-->

Hali ya Bulaya bado tete

Dar es Salaam. Hali ya Mbunge wa Bunda Ester Bulaya aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH ) imeelezwa kuwa bado ni tete.

Hali hiyo ni kufuatia tatizo la kupumua alilolipata baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya Kituo cha Kati cha Polisi mjini Tarime.

Mwananchi lilifika katika wodi namba 18 Sewahaji alipolazwa mbunge huyo, lakini lilishindwa kuwasiliana naye kutokana na hali yake.

Hata hivyo wauguzi wa wodi hiyo hawakutaka kuruhusu mtu yeyote kuingia katika chumba alicholazwa Bulaya.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee anayemuuguza kwa sasa hospitalini hapo, jana aliliambia Mwananchi kuwa haiwezekani mtu yeyote kuingia katika chumba hicho kwa sasa.

“Hapana hali yake si nzuri kwa sasa hawezi kuingia yeyote huku tafadhali, labda tuombe Mungu kesho hali yake ikiimarika mnaingia,” alisema Halima Mdee huku akitoka katika chumba namba 4 alicholazwa mbunge huyo.

Akizungumza Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Stephen amesema Bulaya alifikishwa hospitalini hapo jana saa tano usiku akitokea Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara.

“Tulimpokea jana usiku na alipatiwa matibabu hali yake kwa sasa yupo vizuri kwani ameshaanza kupatiwa vipimo mbalimbali,” amesema Stephen.

Mbunge huyo alianza kujitambua tangu alipofika hospitalini baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya Kituo cha Kati cha Polisi mjini Tarime.

Bulaya amesota rumande tangu akamatwe Ijumaa ya Agosti 18 kwa madai ya kuingia jimbo la Tarime na kufanya shughuli za kisiasa kwa kutoa msaada wa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi jimboni humo baada ya kualikwa na mbunge mwenzake Ester Matiko.

Wakati Bulaya akikamatwa na kusota mahabusu kwa kushiriki shughuli za maendeleo na kusalimia wananchi kwenye jimbo la uchaguzi lisilo lake, matukio ya wabunge wa majimbo kuwaalika wenzao kusaidia juhudi za maendeleo na kusalimia wananchi katika mikutano ya hadhara yameshuhudiwa sehemu mbalimbali nchini.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364