-->

Lulu Usitukane Wakunga, Uzazi Ungalipo!

KWAKO mtoto mzuri ndani ya Bongo Muvi, Elizabeth Michael ‘Lulu’. Hujambo? Habari ya huko ulipo? Wazima wote na familia yako? Shemeji yetu naye hajambo? Hongera maana naona siku hizi umeamua kumuanika hadharani.

LULU32

Ukitaka kujua afya ya mimi kaka yako, sijambo. Namshukuru Mungu, naendelea kupambana ndani ya mjengo wa magazeti Pendwa, Global Publishers Ltd. Hapa sisi ni kazi tu!

Nimekukumbuka leo kwa barua. Kitambo kidogo sijakuona. Siku hizi umekuwa mzito sana kuzurura kwenye viwanja vyetu vya kujidai. Sikulaumu katika hilo, huenda ni utaratibu mpya ambao mwenyewe umejipangia. Ni jambo zuri pia. Staa anapaswa kupotea kidogo siyo kila kiwanja awepo.

Historia ya maisha yako inaonesha umeweza kukutana na changamoto nyingi ambazo naamini zilikuwa kubwa kuliko umri wako. Umejitahidi sana kuzikabili na maisha yanaendelea vizuri, mshukuru Mungu pia kwa hilo. Si akili zako bali ni kwa neema na rehema zake.

Madhumuni ya mimi kukuandikia barua hii, nina jambo. Nataka kukumbusha kwamba; usitukane wakunga wakati uzazi ungalipo. Sikufurahishwa na kitendo cha wewe kuwatukana waandishi wa Global Publisher hivi karibuni.

Wewe na vyombo vya habari (hususan Global) ni kama chanda na pete. Ukubali ukatae, magazeti yake yamechangia kwa kiasi kikubwa sana kukufikisha ulipo leo. Hata kama yanauza kupitia habari za mastaa lakini mchango wake katika maendeleo yenu ni mkubwa.

Kwa kuandika habari zako, zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuwashawishi Watanzania kukufuatilia. Kujua unafanya nini kwa wakati husika na kisha kukusapoti kwa kununua kazi zako.

Hata pale ulipopata majanga mbalimbali, kama kampuni kwa namna moja au nyingine iliweza kutoa mchango wake. Hata usipokiri hilo hadharani, lakini moyoni unajua. Siwezi kufafanulia kila kitu lakini ukweli unaujua.

Katika hilo si wewe tu, hata familia hususan mama yako anajua mchango wa Global katika maisha yako. Haujavuka mto kiasi cha kutukana mamba. Unaanzaje kuwatukana waandishi wa Global? Ujasiri huo unautoa wapi? Mafanikio gani yanayokupa jeuri?

Unawatukana waandishi wa kampuni ambayo unajua imekutoa wapi kweli? Kwani ukiwapa majibu ya kwamba hilo siwezi kulizungumzia, utapungua nini? Hujisikii kuongea, unaweza ukakaa kimya, hakuna atakayekulazimisha. Maana misingi ya habari inatoa nafasi kubalansi, ukiwa hautaki wao wanajua nini cha kufanya.

Global ina watu wanaokuzidi umri mara tatu au nne. Kuna wafanyakazi ambao wanaweza kukuzaa, unapata wapi ujasiri wa kuwatukana? Unaweza kumtukana mtu aliye sawa na umri wa wazazi wako? Au unataka kutuaminisha kwamba huwa unafanya hivyo kwa wazazi wako? Naamini jibu ni hapana, sasa kwa nini ufanye hivyo kwa watu ambao unajua wana umri sawa au zaidi ya wazazi wako?

Mdogo wangu nataka uelewe kwamba ulikosea, unapaswa kuomba radhi. Hupaswi kuwavimbia kichwa waandishi wa habari wakati haohao bado utawahitaji huko mbeleni. Haohao wanaweza kukusaidia jambo kubwa sana pengine huko uendako.

Nakushauri kuwa muungwana, omba radhi na maisha yataendelea kama kawaida. Kwa umri wako hauna sababu ya kuweka bifu na waandishi wa habari, si wa Global tu hata wa vyombo vigine vya habari. Unahitaji sapoti yao ili uweze kusonga mbele.

Yangu mimi ni hayo tu kwa leo, ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na utatumia busara katika hili. Mungu akusimamie!

Mimi ni kaka yako;

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364