naogopa aliomshirikisha Baraka Da Prince.

Mara nyingi amewahi kulalamika malipo kiduchu wanayolipwa warembo hao na wasanii wa muziki. Akaona isiwe tabu kwa sababu kipaji na uwezo wa kuimba anao ikamlazimu kumtafuta Barnaba na wakafanya ngoma kali inayoitwa Milele.

Mwaka 2016 ulikuwa na neema kwake kwani wimbo huo ulioandikwa na Barnaba mwenyewe ulimpa umaarufu hali kadhalika video aliyoifanya Afrika Kusini ilimpa nafasi ya kutazamwa kama msanii wa muziki na siyo Video Viven tena.

Amber Lulu

Jina lake ni Lulu Mkongwa maarufu kama Amber Lulu aliyejizolea umaarufu baada ya picha zake tata kusambaa kwenye mitandao ya kijamii huku mwonekano wake ukifanana na mwanamitindo Amber Rose.

Akaanza kuonekana kwenye video za muziki mfano ni ile Inde ya Dully Sykes huku akiendelea kufanya michongo ya umodo na kuhosti matukio mbalimbali ya burudani.

Mwaka 2016 aliingia kwenye orodha ya Mavideo Vixen waliotupa karata zao kwenye muziki huku akidai hawezi kuiacha kazi yake ya awali na kikubwa anachoangalia ni mkwanja.

Anamiliki singo inayoitwa Watakoma aliyomshirikisha rapa Country Boy. Inafanya vizuri kwenye vituo vya redio huku video ikiwa inasubiriwa kwa hamu.

Kunani Bongo Fleva?

Hakuna sanaa inayolipa hivi sasa kama muziki, kwenye filamu hakupo vizuri, soko lake limeyumba vibaya ndiyo maana tunaona wengi wakitoka huko na kuingia kwenye Bongo Fleva.

Mavideo Vixen hawa licha ya kuuza sura kwenye video za muziki, wamecheza vyema na fursa ya ukubwa wa majina yao, wakaona siyo vibaya wakiingia kwenye muziki huku wakiendelea kufanya michongo mingine inayokuja mbele yao.

Chukueni tano.

Na Christopher Msekena-Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364