JB Awachana Wakina Gabo na Duma
Muigizaji mkongwe nchini Jacob Stephen ‘JB amefunguka na kuwachana Gabo Zigamba pamoja na Duma kwamba njia pekee ya kufahamika ni kupitia kazi zao wanazozifanya na wala siyo masuala ya ugomvi baina yao.
JB amesema hayo kupitia kipindi cha eNewz kutoka EATV, baada ya msanii Duma kutoa kauli yake iliyokuwa inamponda Gabo siku za hivi karibuni kwa kudai hana muonekano wa kuwa ‘star’ kwa maana anarudi nguo kuvaa katika ‘show’ zake, pamoja na kuwa ndiye chanzo cha tasnia ya filamu kulega lega kwani ameaminiwa na watanzania wengi lakini ameshindwa kuwatendea haki mashabiki zake jambo ambalo likazua mada ndefu katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Vijana wana njia nyingi za kulishika soko si unajua tena ujana, lakini sidhani kama wataweza kuleta madhara ama wakagombana kwa kitu kama hicho. Tupo wazee tutahakikisha hawafiki huko, kwa hiyo wapenzi na mashabiki zao wasiwe na wasiwasi”, amesema JB.
Pamoja na hayo, JB amesema moja ya kazi ya wazee kuwepo katika tasnia ya filamu ni kuhakikisha amani inapatikana kwa vijana hivyo atahakikisha kila kitu kitaenda sawa kwa vile yeye bado yupo.
“Kwenye ‘movie’ muda mrefu tumekuwa kimya sana lakini kama wao wameamua kuchangamsha soko kwa kutumia njia hiyo ni sawa, ila nawakumbusha pia ‘the best way’ ya wao kufahamika ni kupitia kazi zao wao wenyewe maana sisi tunaenda ku-staff, hii ni nafasi yao sasa ya kufanya vizuri na kutambulika kupitia kazi zao. Gabo ni mmoja katika ya waigizaji bora tuliyokuwa nao na Duma ni muigizaji mzuri tuliyokuwa nao wanaweza wakawa wanafanya vituko vyao huwezi kuwazuia kwa sababu miaka yao inawaruhusu”, amesisitiza JB.
Mtazame hapa chini msanii Jacob Stephen ‘JB akitoa maneno yake ya busara kwa vijana wake wa bongo movie.