-->

Hamisa Mobeto Afunguka Penzi Na Diamond, Ujauzito

TANGU ilipoachiwa video ya kibao cha Salome ya mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ akishirikiana na Rayvanny, kulianza maneno kuwa Diamond anatoka kimapenzi na mwanamitindo mwenye mvuto Hamisa Mobeto.

Hamisa Mobeto

Hamisa alikuwa mmoja wa video vixens waliopamba video hiyo kali iliyomrudisha mwanamama Saida Karoli kwenye game baada ya kujipa likizo kwa muda mrefu.

Lakini wiki kadhaa mbele, Hamisa alionekana kuwa na ujauzito na hapo ndipo maneno yalipozidi kwenda mbali kwamba, mhusika wa mimba hiyo ni Diamond.

Wakati madai hayo yakizidi kupamba moto kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na baadaye magazetini, Hamisa hakuwahi kuzungumza lolote kuhusiana na madai hayo.

Swaggaz la Mtanzania limefanikiwa kuzungumza na Hamisa mwenyewe ambaye anafafanua kila kitu kuhusiana na madai hayo.

HAMISA AFUNGUKA

Akizungumza kwa kujiamini mbele ya mwandishi wa Swaggaz, Hamisa alisema ni kweli amesikia maneno mengi kuhusu mimba yake akihusishwa mwanamuziki Diamond, lakini ukweli ni kwamba mimba yake ina mwenyewe na siyo Diamod kama inavyosemwa.

“Huu uvumi unataka niweke wazi maisha yangu, hilo halitajitokea kwangu kwani mtu akishaumwa na nyoka akimwona mjusi anamwogopa. Baba wa mtoto wangu mtarajiwa namjua mimi na familia yangu nadhani inatosha.

“Sidhani kama ni lazima nimtaje kwenye media, lakini wale wanaosema ni Diamond, tafadhali sana siye. Baba wa mtoto wangu yupo na sio matangazo ya biashara kila mtu amjue mpenzi wangu.

“Hao wanaotutukana mbona wao maisha yao wameyaweka siri au mimi tu ndiyo nijianike? Siwezi kufanya hivyo. Najua nachokonolewa ili niseme… sitasema,” anasema Hamisa.

Akizidi kujipambanua, Hamisa amesema hivi sasa yeye ni mtu mpya na kwamba mashabiki wake watamjua kwa kazi zake na siyo maisha yake binafsi kwa sababu ameshajua madhara ya kuweka maisha yake hadharani.

“Maisha yangu binafsi yatabaki kuwa yangu mimi mwenyewe ila ya kibiashara yatajulikana na kila mtu. Mimi kwa sasa sihitaji sifa za kijinga, nahitaji mashabiki wangu wafahamu nafanya nini katika jamii na wanishabikie hivyo, siyo kwa maisha yangu binafsi,” anasema na kuongeza:

“Kuruhusu ushabiki katika maisha yako binafsi hasa ya mapenzi ni kujijengea uadui na marafiki wa uongo ambao wengi wao wanakuja kinafiki na kujifanya wanakufahamu kiundani au mpenzi wako kumbe ni waongo, wanataka kuwavuruga na wakifanikiwa hutawaona.”

 

HAMISA WA KAZI

Akionyesha kuwa serious katika kile alichokiita msimamo wake mpya, Hamisa alitumia nafasi hiyo kuwaomba Watanzania na vyombo mbalimbali vya habari washabikie kazi zake za kimataifa anazofanya nyingi kwa muda mrefu sasa, ambazo zinailetea sifa nchi kwa kuwa anabeba bendera ya Taifa.

“Ningependa sana kuhojiwa kwa kazi ninazofanya nje ya nchi, siyo maisha yangu binafsi. Mimi siitwi nje kama Hamisa na mahusiano yangu bali Hamisa mwanamitindo kutoka Tanzania.

“Hata nikipanda jukwaani situmii Hamisa, linatumiwa jina la Tanzania sasa hapo vipi kama nitatangazika kwa hayo au vitu vingine vya kuungaungua? Haina maana. Narudia kusema, katu sitamtaja mpenzi wangu,” anasisitiza.

HAMISA NI NANI?

Inawezekana unamfahamu juujuu tu kama Hamisa Mobeto, mwanamitindo maarufu na muuza sura kwenye nyimbo za wasanii wa Bongo Fleva, hapa Swaggaz linakujuza.

Anaitwa Hamisa Hassan Mobeto ambaye alizaliwa mwaka 1994 mkoani Mwanza, kabila lake ni Mnyamwezi.

Kitu cha kwanza kumwingiza kwenye ulimwengu wa mastaa wa Bongo ni pale aliposhiriki na kuibuka mshindi wa Shindano la Miss XXL BACK TO SCHOOL BASH mwaka 2010 lilioandaliwa na Kipindi cha XXL cha Radio Clouds FM cha jijini Dar es Salaam.

Mwaka 2011 Hamisa alishiriki Miss Dar Indian Ocean na kufanikiwa kuchukua namba 2, iliyompa tiketi ya kushiriki Miss Kinondoni ambapo pia alikuwa mshindi wa pili.

Ushindi huo ulimpa tiketi ya kupanda kwenye Fainali za Miss Tanzania na kuishia nusu fainali ambapo mlimbwende aliyeibuka Miss Tanzania mwaka huo alikuwa ni Salha Israel.

Mwaka 2012 Hamisa alishiriki mashindano ya Miss Univeristy Africa na kufanikiwa kufika 10 Bora. Tangu hapo amekuwa gumzo kwenye mitindo na filamu. Ameshiriki kazi kadhaa za wasanii mbalimbali wa Bongo.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364