-->

Huko Kwenye filamu za Kibongo Hakukaliki

FILAMU za Kibongo kwa sasa zimedorora sana. Takriban miaka miwili hali ya soko la filamu hizo imekuwa ikisuasua, lakini kwa 2017 limedorora kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hata wasanii wake wanaishi kwa kubangaiza.

Wasanii wa Bongo Movie, JB ,Ray na Marehemu Kanumba

Kipato kupitia tasnia hiyo kimekuwa muhali, kiasi cha kuleta mashaka makubwa kwa baadhi ya wasanii wakiamua kubadilisha upepo ili kupisha jinamizi lililopo sasa lipite kabla ya kurejea mambo yakiwa shwari.

Kumekuwa na mitazamo tofauti juu ya hali hiyo, wanunuzi wa kazi hizo na hata wasambazaji kila mmoja amekuwa na hoja zake kubwa ikielezwa kifo cha nyota wa zamani wa fani hiyo, Steven Kanumba ni tatizo lililochangia kuzika filamu. Wanadai kifo chake kimechangia kushusha soko la filamu za Kibongo wakiamini kama angekuwa bado yu hai angeendeleza moto wake wa kuitangaza tasnia hiyo nje ya nchi kama alivyofanya na kuipaisha kimataifa.

Kanumba alifariki mwaka 2012 ambapo kila sinema kwa wakati huo ilikuwa ikiuza tofauti ilikuwa ni uuzaji wa nakala nyingi tu huyo ameuza nakala kadhaa na yule kamzidi kwa kuuza nyingi lakini wadau wa filamu wanasema kuwa tangu filamu na muziki virasimishwe hali ni mbaya kwa watu wa filamu.

Mwanaspoti limefanya utafiti mdogo kubaini kudodora kwa soko la filamu Bongo, kuna mambo kadhaa yaliyolifikisha soko la filamu kushuka, ikiwa kiuchumi, ubora wa kazi, Tafsiri ya sinema za nje, wauzaji wa kazi za nje na kutegemea wafanya maamuzi kuwa sehemu moja yaani Kariakoo.

KIUCHUMI

Kwa sasa hali ya kiuchumi kwa wapenzi wa filamu ambao sehemu kubwa ni wale waliojiajiri haipo sawa hivyo si rahisi sana mtu kununua filamu moja kwa kiasi cha Tshs. 3,500 wakati akitoa Tshs. 700 hadi 1,000 anapata tamthilia yenye sehemu nyingi kuliko filamu moja tena iliyogawanywa mara mbili.

Hali hiyo imewafanya watengenezaji wa filamu za ndani kujikuta wanakosa wateja wa kununua kazi zao ambazo zinaonekana ni gharama kuliko zile za kutoka nje ambazo zinauzwa kwa bei nafuu zaidi lakini huku zikiwa zimesheheni ustadi mkubwa kwa kila Nyanja.

Wasanii wa Bongo Movie

Wasambazaji wa ndani wanalalamika kuwa ushindani haupo sawa kwani sababu inayowafanya wao wauze bei kubwa ni kulingana na uwepo wa kodi lukuki na taratibu za kisheria ambazo wale wauzaji wa filamu za nje hawawajibiki nalo, sinema zao hazikaguliwi, hazilipiwi kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kupewa Stempu zinazotambulisha mlipa kodi katika sinema.

“Sisi tunabanwa kodi ni nyingi sana nikienda Cosota nalipia, baada ya hapo nakwenda Bodi ya Filamu kukagua sinema yangu nalipia kwa kila dakika 1,000 nitokea hapo naenda TRA nanunua Stempu nitauza Dvd 700?,” anauliza Athuman msambazaji.

Muasisi wa tafsiri alikuwa marehemu Lufufu ambaye alikuwa kama msimuliaji tu na kuteka hisia za watazamaji baadae wakajitokeza wengi kuweka umaridadi zaidi lakini wapo wanaotafsiri kwa kuweka sawa neno kwa neno wasambazaji wanasema hawa wameua biashara kwani wengi wamevutiwa sinema hizo kusikia lugha waliyoizoea.

UBORA WA KAZI

Bila shaka ni ukweli usiopingika kuwa sinema kutoka nje zina ubora zaidi za hapa Bongo hivyo imekuwa ni vigumu sana mtu kununua kazi za ndani kuliko za nje hivyo wateja pekee wa kazi za ndani ni watu wa Maktaba za video na wamiliki wa Mabanda ya kuonyeshea Video huku kundi lililobaki wakisubiri waone kwanza ndio wanunue.

Wasanii wa Bongo Movie

Changamoto ya pili ni kuwa na wasanii ambao wanarudia kwa kila sinema huku hadithi zikikosa ubunifu na watazamaji wakisalia kuona ni kama vile wasanii wanabadili nguo, uhusika na mandhari huku hadithi zikiwa zile zile wauzaji wanasema huko ni kudumaa kwa sanaa ambayo haitoi fursa kwa chipukizi kuingia.

WADAU WANASEMAJE

Rais wa Shirikisho la Filamu, Simon Mwakifwamba anasema kuwa awali kulikuwa na maduka 75 yakiuza filamu za Kibongo kwa sasa maduka ya kuuza filamu Kariakoo yameongezeka na kufika 214 huku yaliyobaki yakiuza filamu za Bongo ni mawili tu mengine yote yakiuza kazi nje.

“Hatupingi watu kuuza filamu za nje lakini tunataka wafuate utaratibu kama sisi walipe kodi wakaguliwe ili kulinda maadili wafuate sheria za nchi siyo wao waachiwe sisi tubanwe,”alisema Rais Mwakifwamba.

Waziri mwenye dhamana na Sanaa, Nape Nnauye, alifanya oparesheni akiwashirikisha wenye mamlaka TRA, Bodi ya Filamu, Cosota, Watoa leseni vyombo vya usalama na kuwakamata wale wote ambao wanakiuka taratibu kwa kuuza sinema ambazo hazijakaguliwa wala kulipia ushuru na kuwafananisha na wahujumu uchumi.
Kwa sasa maduka mengi Kariakoo yamefungwa na kubaki mawili tu huku yale ambayo hayajafuata sheria za uuzaji kazi ndani ya nchi sheria ya filamu na michezo ya kuigiza mwaka 1976 namba 4 imeipa mamlaka Bodi ya Filamu kukagua na kutoa madaraja kwa ajili ya kuonyeshwa.

Wadau wamefurahishwa na oparesheni hiyo kwa sababu wauzaji wa kazi za nje wamekuwa wakionekana hawawezekani kwani oparesheni za awali ilikuwa kila maduka yanapofungwa siku ya pili tu yanakuwa wazi na kujenga taswira mbaya kama kuna mambo ya kuzembea kuhusu kuwalinda walipa kodi.

Mwanaspoti

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364