Gwajima Kumuombea Lissu
Mchungaji Mchungaji Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima amefunguka na kusema kuwa siku ya Jumapili atafanya maombezi maalum kwa afya ya Mbunge Tundu Lissu ambaye jana alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa Dodoma nyumbani kwake.
Mchungaji Gwajima amesema kuwa atatumia misa hiyo kulaani vikali kitendo cha kinyama alichofanyiwa Tundu Lissu na watu hao wasiojulikana ambao waliweza kupiga gari lake zaidi ya risasi 30 huku risasi tano ndizo ziliweza kumjeruhi Mbunge huyo.
“Jumapili hii Septemba 10, 2017 nitaongoza maombi maalumu ya kuombea Afya ya Mhe. Tundu Lissu na kulaani Vikali kitendo cha Kikatili na Kinyama alichofanyiwa. Maombi haya yatafanyika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Ubungo Dar es Salaam tunawakaribisha wote watakaopenda kuungana nasi katika maombi haya” aliandika mchungaji Gwajima kupitia ukurasa wake wa facebook
Mchungaji Gwajima amekuwa akilaani mambo mbalimbali ambayo huwa yanatokea katika nchi kupitia misa mbalimbali ambazo huwa anafanyia katika kanisa lake hilo ikiwa pamoja na kuombea taifa amani na usalama.