JB Afungukia Soko la Kazi Zake
Msanii maarufu wa filamu hapa nchini, Jacob Steven ‘JB’ amefunguka na kuweka wazi kuwa tangu ameanza uigizaji hajawahi kupata changamoto ya soko ya kazi zake kama ambavyo baadhi ya wasanii wa filamu bongo wamekuwa wakilalamika.
JB ambaye mpaka sasa ametengeneza filamu zaidi ya 40 ikiwa ni pamoja ya zile kazi alizoziandaa na kuigizwa na watu wengine anasema anashukuru Mungu hajawahi kupata changamoto hiyo na siku zote kazi zake zimekuwa zikifanya vizuri kila alipoingiza sokoni.
“Sijawahi kupata matatizo ya soko katika kazi zangu, kwa hiyo lazima niwe mkweli sijawahi kupata matatizo ya soko kazi zangu zimekuwa zikiuzwa na nilikuwa napata mauzo mazuri kwangu hivyo hilo lazima nimshukuru Mungu, kizuri zaidi niliweza kutengeneza kazi ambazo mimi sikuigiza mimi ila zilifanya vizuri pia, labda mwaka 2003 wakati natoa kazi yangu ya kwanza kidogo lakini baada ya hapo nilipata mkataba wa kudumu, kwa hiyo mimi binafsi sijawahi kupata matatizo ya soko” alisema JB
Mbali na hilo JB alizungumzia kitendo cha rushwa ya ngono katika tasnia ya filamu na kusema ni producer mjinga ambaye atakubali kumuingiza muigizaji kwenye filamu yake kwa ajili ya rushwa ya ngono ilihali anajua wazi kuwa mwigizaji huyo hana uwezo na kusema kwa kufanya hivyo ina maana atakuwa ameiharibu kazi yake hiyo kwa kuwa haiwezi kuwa kazi nzuri kwa kuwa amewaweka watu wasiokuwa na uwezo wa kuigiza.
eatv.tv