-->

NDANI YA BOKSI : Anguko la Bongo Movie lilitabirika

Inasemekana soko la filamu za Kitanzania linadoda kila uchao. Katika harakati la kuliokoa, Aprili 19 mwaka huu, wasanii wa filamu waliandamana na kufanya mkutano mkubwa kuwahi kuratibiwa.

William Mtitu akiwa na JB -Wadau wa bongo Movie

Hata hivyo, mkutano huo ulidhihirisha pia kuwa wasanii wenyewe hawajui nini hasa kiini cha kuanguka kwa tasnia yao.

Kwa mfano wakati wakiandamana na kuimba vibwagizo vya “Hatutaki movie za nje au movie za nje bai bai”. Mpaka leo wasikilizaji tumeshindwa kuelewa mwingiliano wa ujumbe huo.

Wazungumzaji katika mkutano huo walikuwa kama walenga shabaha waliorusha risasi zao gizani. Wengine wakikazia uharamia wa kazi za filamu, wengine marufuku ya kazi za nje, wengine maadili ya Kitanzania katika utengenezaji wa filamu. Mkutano haukua na maudhui maalumu. Kwenye mitandao ya kijamii mkutano huo umedhihakiwa vya kutosha. Wachangiaji wengi wakiapa kutoangalia sinema mbovu za Kitanzania.

Kisichoeleweka pengine ni kwamba, hata huko Nigeria kulikosifika, soko la sinema zinazotengenezwa nchini humo limeanguka vibaya. Wanigeria wanajiuliza kitu gani kimeisibu tasnia waliyowahi kujivunia kama ya pili kwa ukubwa duniani. Tasnia iliyowahi kutajwa na tafiti nyingi za kimataifa kama sekta namba mbili katika utoaji wa ajira nchini.

Hapa Tanzania pia, kushamiri kwa biashara ya sinema kulivutia tafiti nyingi toka mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Kilichovutia watafiti wa kimatafa kufanya tafiti si umahiri wa filamu zilizokuwa zikitengenezwa Nigeria au hapa Tanzania bali ni ujio nadra wa tasnia za filamu zinayojiendesha kibiashara. Ikumbukwe kwamba katika nchi nyingi, hata zilizoendelea, sinema bado zinatengezwa na fedha za mifuko mbalimbali ya utamaduni na si mauzo.

Kwa hiyo basi, kitu gani kilifanya biashara ya filamu hizo kushamiri awali na kitu gani kimetokea hiyo inaanguka? Kwa maoni yangu, tasnia hii ulikuwa ni ujenzi wa ghorofa ndefu katika msingi wa tope; anguko lake lilikuwa likitabirika.

Filamu ni taaluma rasmi, ikifundishwa katika vyuo na kutolewa shahada zote kama taaluma zingine. Je, tungetegemea utengenezaji wa filamu zetu ujiendee hivyohivyo bila misingi yoyote ya kitaaluma kwa miaka mingapi? Je, ingewezekana kuwa na madaktari wetu ambao, mbali na kutosomea, wangeendelea kutibu bila kufuatisha mbinu za utoaji tiba zilizojaribiwa kwa miongo mingi na kukubalika ulimwenguni pote?

Kwa hiyo fursa moja muhimu ambayo haikuendana na kustawi kwa kwa utengenezaji wa filamu ilikuwa ni fursa ya elimu. Mara kadhaa chuo mahiri cha filamu duniani New York Film Accademy, kilitembelea Nigeria na kuwasihi vijana wanaonuia kutengeneza sinema zitakazovuka mipaka kusomea ujuzi wa kazi hiyo. Hapa nyumbani ninafahamu pamekuwa na fursa nyingi za stadi za utengenezaji wa filamu kutoka kwa wataalamu wa nje lakini naambiwa wasanii mahiri wa filamu zetu huwa hawaitikii mialiko hii.

Watengeneza sinema wetu wanahitaji kutanua uwezo wao, kama si kwa kwenda vyuoni basi kwa kusoma vitabu vya taaluma au kuhudhuria warsha mbalimbali.

Sababu nyingine ya msingi inayodororesha sinema zetu inaweza kuwa ndiyo iliyobeba kiini cha tatizo. Sinema ni tanzu moja tu ya sanaa za masimulizi. Imekuja wakati sanaa za uchoraji wa picha, muziki, mashairi, ngano, maigizo au riwaya zikiwepo tayari. Umashuhuri wa filamu umetokana na uwezo wake wa kujumuisha na kutumia sanaa zote nilizozitaja hapo juu. Uwezo wa kutumia hadithi zilizoandikwa vizuri, kupangilia picha, matumizi ya lugha ya kishairi, muziki na kadhalika. Kwa maneno mengine msingi sinema ni sanaa hizo zingine.

