Maisha Yangu Sasa ni Magumu – Ray C
Mwanadada ambaye alifanya vizuri kwenyesekta ya muziki wa bongo fleva Ray C amefunguka na kusema kuwa maisha yake kwa sasa ni magumu.
Ray C alisema hayo kupitia kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa kupitia ting’a namba moja kwa vijana EATV, Ray C amedai kuwa kuna muda mwingine analazimika kuvaa hijabu kujificha ili aweze kupanda daladala na kuweza kufika hospital kwa ajili ya matibabu.
“Unajua maisha haya wanasema mficha uchi huzai, mimi kiukweli maisha kwa sasa magumu maana kulipa kila siku elfu ishirini kwa ajili ya usafiri kwenda Hospital inakuwa changamoto sana na ndio maana muda mwingine navaa kininja ili nipande zangu daladala kwenda kupata dozi hospital”
Ameendelea kusema “Wewe mwenyewe unafahamu mimi msanii na sasa nahangaika kurudui tena kwenye game hivyo kama watu wakiwa wanaona napanda daladala itakuwa shida ndio maana muda mwingine nafanya hivyo” Alisema Ray C
Lakini mbali na hilo Ray C amesema kwa sasa anahitaji sana kurudi kwenye game kwani tayari ameshafanya kazi kama tano ila mtu ambaye alikuwa akimtegemea kumrudisha kwenye muziki hajamsaidia kwa lolote mpaka sasa, hivyo amedai anahitaji msaada wowote ule ili aweze kufanikisha lengo lake hilo.
“Nahitaji kurudi kwenye game ila mtu niliyekuwa namtegemea hajanisaidia, nahitaji msaada, hata ukiwa na buku, buku kumi naomba kwani kwangu zitakuwa ni msaada mkubwa”
“…. unajua ndio maana Q Chief saizi amefanikiwa na amekuwa Role Model kwangu sababu alisema matatizo yake na wakajitokeza watu wakamsaidia na saizi anafanya kazi nzuri kabisa” Aliongeza Ray C.
Ray C aliweza kuonesha masikitiko yake makubwa kwa baadhi ya magazeti ambayo yanamuandika vibaya na kusema magazeti hayo yana lengo la kumuua kabisa na kudai kuwa mambo mengi yanayoandikwa kwenye magazeti hayo ni uzushi.
“Unajua hawa watu sijui wana lengo gani na maisha yangu, nadhani wanataka kuniua kabisa, maana wanaandika uzushi na uongo kuna muda wanasema Ray C amerudia kuvuta unga nawaomba wakiniona wanipige picha na kuziambatanisha na stori zao kama kweli na si kuandika tu vitu visivyo na ukweli, kwani stori hizo zinampa shida sana mama yangu mzazi.” Alimaliza Ray C
EATV.TV