Mrisho Mpoto Awafungukia Wakuu wa Wilaya Wapya
MWANAMUZIKI wa nyimbo za asili, Mrisho Mpoto, amewaasa wakuu wa wilaya wawatumikie wananchi wao katika wilaya walizopangiwa katika sherehe za kuapishwa Wakuu wa Wilaya wa Jiji la Dar es Salaam.
Akiimba shairi la kuwaasa wakuu hao wa wilaya katika sherehe hiyo, alisema wanatakiwa watekeleze majukumu yao na si kujibweteka na kufanya mambo mengine yasiyo na faida kwa wananchi.
“Wakuu wa wilaya mnatakiwa kuhakikisha mtaitumikia nchi yenu kwa moyo, mnatakiwa kupambana na kuhakikisha mnafanya kazi kwa moyo mmoja na kuachana na mambo ya kujibweteka,” aliimba Mpoto.
Mpoto alisema anaamini hao waliochaguliwa na kuapishwa jana ni wachapakazi na watajitoa kwa moyo kuhakikisha wanayatimiza majukumu yao vyema kwa wananchi.
Wakati huo huo; Mpoto ameibuka na kudai kwamba kudumaa kwa muziki wa asili kunatokana na wasanii wa nyimbo hizo kutotambua namna ya kuongeza thamani ya nyimbo zao ili ziendane na wakati.
Mpoto alisema nyimbo zake zinapendwa zaidi kwa sababu anajua kuongeza thamani ya muziki wa asili si kuishia kwenye mavazi kama baadhi ya wasanii wanavyofanya.
“Wanamuziki wengi hawaendi na nyakati, ni lazima msanii uongeze thamani ya nyimbo zako na ujumbe uendane na kipindi husika na si kung’ang’ania mavazi tu, kuvaa majani na vibwaya,” alisema Mpoto.
Mtanzania