Ndio maana basi wasanii wa sinema karibu wote huko nje, ukisoma, utagundua awali walikuwa ni wasanii wa aina fulani. Au walikuwa wachoraji, waandishi, wapiga picha, wasanifu wa majengo, wabunifu wa mitindo, waigizaji wa jukwaani au wanamuziki. Hapa kwetu wasanii wengi wa sinema wameibuka tu kama uyoga. Ni ngumu mno kutengeneza sinema zenye mashiko ikiwa jamii haina msingi wa riwaya na ngano, ushairi, uchoraji na sanaa zingine za masimulizi. Sinema zinazotengenezwa kutokana na hadithi za vitabu ni ushahidi mmoja tu wa mwingiliano wa sanaa za awali na sinema.

Kwa maoni yangu kozi inayohitajika kufundishwa haraka ni ya stadi za kuandika hadithi katika mfumo wa sinema. Umuhimu wa tungo zilizoandikwa vizuri kisinema ndio msingi wa sinema duniani kote na haukwepeki. Sisemi kwamba maeneo mengine si ya muhimu ila najaribu kufikiria mahali pa dharura pa kuanzia. Sinema nyingi mno za Kiafrika zinaangukia katika kaburi hili. Hadithi za sinema zina muundo na sayansi yake ili kuhakikisha zinamvutia mtazamaji mwanzo hadi mwisho. Ukihudhuria warsha za misingi ya uandishi wa miswada ya sinema utagundua kumbe sinema zetu wala hazina hadithi.

Mkusanyiko wa mawazo tu (yasiyowiana wakati mwingine) hayawezi kutumika kama muswada. Stadi ya uandishi wa sinema inahitaji nidhamu maalumu kuhakikisha kuwa mtazamaji hachoki wala kupotea katikati ya hadithi. Haishangazi hamasa ya watazamaji imefikia ukomo na soko kudorora baada ya kubaini kuwa hakuna jipya katika tungo hizi.

Pengine Bongo Movie, kama wenyewe wanavyoiita, inaweza kufa lakini sinema kama sanaa tanzu ya masimulizi haiwezi kufa kamwe. Huu unaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuchipua tasnia inayokua taratibu huku ikizingatia misingi ya taaluma. Vijana wenye vipaji waingie kwenye tasnia wakijua kuwa hii ni taaluma kamili na si mahala pa kupatia umaarufu, kutembea kwenye mazuria mekundu na kupata fursa za kuongea na wanasiasa tu. Watafute namna ya kujiongezea ujuzi kila siku.

Kila ninapokutana na vijana waliobahatika kupata fursa ya kwenda kusoma nje huniambia wanaenda kusomea IT au biashara, sijawahi kusikia kijana anaenda kusomea filamu. Bado wengi tunadhani kuwa kigezo cha kutengeneza filamu ni kipaji na uwezo wa kununua kamera tu.

Kwa kuelewa mvuto wa sinema katika jamii wanasiasa wamejenga uswahiba mkubwa na wasanii wa filamu. Wamewatumika kwenye kampeni, wanawasiliana nao moja kwa moja. Viongozi hawa wana fursa nzuri zaidi si tu ya kuinua sanaa bali kukuza uchumi kama ilivyoshuhudiwa Nigeria kwa kuwekeza katika elimu ya utengenezaji wa filamu. Soko la nje lina njaa kubwa ya kununua filamu za kigeni endapo tu zitakidhi viwango vya kitaaluma.

 

Hitimisho

Juhudi iliyofanywa na watengeneza sinema wetu ni uthubutu mzuri na wa kupongeza. Vipaji vingi vimeonekana lakini hatuna budi kufikiria namna ya kutoka hapa na kufikia viwango vya kidunia. Ninawajua Watanzania wachache ambao ama wamesoma kwenye vyuo vya filamu au wamejiendeleza kwa namna mbalimbali lakini baada ya kurejea na kuona mazingira ya kienyeji ya utengenezaji wa filamu yanakinzana na elimu yao, wameamua kukaa pembeni na kuponda sinema zilizopo. Udhuru wao una mashiko lakini unanikumbusha swali lililowahi kuulizwa na mtu mmoja: Je, daktari asiyekubaliana na mazingira ya kazi akae pembeni na kuwaangalia waganga wa kienyeji wakiua watu?

Na; James Gayo

James Gayo ni shabiki wa filamu

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364