-->

NDANI YA BOKSI: Mnalazimisha Kuuza Kitimoto Saudi Arabia !

Kuna kitu kinaendelea Dar es Salaam kwa sasa. Ukikifikiria sana unaweza kulia. Vituko vya Harmorapa vina tija na mvuto kuliko haya ya Bongo Movie. Yaani ni filamu tosha inatengenezwa.

Aunt Ezekiel, JB na Kajala, Wasanii wa Bongo Movie

Bongo Movie wanachofanya ni kuliua zaidi soko la filamu zao. Pamoja na kelele za wadau mbalimbali hawasikii la muadhini wala mnadi swala. Wameweka pamba sikioni na kudumisha ule msemo wa “Sikio la kufa halisikii dawa”.

Wameamua kushika kisu na kuchinja shingo zao. Kuna tatizo kubwa kwenye mishipa ya fahamu. Dah!

Tatizo si Wamachinga. Tatizo ni kutaka tununue filamu ya mtu kaigiza kama malaika kwenye filamu halafu anamwambia mtu mwenye matatizo kuwa “Usijali ndugu, yupo Mungu juu atakusaidia.” Malaika huyo eti. Tatizo wasanii wetu wameamua kutulisha matango pori. Halafu tunaoshindwa kula wanatulazimisha tumeze bila kutafuna. Kweli imefika wakati wasanii wetu wameshindwa kucheza uhusika kwenye filamu zao. Wameshindwa kuandika stori nzuri. Wameshindwa kuandika miswada bora. Na zaidi wameshindwa kabisa kujua kwa nini soko lao limetoweka kama magagulo. Dah!

Mtu anafyatua risasi kwenye filamu halafu inachukua dakika kadhaa kumfikia mhusika. Risasi yenyewe mlio wake kama mtu kawasha njiti ya kiberiti. Inampata mhusika kifuani na damu inatoka kama ile ya kipimo cha malaria.

Mtu yupo na demu wake supermarket nusu saa nzima wanachagua na kutazama vitu, halafu filamu ina saa moja na nusu tu. Dah! Hivi haya mapungufu hawayaoni kabisa Kwenye filamu zao mpaka kuwaonea vijana wanaovuja jasho mitaani wakisaka hela ya kula? Dah!

Haya mambo ndiyo yaliyofanya mioyo ya watu ikinai kazi za wasanii wetu siyo filamu kutoka nje. Eti mtu akipigwa ngumi anaangalia sehemu ya kuangukia kwa usalama wake asije kiumia. Dah!

Kahaba lazima avute sigara, jambazi lazima avae koti refu na miwani ya giza. Hamuoni majambazi wanaokamatwa na jeshi la polisi kila siku kwenye taarifa za habari na magazeti? Wanavaa mnachoigiza? Dah!

Eti mganga wa kienyeji lazima awe porini, mchafu, halafu anaongea kwa ukali kutoa maelekezo kwa mgonjwa.

Inakuaje kwenye filamu jini anavuka barabara kwa kuangalia usalama kwanza kulia na kushoto asigongwe na bodaboda? Huyo ni jini kweli? Dah!

Filamu moja inaonesha mjini ni usiku, kijijini inaonekana ni mchana ila ni siku moja hiyo hiyo na muda ni huo huo. Hakuna uhalisia, wasanii hawavai ule uhusika kabisa.

Ni bora kuwatazama kina Mzee Majuto na Joti kwenye matangazo ya biashara kuliko filamu hizi ambazo wanataka kutulazimisha tununue kinguvu. Sawa hamtaki tuuziwe filamu za nje, kwa lengo la kutuuzia filamu ambazo jambazi anavua viatu akivamia kwenye nyumba ya mtu? Dah!

Katika mapambano ndani ya filamu mnazotaka tununue kinguvu unaweza kuzuia risasi kwa viti au meza za plastiki. Pia Mtanga au mchekeshaji yeyote ni lazima awe mlinzi kila filamu. Na siyo mlinzi tu pia awe mwehu. Taahira au zuzu.

Yaani mtu fulani fyatu asiyejielewa. Kweli Mzee Mengi analindwa na mataahira? Mnatulazimisha tuamini kuwa Mohamed Dewji analindwa na mapunguani. Wasiojielewa? Ndo somo mnalotupa kwenye filamu zenu hizo mnazotaka tununue kwa lazima? Dah!

Hapana kina JB tupeni ‘breki’. Sisi si makoro kiasi hicho, rudini nyuma kajiulizeni kwanza na hata jini ni lazima awe mwanamke?

