-->

Matano (5) Muhimu Kuyajua Kutoka kwa Vanessa Mdee

UKITAJA listi ya wasanii wakubwa wa kike wanaofanya vizuri kwenye muziki wa Bongo Fleva, jina la Vanessa Mdee maarufu V Money, haliwezi kukosekana kutokana na juhudi zake za kuhakikisha muziki wake unapasua anga.

Vanessa hivi sasa anatamba kimataifa, akifanya shoo za nje ya nchi lakini pia akishiriki kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa.

Diva huyu anayetamba na wimbo wake mpya wa ‘Cash Madame’ tayari amekwishafanya kolabo na baadhi ya wasanii wakubwa kutoka nje ya Tanzania na Afrika kwa ujumla ambapo miongoni mwao ni mkali wa RnB kutoka nchini Marekani, Trey Song.

Alhamisi ya wiki iliyopita, msanii huyo alitembelea ofisi za New Habari (2006) Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Dimba, Bingwa, Rai na The African ambapo alipata nafasi ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni yetu.

Hata hivyo, Juma3tata halikutoka kapa. Lilimvuta chemba na kufanya naye interview ya nguvu ambayo iliibua mambo mengi mapya kuhusiana na staa huyo wa muziki wa Bongo Fleva.

Katika mazungumzo na Polisi wa Juma3tata, V Money alizungumza mengi lakini hapa tunakuletea yale makubwa zaidi matano ya kusisimua.

Tembea na paparazi wetu.

ALIWAHI KUJIPELEKA POLISI

Anasema siku moja akiwa barabarani alikutana na msala baada ya kupata ajali ndogo iliyosababishwa na bodaboda, lakini alipotaka kusaidia, wenzake wakatokea ili kumdhuru, ndipo alipochukua hatua ya kukimbilia polisi mwenyewe.

“Hiyo siku nilikuwa kwenye mishemishe zangu, nilikuwa na Feza Kessy. Wakati navuka tuta katika barabara, mara bodaboda akanigonga nyuma ya gari langu. Abiria aliyembeba akaanguka chini.

“Licha ya kuwa mwenye kosa ni bodaboda, lakini kwa utu nikasimama ili nimuone aliyeanguka kama ameumia, nimpatie msaada. Niliposhuka kwenye gari na kukuta abiria hajaumia, nikaanza kumuuliza yule bodaboda, amejifunzia wapi uderava?

“Mara ghafla nikaona wenzake wanakusanyika, Feza akaniambia tukimbie maana kuna hatari eneo lile. Nikafanya hivyo. Yule bodaboda na wenzake wakatukimbiza kwa nyuma.

“Ikabidi nichukue uamuzi wa haraka wa kukimbia mpaka Central (Kituo Kikuu cha Polisi – Dar es Salaam). Huko ndipo nilipoona kuna usalama. Kweli polisi wakatusaidia,” anasema.

NUSURA ATAPIKE STEJINI

Akisimulia kisanga kingine, V Money anasema hawezi kusahau siku alipokuwa kwenye jukwaa la Coke Studio na kuhisi kichefuchefu kikali ambacho kilitaka kumfanya aharibu wakati wakirekodi.

“Ilikuwa kwenye msimu huu wa Coke Studio, siku hiyo  niliamka asubuhi nikiwa nimepoteza sauti kabisa, yaani sikuwa hata na sauti ya kuongea. Kabla ya kupanda stejini nikaamua kunywa mayai mabichi ili kutengeneza sauti.

“Wakati napafomu mara nikaanza kuhisi kama nataka kutapika. Nilijitahidi sana kujizuia, nilifanikiwa lakini ukiangalia kwa makini ile video utaona kuna kitu cha tofauti.”

HAKUNA KAMA YEYE

Vanessa anasema kwa upande wa wasanii wa kike, haoni msanii anayempa changamoto, zaidi ya kujitazama yeye mwenyewe namna ya kupaa kimafanikio.

“Najipa changamoto mimi mwenyewe kwa sababu huwa siangalii kazi ya mtu mwingine… nataka kuwa Vanessa bora zaidi ya Vanessa wa ‘Never Ever’.

“Maana ukianza kutazamatazama utapata yale yaliyompata muogeleaji wa Afrika Kusini kwenye Olympic, aliangalia wa nyuma yake halafu wakamwacha ingawa huwa nafurahi watu kunifananisha na wasanii wanaofanya vizuri kama Yemi Alade, Tiwa Savage, Victoria Kimani na wengine,” anasema Vanessa.

MTV Mamas

Akizungumzia ushiriki wake katika Tuzo za MTV Mamas, Vanessa anasema kuna jamaa alimkatisha tamaa mwanzoni ili aone kuwa hawezi, lakini aligundua kuwa ni kwa masilahi yake.

“Wakati tunawania Tuzo za MTV Mamas nimewahi kuambiwa na meneja wa msanii mmoja mkubwa, lakini si wa Tanzania kwamba sitaweza ushindani. Aliniambia: ‘Naona unawania tuzo na msanii wangu lakini hutashinda.’

“Nikamwambia kweli! Kweli tena sikushinda, wakati kabla ya yule meneja hajaniambia maneno hayo nilishakutana na Patronking akanipa moyo kwamba nitashinda, baadaye jamaa akaniambia siwezi kushinda. Kama ni muoga unaweza kuvunjika moyo maana ndizo changamoto tunazokutana nazo.”

AMEWAHI KUPIGA SHOO NA SCOPION

“Yule jamaa anayeitwa Scopion yule, mimi nimewahi kufanya naye shoo kwenye Shindano la Dume Challenge, alikuwa mpole sana. Niliposikia taarifa zake sikuamini, kwanza niliuliza wanamwongelea nani? Aliyeshinda Dume Challenge?

“Nikasema no… nikakataa katakata, nikawaambia wanioneshe picha, kuja kuangalia kumbe ni yeye. Niliumia sana kwa kweli, sikuamini kama ni yule jamaa niliyeshiriki naye shoo moja angekutana na maswahibu hayo.”

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364