Mc Pilipili, Rose Ndauka Muwaache!
TASNIA ya uchekeshaji imeendelea kupiga hatua na kuonyeha tofauti ya wazi baina ya wachekeshaji wa zamani na wa kizazi hiki.
Wachekeshaji wa zamani walishindwa kunufaika na sanaa yao kutokana na ukosefu wa uwekekezaji katika vipaji vyao lakini kwa sasa wachekeshaji wanakula bata kutokana na fedha wanazoingiza kupitia sanaa yao.
Miongoni mwa wachekeshaji wanaotengeneza pesaa ndefu kupitia sanaa hiyo ni Emmanuel Mathias maarufu kama Mc Pilipili, ambaye ameendelea kujizolea umaarufu baada ya kuongeza thamani na kuwa mshehereshaji katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Mc Pilipili ambaye ni bosi wa Kampuni ya Pilipili Media House inayojihusisha na biashara kadhaa, amekutana na ripota wa Swaggaz na kupiga naye stori kuhusu sanaa, maisha na mengine mengi.
Cheki mazungumzo yetu.
Swaggaz: Unadhani kwanini tasnia ya uchekeshaji imekuwa na wasanii wachache wenye mafanikio?
Mc Pilipili: Kwa sasa ni tofauti unaona wachekeshaji wengi wanafanikiwa, ukiwatazama kama kina Masanja, Joti na wengine wananufaika na sanaa yao ni ile tu zamani kwamba wasanii walishindwa kuji-brand mfano ni vipaji vikubwa kama Pembe na Senga.
Swaggaz: Ukikaa meza moja na mchekeshaji wa Marekani, Kevin Hart utamwambia nini?
Mc Pilipili: Kevin Hart ni moja ya wachekeshaji wanaoingiza fedha nyingi siyo kwa viingilio vya getini bali kwa bidhaa zake mfano nguo, viatu nk, kwa hiyo nikikaa naye meza moja nitamwambia anifundishe ili Pilipili niwe kama yeye, nivutie kampuni kubwa kuwekeza kwangu.
Swaggaz: Inajulikana upo kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji Rose Ndauka, mashabiki watarajie ndoa siku za hivi karibuni?
Mc Pilipili: Mashabiki waendelee kusubiri, unajua ndoa haitaki haraka ndiyo maana wapenzi wetu tulioanza nao shule za msingi leo hii hatupo nao kwa hiyo inahitaji kujipanga, wasubiri mambo mazuri yanakuja.
Swaggaz: Umewahi kuchekesha halafu mashabiki wakagoma kucheka? Ilikuwa wapi na ulifanya nini?
Mc Pilipili: Hiyo iliwahi kunitokea siku nilipokwenda kufanya shoo Kanda ya Ziwa, sasa kilichotokea ni kwamba ukumbi ambao onyesho liliandaliwa ghafla ukabadilishwa, shoo ikahamia kwenye ukumbi mwingine ambao mashabiki waliingia kwa ajili ya kucheza muziki na siyo kuchekeshwa.
Baba.. nilipopanda jukwaani nikaanza kuchekesha watu wananiangalia tu, zile taa za disko nd’o zinachanganya kabisa, kila nikipiga kitu watu hawacheki tena wanaona nawazingua tu, hiyo siku siwezi kuisahau kabisa.
Swaggaz: Staa gani wa kike ambaye kwako ni smati kichwani, anakuvutia zaidi na kipi kinakuvutia kwake?
Mc Pilipili: Navutiwa na Rose Ndauka, yupo vizuri, anajipanga ni smart kichwani, ana miguu mizuri yaani jamani Rose ooh my God, anavutia kiukweli.
Swaggaz: Nguo gani ya gharama uliwahi kununua?
Mc Pilipili: Kwa sasa naweza kununua nguo ya bei yoyote ninayoitaka ila sema kipindi hicho kwangu mimi nguo ya gharama kununua ilikuwa ni suti, nilinunua Shilingi 17,000 baada ya kudunduliza kwa muda mrefu, hiyo suti ipo mpaka leo kwenye kabati kama ukumbusho, nikiiangalia huwa nafurahi sana sema siwezi kuivaa sababu nimeongezeka mwili.
Swaggaz: Ukiwa kama MC maarufu hapa Bongo, unatekeleza vipi jukumu la ulipaji kodi?
Mc Pilipili: Mimi na kampuni yangu ni walipaji wazuri wa kodi, ni kitu kizuri kwa sababu inaonyesha namna sanaa yetu inavyokua na tunaweza kusaidia nchi yetu.
Swaggaz: Unapenda mashabiki wasikie neno gani zuri kutoka kwako?
Mc Pilipili: Neno ambalo ni muhimu kwa sasa mashabiki waingie Youtube wasisahau ku-subscribe (PilipiliTv) ili waweze kukutana na vichekesho vyangu.
Mtanzania