Matuta Yalifanya Nijifiche -JB
MSANII nguli wa filamu za Bongo na shabiki wa klabu ya Simba, Jacob Steven ‘JB’, amesema wakati timu yake ilipoingia hatua ya matuta katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa juzi, hakuweza kuangalia na badala yake alijificha.
Akizungumza na MTANZANIA mara baada ya mchezo huo kumalizika, JB alisema pamoja na ushindi walioupata, hakukiamini kikosi chao hivyo alilazimika kujificha kusubiri matokeo.
Alisema kikosi chao ni kizuri, lakini hatua ya matuta ilikua ni kubahatisha kushinda au kushindwa, hivyo alikosa moyo wa kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
“Mimi bwana likija suala la penalti ni mipango ya Mungu, hakuna cha fundi, sikuweza kuangalia timu, niliamua kujificha na kusubiri kuona nini kinatokea, baada ya kumalizika niliona Simba wakishangilia nikajua tayari tumewamaliza,” alisema JB.
JB alisema Simba inapaswa kujipanga kikamilifu katika msimu huu mpya, kwani wapinzani wao Yanga wameonyesha ushindani wa hali ya juu, jambo linaloashiria ubingwa utakavyokuwa mgumu.
Mtanzania