Maswali 3 Ndoa Tata ya Irene Uwoya
STAA wa filamu za Kibongo Irene Uwoya anafunga ndoa leo. Hiyo ni kwa mujibu wake mwenyewe, baada ya kutangaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii tangu mwanzoni mwa wiki hii.
Uwoya mwenye sura na mwonekano wa kuvutia aliyeibuliwa na Filamu ya Division of Love akiwa na Yusuph Mlela ametangaza kufunga ndoa leo Jumamosi Oktoba 28, mwaka huu na mwanaume aliyemtaja kwa jina la Yousouf Enow Piere.
Fujo nyingi mitandaoni ni kuhusiana na ishu hiyo, ambapo bi dada huyo aliyetambulishwa rasmi kama msanii wa filamu za Kibongo baada ya kucheza Filamu ya O’prah aliyoshirikishwa na wakongwe wa muvi za Kibongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ na Steven Kanumba (marehemu) ameibua maswali mengi yanayozua utata.
Inafahamika wazi kuwa Uwoya, mtoto wa Kichagga alipanda madhabahuni Julai 11, 2009 katika Kanisa Katoliki la Mt. Joseph jijini Dar es Salaam na kufunga ndoa na msakata kabumbu Hamad Ndikumana ‘Kataut’ kisha kufuatiwa na sherehe ya kukata na shoka iliyoteketeza mamilioni ya shilingi.
Ndoa ya Uwoya na Ndikumana ilidumu kwa miaka miwili tu, ambapo mwaka 2011 walitengana, wakiwa na baraka ya mtoto mmoja wa kiume waliyempa jina la Krish.
Tuachane na stori za nyuma, kabla ya ndoa yake na Ndikumana ambaye alikiri wazi kuvutiwa na diva huyo baada ya kumuona kwenye sinema ya O’prah, lakini baada ya ndoa hiyo kulegalega na hatimaye kuvunjika rasmi kulipata kutokea maneno ya hapa na pale.
Wametajwa watu kadhaa kupita kwa mrembo huyo wakiwemo wasanii Msami na Dogo Janja, huku wote wakikanusha kuwa na uhusiano, lakini kumi ni pale anapoibuka sasa na kusema kuwa anafunga ndoa na kijana aliyemtaja kwa jina la Yousouf Enow Piere.
Katika picha zinazoonekana kwenye mitandao, Uwoya anaonekana akiwa amevaa gauni la harusi, akiwa amepaka hina, kuashiria kuwa amedhamiria kufunga ndoa ya Kiisalam na kwamba kwa sasa anajulikana kwa jina jipya la ….
Wadau wamekuwa na maswali mengi kuhusiana na ishu hiyo, huenda nawe umejiuliza yako. Cheki haya matatu yanayoonekana kugonga zaidi vichwani mwa wengi.
NI YULE MGUMU?
Juzi kati hapa, Uwoya aliibuka na kudai kuwa mpenzi wake wa sasa ana ngeu nyingi mwilini na kwamba kwake ni fahari kuwa na mwanamume wa aina hiyo.
Katika maelezo yake hayo, Uwoya alisema kuwa mwanamume ambaye ana ngeu kwake ni mshindi kwani anaonesha uanaume halisi tofauti na wale ma-handsome boy.
Wanadai wanajiuliza, je huyu jamaa anayedai kuwa amefanikiwa kumrithi Ndikumana, raia wa Rwanda ndiye yule aliyesema ana makovu ya visu mwilini?
AMEBADILI DINI?
Inafahamika wazi Irene ni Mkristo tena wa kuzaliwa kwa baba na mama. Kuibuka huku na kudai kufunga ndoa ya Kiisalam kuna ukweli au itakuwa ndoa ya bomani?
Hata hivyo, uchunguzi wa Swaggaz kupitia ndugu wa karibu na Uwoya, unaonyesha kuwa wazazi wa Uwoya siyo wana msimamo mkubwa wa dini yao na siyo rahisi kumruhusu binti yao abadili dini.
Hata hivyo, ikiwa Uwoya kweli atafunga ndoa basi huenda ameamua kubadili dini ili kuhalalisha ndoa yake na mwanamume mwingine kwa vile ndoa za Kikristo huwa ni moja tu.
NDOA AU KIKI?
Ndoa hiyo ya Uwoya kwa kiasi kikubwa inaonekana kuwa kiki kutokana na namna alivyoanza kulirusha kwa wadau wake.
Kwa mara ya kwanza, Jumatatu wiki hii, Uwoya alitupia picha ya pete za ndoa, kisha baadaye kadi za mwaliko wa harusi yake hiyo.
Hata hivyo kinachoibua zaidi utata ni kitendo cha kuweka clip inayomwonyesha yupo location akirekodi kazi mpya inayotarajiwa kutoka hivi karibuni.
Matukio mengi ya mastaa hivi karibuni yamekuwa na mfuatano na kiki zaidi hivyo katika hili huenda kuna kiki inatafutwa kabla ya sinema mpya kuingia mtaani.
Lakini huenda kuna ndoa kweli. Ni jambo la kusubiri na kuona.
Mtanzania