Nadhani wanapita kwenye mfereji ule aliopita Jini Kabula na kupata umaarufu kwenye Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu. Dah!

Kutokana na haraka ya kucheza filamu nyingi kwa wakati mmoja na kubana matumizi. Siyo ajabu JB kuonekana na shati la aina moja kwenye filamu tatu. Halafu kwenye kila filamu anaachama mdomo wake (kucheka eti) kwenye kila ‘sini’. Naona hiyo ‘swaga’ imekuwa sehemu ya kiungo chake mwilini.

Hakuna uhalisia. Wasanii wetu wanaigiza tu ili mradi. Sasa usishangae filamu inayochezwa ni matukio yaliyokea mwaka 1977 lakini ndani ya ofisi husika ukutani kuna picha ya Rais wa sasa Dk John Magufuli. Bora liende. Dah!

Kila mtu akichomwa kisu lazima iwe tumboni. Familia ya kitajiri lazima waongee kizungu, dadiiii, mamiiiii. Wanatuaminisha kuwa matajiri na watu wenye uwezo wote wanastahili kuwa na tamaduni za Wazungu. Wakati nchi hii matajiri wengi ni Waarabu na Wahindi.

Ukiangalia hizi filamu tunazotakiwa kuzinunua tutake tusitake lazima ukae na ‘rimoti’ karibu maana sehemu ya kugombana sauti inapaaa hadi inakera lazima upunguze, likivuka hilo tukio ndipo uongeze tena sauti. Dah!

Kama filamu waliigizia juani utakiona kivuli cha mtu aliyeshika ‘maiki’ kinatokelezea.

Mama wa kijijini ana mkufu wa dhahabu shingoni na hereni kisha ana kilemba kichwani na kubeba kuni kachakaa nguo na kutinda nyusi na kucha za bandia. Anaongea na simu kizungu kitupu “Okay baby thanks… miss u honey”. Mama wa kijijini huyo. Dah!

Dada anaigiza kama mwanasheria anaenda mahakamani kumtetea mtu na nguo za kutokea usiku, yaani lazima akikaa mapaja yote nje. Dah!

Kituo cha polisi ni kimoja tu. Hata kama wanaishi maeneo tofauti kukiwa na kesi kituo ndio hicho hicho. Na sare zao unaweza kudhani ni askari wa Malawi na wa Comoro.Na wanajitambulisha “Sisi ni askari polisi kutoka kituo cha kati”. Ni hivyo hivyo kila filamu yenye tukio la kipolisi.

Kila anayetoa habari za maisha yake ya nyuma lazima anyanyue uso juu kisha kamera imuoneshe macho. Au lazima asogee dirishani kakunja mikono kifuani, usipoigiza hivyo kwenye filamu hizi tunazolazimishwa kununua hupewi ‘sini’.

Mwanamke amelala kapaka lip shine na make up. Mtunzi, muongozaji, mtayarishaji, mwandishi wa muswada, editor, location manager, mwigizaji mkuu na mtu wa sauti ni mtu mmoja. Dah!

Ukute sasa wanapigana na yale makelele yao “Hwaaaaaaa… Hiyaaaaaaaaa”.

Halafu anayekuja kulipiza kisasi anafika ameshika bastola kisha anaangalia juu huku kamuelekezea mbaya wake bastola. Kamera inaonesha macho yake akikumbuka mabaya aliyotendewa nusu saa nzima, mbaya wake yupo palepale anatetemeka akisubiri kuuliwa. Dah!

Mume na mke wapo ndani ya nyumba yao lakini ukutani kuna picha ya mume na mke mwingine.

Stori zao ni kama hadithi za Madenge tu.

Baba: Madenge nikusimulie hadithi?

Madenge: Ndio baba.

Baba: Hapo zamani za kale palitokea sungura na fisi.

Madenge: Aaaah! Hiyo nishaijua, mwisho wa siku sungura atamzidi ujanja fisi!

Hizo ndo filamu tunazolazimishwa kununua sasa. Dah!

Badilikeni. Fanyeni kazi bora badala ya kuandamana kuwaumiza vijana wanaotafuta pesa za mafuta ya kupakaa watoto wao wanapoenda shule.

Suala hapa siyo filamu kutoka nje. Hapa cha kufanya ni kuwalisha walaji chakula bora. Huo upuuzi wa Wakorea utatoweka automatically kama Babu wa Loliondo. Endeleeni kuigiza mpaka namna ya kurudisha soko lenu. Mtachonga viazi.

By Dk Levy

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364