Kajala Aenda Kumlilia Mumewe Gerezani!
Staa wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja ‘Kay’ hivi karibuni amekwenda kumlilia mumewe, Faraji Chambo anayetumikia kifungo cha miaka kumi na mbili gerezani.
Kwa mujibu wa chanzo makini ambacho ni mtu wa karibu wa Kajala, mwanamama huyo alitinga kwenye Gereza la Ukonga, Dar alikofungwa mumewe ambapo alipata nafasi ya kumjulia hali kisha kumwaga machozi akimuonea huruma anavyosota gerezani hasa akikumbuka walivyokuwa wakiishi kabla ya msala huo.
Katika safari hiyo, Kajala aliongozana na mwanaye, Paula Paul na mdogo wake Kajala ambao ndiyo waliokuwa wakimtuliza staa huyo ambaye alisababisha mumewe naye kutokwa machozi.
Akizungumzia ishu hiyo, Kajala ambaye wiki iliyopita alizindua filamu yake kali ya Sikitu alisema kuwa ni utaratibu wake wa mara kwa mara kwenda kumjulia hali mumewe huyo ila mara zote huwa anakwenda kimyakimya.
“Huwa nakwenda mara nyingi tu sema ndiyo hivyo huwa sipendi kuongozana na msururu mrefu, namshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema Kajala. Machi 2013, Kajala na Faraji walihukumiwa ambapo Kajala alitakiwa kwenda jela miaka mitano au faini ya shilingi milioni kumi na tatu na mumewe miaka kumi na mbili au faini ya shilingi milioni mia mbili kwa kosa la kutakatisha fedha haramu kwenye Benki ya NBC, Tawi la Dar.
Hata hivyo, Faraji alishindwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kujikuta ‘akiozea’ gerezani huku Wema Sepetu ‘Madam’ akimlipia Kajala faini ya shilingi milioni kumi na tatu, iliyomnusuru kwenda jela.
Chanzo:GPL