-->

Lowassa Afika Polisi, Ulinzi Mkali, Atakiwa Kurudi Tena Julai 13

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amewasili katika makao makuu ya Jeshi la Polisi leo (Alhamisi) kama alivyoelekezwa siku ya Jumanne wiki hii baada ya kuhojiwa kwa saa nne.

Lowassa amewasili saa 5:52 asubuhi akiwa ameambata na viongozi wengine wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe huku ulinzi mkali ukiwa umewekwa katika makao makuu hayo.

Kando na hao walikuwepo watu wengine aliombatana nao, lakini walizuiliwa kuingia na askari walioimarisha ulinzi katika eneo hilo.

Askari hao pia waliwafukuza waandishi wa habari waliokuwa katika eneo hilo na kuwataka kusogea mbali ya viunga vya makao makuu hayo.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi Lowassa aliondoka katika makao makuu hayo huku Mbowe akieleza kuwa ametakiwa kurudi Julai 13 kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika

Lowassa alitakiwa kufika polisi leo tena kwa tuhuma za kutoa kauli ya kichochezi wakati wa futari iliyoandaliwa Juni 23 na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.

Katika futari hiyo, Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi kuhusu masheikh wa Taasisi ya Uamsho wanaoshikiliwa na magereza akidai kwamba utaratibu wa kisheria ufanyike ili kuwaachia huru masheikh hao.

Jumatatu wiki hii Lowassa alipokea wito wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz kwenda kuhojiwa juu ya tuhuma hizo na alitakiwa kuripoti saa 4 asubuhi siku ya Jumanne.

Lowassa aliwasili Jumanne saa 3:58 asubuhi kama alivyotakiwa akiwa na msafara wa magari manne ambayo yaliyosindikizwa na magari mawili ya polisi.

Alihojiwa kwa saa nne mfululizo kabla ya kuachiwa kwa dhamana saa 8:15 mchana na kuelekea nyumbani kwake, Masaki ambako alizungumza na vyombo vya habari.

Baada ya kuachiwa, wakili wake Peter Kibatala ambaye pia alikuwepo katika mahojiano hayo alisema Lowassa amejidhamini mwenyewe na ametakiwa kuripoti tena kwa DCI leo saa sita mchana ili kujua taratibu watakazoambiwa.

Kibatala alisema Lowassa alihojiwa kwa kosa la uchochezi kwa kauli yake aliyoitoa Juni 23 na kwamba baada ya kuhojiwa aliandika Maelezo ya Onyo juu ya kauli yake ambayo imetafsiriwa kuwa ni ya kichochezi.

Maelezo hayo ya onyo yanaweza kutumika dhidi ya Lowassa kama akifikishwa Mahakamani.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364