-->

Hatimaye Mashabiki na Wapenzi wa Lulu Kuanza Kumuona

Zikiwa zimepita siku 54 tangu muigizaji wa filamu bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, sasa mashabiki wake wataanza tena kumuona kupitia tamthiliya ya Sarafu inayotarajiwa kuanza kurushwa kuanzia Januari 10 siku ya Jumatano.

Sarafu ni moja ya tamthiliya zitakazoonyeshwa katika king’amuzi cha DSTV kupitia chanel yao ya Maisha Magic Bongo ambapo itakuwa inarushwa siku ya Jumatano na Alhamisi.

Katika tamthiliya hiyo ambayo msimu wake wa kwanza utaenda mpaka Machi mwaka huu, imesheheni waigizaji mbalimbali maarufu, ambapo mbali na Lulu wapo Funga Funga(Jengua), Mzee Chilo, Hemed Suleiman, Irene Uwoya, Idris Sultan, Yusuph Mlela na mastaa wengineo.

Ndani ya tamthiliya hiyo Lulu anaigiza kama mtoto wa familia tajiri ya Mhandisi Sanga akiwa anatumia jina la Jack huku mama yake akiwa ni muigizaji wa siku nyingi Suzan Lewis ‘Natasha’.

Uzinduzi wa tamthiliya hiyo uliofanyika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, uliendana sambamba na uzinduzi wa tamthiliya nyingine ya Sarafu ambapo baadhi ya wadau waliweza kushuhudia moja ya kipande alichoigiza Lulu, ambacho alionekana kukitendea haki.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliokiona kipande hicho walikuwa na maoni yao kuhusu namna walivyojisikia baada ya kumuona msanii huyo akiwemo mrembo Wema Sepetu, ambaye alisema kipande hicho kimemuhuzunisha kwani alitamani naye angejumuika nao siku hiyo lakini kutokana na matatizo aliyoyapata imekuwa ngumu.

Kwa upande wa Natasha, amesema yeye sehemu hiyo ilipofika alitamani hata kutoka nje ya ukumbi, kwa kuwa yeye kama mama inamuumua kwa mtihani anaopitia Lulu kwa sasa ukilinganisha na umri wake mdogo aliokuwa nao.

Novemba 13, mwaka jana, Mahakama Kuu ilimhukumu kwenda jela miaka miwili Lulu kutokana na kukabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa anaendesha kesi hiyo na kusema kwamba mshtakiwa amekutwa na hatia ya kuua bila kukusudia kutokana na ushahidi wa mazingira.

Chanzo: Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364