-->

Ndoa za Mastaa Ndoa Ndoano!

MAPENZI matamu bhana, asikuambie mtu. Katika ulimwengu wa mastaa, hasa masuala ya mapenzi hutawaliwa na mikasa mingi.

Hata hivyo, kuna wakati katika kuhakikisha wanawekana sawa kwenye masuala hayo ya mapenzi, mastaa hukubali kuwa wapole kwa wenzi wao ili mambo yaende sawa.

ROSE NDAUKA98

Makala haya yanakuletea orodha ya mastaa wa Kibongo ambao katika harakati za kusaka ndoa waliamua kubadilisha imani zao za kidini ilimradi mambo yawe bambam.Hata hivyo, katika orodha hiyo wapo waliofanikisha mipango yao ya ndoa, lakini hazikudumu na hivyo kujikuta wakiambulia patupu, huku wengine wakipeta.

FLORA MVUNGI

Nyota huyo wa filamu, Flora Mvungi katika harakati za kusaka ndoa, aliamua kubadili imani yake ya kidini kutoka Ukristo hadi kuwa Mwislamu ili mradi aolewe na Hamis Ramadhani maarufu kama H-Baba. Kwa sasa Flora anafahamika kama Khadija na yeye na mumewe wamebahatika kupata watoto wawili, Afrika na Tanzanite na mwanadada huyo anajinadi anajiandaa kupata mtoto mwingine wa tatu na H-Baba.

JACQUELINE WOLPER

Huyu ni staa mwingine wa filamu za Kibongo ambaye naye aliamua kuachana na imani yake ya Kikristo baada ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na Abdallah Mtoro ‘Dallas’. Uamuzi huo wa Wolper ulisababisha pia kupewa jina jipya na mpenzi wake huyo la Ilham, lakini mambo hayakwenda kama yalivyotarajiwa kwani muda mfupi uhusiano wao ulikoma, hata kabla ya kufungwa kwa ndoa na ingawa Wolper alikuwa akisisitiza kwamba ataendelea kuabudu katika Uislamu, watu wa karibu wanadai amerudia imani yake ya zamani.

ROSE NDAUKA

Mkali mwingine wa filamu nchini, Rose Ndauka naye yumo kwenye orodha hii baada ya kutangaza kuachana na imani yake ya Kikristo alipoingia kwenye uhusiano na msanii wa muziki wa Bongofleva, Malick Bandawe wa Kundi la TGN.

Hata hivyo, wawili hao hawakufanikiwa kufunga ndoa, baada ya uhusiano wao kuvunjika mara baada ya kufanikiwa kupata mtoto na kusababisha mashabiki wao wabaki pasipo kujua nini kinaendelea.

JACQUELINE PENTZEL

Ni msanii wa filamu na mwanamuziki wa Bongofleva, anafahamika zaidi kama Jack wa Chuz. Jack aliamua kuachana na imani ya Kikristo na kuingia kwenye Uislamu baada ya kufunga ndoa na jamaa anayefahamika kwa jina la Gadna Dibibi.

Jack alikiri kuwa alilazimika kubadili imani kutokana na kuwa na mapenzi mazito na mwanamume huyo ila kwa sasa wawili hao nao wameshaachana.

MICHAEL SANGU

Mwigizaji huyu mkongwe aliwahi kubadili imani yake kutoka Ukristo hadi Uislamu baada ya kuzama kwenye penzi la mwigizaji mwenzake, Kuruthum Mpalu ‘Ummy’, nyota wa zamani wa Mambo Hayo. Hata hivyo, ndoa ya wasanii hao haikudumu kwani ilivunjika na Mike kuamua kurejea Ukristo na kufunga ndoa na mwigizaji mwingine mkali, Salome Ndimbagwe ‘Thea’, hata hivyo kwa sasa ndoa hiyo inadaiwa kuvunjika kwa wawili hao kutengana.

JIMMY MAFUFU

Jembe jingine la filamu za Kibongo ambaye naye aliamua kuachana na imani yake ya Kikristo na kuingia kwenye Uislamu ili kumuoa mwanadada anayefahamika kwa jina la Salma. Wawili hao bado wanaendelea kupeta kama kawaida wakifurahia maisha.

AUNT EZEKIEL

Kisura huyu wa filamu aliyeanzia kwenye shindano la urembo la Miss Tanzania, aliamua kuachana na imani yake ya Kikristo na kuingia Uislam, ilimradi afunge ndoa na Sunday Demonte.

Hata hivyo, ndoa hiyo haikudumu mara baada ya kuoana kwani walikuwa hawaishi pamoja. Aunty aliweka makazi yake jijini Dar es Salaam, huku mumewe akiwa anakula maisha ughaibuni, Dubai.

Inadaiwa mumewe huyo alipatwa na mkasa wa kutiwa gerezani huku kukawa na habari za Aunty kula ujana kwa kuanzisha uhusiano na mcheza shoo wa Diamond, Moze Iyobo, aliyezaa naye mtoto wa kike wakiishi kama mume na mke kwa sasa jijini Dar es Salaam.

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364