Mwakifamba: Hakuna wa Kufikia Kiwango cha Kanumba
RAIS wa Shirikisho la Filamu Nchini (TAFF), Simon Mwakifamba, amesema hakuna atakayeweza kufikia kiwango cha marehemu Kanumba katika sanaa.
Alisema sababu kubwa ni kwamba, msanii huyo alikuwa na uthubutu na alijitoa kwa lolote katika kazi zake tofauti na wasanii wa sasa.
Pia Mwakifamba aliongeza kwamba, sanaa nchini inaendelea kukumbwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ubunifu kwa waigizaji na wanamuziki kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wasanii wanaonakili hadithi za filamu na muziki kutoka kwa wasanii wa nje.
Alivitaja vitu vingine vinavyoongeza changamoto katika sanaa hizo kuwa ni soko na mazingira ya miundombinu kwa ujumla kuanzia uandaaji wa kazi za muziki na filamu.
Mwakifamba alisema sanaa inaweza kupoteza mashabiki na wawekezaji kwa kuwa hakuna ubunifu wa kushawishi wadau kuwekeza katika sanaa hizo kama alivyokuwa Steven Kanumba (marehemu).
Hata hivyo, Mwakifamba aliwataka wasanii kwa ujumla waongeze juhudi na bidii katika ubunifu ili kazi zao ziendane na wakati na kujiongezea mashabiki na soko kwa ujumla badala ya kuendekeza sanaa ya ‘ku-copu & ku-paste’ kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii nchini.
Mtanzania