Muigizaji Da Zitta Anusurika Kifo Katika Ajali
AKIWA katika harakati za kukamilisha filamu yake mpya ya ‘Nuru’ muigizaji, Zitta Matembo maarufu kwa jina la Da Zitta amenusurika kifo katika ajali ya gari akiwa anaelekea nchini Kenya kwa maandalizi ya filamu hiyo.
Muigizaji huyo aliyetamba katika filamu ya ‘Gundu’ aliyomshirikisha Anty Ezekiel mwanzoni mwaka huu alifiwa na baba yake mzazi, Fidelis Hokororo Matembo aliyezikwa kijijini kwake Lindi.
Akizungumza na Mtanzania Da Zitta alisema kilichomnusuru katika ajali hiyo kilikuwa ni mkanda alioufunga vyema alipokuwa akiendesha gari lake binafsi aina ya Noah akiwa anaelekea nchini Kenya.
“Nilikuwa nikielekea Nairobi kwa ajili ya kukamilisha filamu yangu ya ‘Nuru’ njiani kulikuwa na gari ilipaki pembeni ghafla ikatoka ikagonga gari yangu tukayumba kisha gari ikahamia upande wa pili ikagonga gari jingine mimi nikatoka salama lakini niliyekuwa naye aling’oka jino na alipata majeraha kidogo kichwani,’’ alisema Da Zitta.
“Sijui yule dereva aliyetugonga alikuwa anafanya nini mle ndani ya gari yake maana alisimama pembeni ya barabara ila namshukuru Mungu kuniepusha na kifo na kuniwezesha kuendelea na safari hadi Filamu yangu imekamilika na wakati wowote itaingia sokoni.’’ Alieleza.
Da Zitta pia ni msanii wa muziki ameshafanya wimbo na mkali wa rap nchini Mr. Blue unaoitwa ‘I don’t think so’.
Mtanzania