-->

Mwaka wa Tabu kwa Wasanii

Wakati tunaingia mwaka 2016 wasanii walikuwa na matarajio makubwa ya kufanikiwa katika shughuli zao za sanaa kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita, lakini mpaka sasa wengi wanalia kutokana na hali halisi iliyopo kwa sasa katika soko la burudani nchini.

Nikki wa Pili

Watanzania wamelazimika kupunguza starehe na mahitaji yasiyo ya lazima na kugeukia majukumu mengine ya kifamilia, ikiwamo chakula, malazi na mavazi.

Hii ndiyo sababu ya kukosekana kwa mapato katika kampuni mbalimbali ambazo zilikuwa zikizalisha bidhaa zao na faida iliyopatikana kupelekwa moja kwa moja katika sanaa kwa njia ya tuzo na matamasha ya muziki.

Shoo hakuna

Kwa miaka mingi sasa, wasanii waliachana na utaratibu wa kutoa albamu. Wengi wanatoa singo na kutegemea mapato yao kupitia shoo za majukwaani, miito ya simu, mirabaha na matangazo.

Lakini, licha ya matangazo nayo kuadimika, mirabaha kutoeleweka na miito ya simu kudai kupata fedha kidogo, shoo za mikoani na zile kubwa zimekuwa adimu kiasi cha kuwanyima mapato wasanii.

Mapromota waliokuwa wakisimamia kazi za wasanii Bongo wameikimbia kazi hiyo, huku wengine wakishindwa kuandaa matamasha na shoo kutokana na uchache wa wananchi wanaohitaji burudani hizo.

Imeelezwa kwamba mapromota ambao walikuwa wakiandaa shoo mikoani kwa sasa hawafanyi hivyo tena kutokana na kukosekana kwa fedha na hata wadhamini kusuasua.

Mwimbaji Benard Paul ‘Ben Pol’ amedai hali ya uchumi kwa wasanii ni mbaya kutokana na kufilisika kwa mapromota wengi ambao walikuwa wanaandaa shoo mikoani.

Alisema ukata huo umewafanya wasanii wengi, akiwamo yeye kushindwa kutimiza malengo yao ndani ya mwaka huu.

“Mwaka huu mambo yamebadilika, mfumo mzima wa biashara umebadilika siyo kama miaka iliyopita. Yaani hiki ni kitu ambacho wasanii wenzangu watakubaliana na mimi, mzunguko wa pesa na kazi umeshuka kidogo ukilinganisha na miaka mingine. Kwa hiyo, unaweza ukawa na matarajio yako au mipango ukashindwa kutimiza au ikawa tofauti,” alisema Ben Pol.

Kili Music Awards zaota mbawa

‘Kilimanjaro Music Awards’ ni tuzo zilizoanzishwa nchini na kufanyika kwa kipindi cha miaka 22 mfululizo, hivyo kuwajengea wasanii utamaduni wa kuenzi kazi zao na kujenga ushindani miongoni mwao.

Hiyo iliwawezesha wasanii kutengeneza kazi zenye ubora, tija na kuleta hamasa, huku wakijitahidi kutengeneza video zenye ubora ili kuweza kushindana vilivyo katika tuzo za ndani na zile za kimataifa.

Ikilinganishwa na miaka ya nyuma, mwaka jana wasanii walijitahidi kufanya kazi nzuri zaidi huku wakiangalia uwezekano wao kushindana zaidi katika tuzo hizo, kwani wengi wao walijitahidi kufanya video na waandaaji wakubwa na hata waliofanya ndani walifanya kazi zenye viwango.

Taarifa zilizopo Basata zinasema kuwa mpaka sasa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hawajaweza kusema chochote kuhusu tuzo hizo, kwa mwaka huu na kwamba taarifa zilizopo ni kuwa imeingia hasara hivyo kushindwa kuendesha bajeti yake kama ilivyokuwa imepangwa.

Kufutia sakata hilo, Mkurugenzi kutoka lebo inayosimamia kazi za wasanii nchini Rockstar 4000, Seven alisema uwapo wa tuzo ni kitu muhimu na cha msingi ambacho wamekuwa wakikitumia kama kigezo mojawapo cha kumpata msanii wanayemhitaji kwenye lebo yao.

“Vitu kama tuzo, chati za redio na mauzo ya ringtone ni kiwango cha kudhihirisha msanii ana nafasi gani katika sanaa, sisi ni vigezo ambavyo tunatumia pia hata kwa msanii wa nje kwani vinasaidia kutambua kama msanii atafaa,” alisema.

Alisema kukosekana kwa tuzo hizo, kutawafanya walio wengi kuanza kubuni wimbo gani uliofanya vema kwa mwaka upi, kiasi kitakachosababisha kupata takwimu zisizo sahihi pasipo vielelezo hivyo itawaangusha walio wengi kibiashara zikiwamo lebo. Rapa msomi nchini, Nickson Simon maarufu Nikki wa Pili anasema kutokuwapo kwa tuzo ni kumuondolea msanii uwezo wake wa kutengeneza jukwaa na wasifu katika kazi zake za muziki.

“Inampa msanii nguvu na ‘platform’ kwenye muziki, tuzo zisipokuwapo kutapoa na wasanii wataona wamefanya kazi bure, lakini pia tuchukulie kama changamoto kwa Basata wafungue milango kwa tuzo nyingine,” alisema Nikki wa Pili.

Kumbi za burudani kufungwa

Watanzania wengi walijenga utamaduni wa kupumzika, huku wakipiga soga katika vilabu mbalimbali vya pombe na starehe, lakini idadi yao kwa sasa imepungua. Hii imewakosesha mapato wanamuziki wengi wa muziki wa dansi ambao walikuwa wakitegemea mapato kutoka katika baa na kumbi za burudani.

Mwaka huu baadhi ya wanywaji wa pombe na vilevi vingine wamepungua kwa kiasi kikubwa, kiasi cha kuwalazimu baadhi ya wafanyabishara kufunga sehemu za kutolea huduma hizo kutokana na hasara wanayoipata.

Hiyo imesababisha bendi mbalimbali kukosa kazi na hata zile zilizopata kazi hiyo kulipwa ujira mdogo kutokana na mapato hafifu yanayokusanywa na wamiliki wa baa husika.

Vyanzo mbalimbali vya taarifa kutoka sehemu hizo za starehe vinasema walio wengi walikuwa ni wafanyakazi katika mashirika ya umma, ambao walikuwa na uwezo wa kupata fedha nyingi kwa mkupuo.

Mbali na starehe za pombe, wamiliki wa kumbi za starehe, wakiwapo wapambaji harusi wanasema biashara kwao sasa ni mbaya.

“Waliweza kutuchangia harusi, kipaimara na hata rambirambi, sidhani kama kukosa kwao fedha kunaweza kusiwe na athari za moja kwa moja kwao na kwetu sisi tuliofaidi fedha hizo,” alisema Magreti Shayo, mkazi wa jiji la Dar es Salaam.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364