-->

Programu ya “YES” Yawakaribisha Wanafunzi wa Kitanzania Nchini Marekani

us

Afisa Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani dar es Salaam , Jeffrey Ladenson (amesimama mbele katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wanafunzi 18 wa shule za sekondari za Tanzania Bara na Zanzibar waliotoka Tanzania (Photo Courtesy of U.S. Embassy)

Dar es Salaam, TANZANIA.  Wanafunzi 18 wa shule za sekondari za Tanzania Bara na Zanzibar wamechaguliwa kuishi na kusoma nchini Marekani kwa kipindi cha mwaka mmoja wa masomo kuanzia Agosti 2016 hadi Juni 2017.  Wanafunzi hao waliondoka nchini tarehe 8 Agosti 2016 ili kuanza kipindi chao cha kuwa nchini Marekani.

Kupitia programu ya mabadilisho na mafunzo ya vijana inayofadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani  iitwayo  Kennedy-Lugar Youth Exchange and Study program (YES). Wanafunzi wa shule za sekondari kutoka nchi mbalimbali duniani huishi na familia za Kimarekani, huenda shuleni na  hushiriki katika shughuli mbalimbali ili kujifunza kuhusu jamii ya wamarekani na utamaduni wake. Aidha, wanafunzi hawa hupata stadi za uongozi na fursa ya kuwaelimisha Wamarekani kuhusu nchi na utamaduni wao.  Wawapo nchini Marekani wanafunzi hawa hutumia saa mbili kila mwezi kwa ajili ya kufanya kazi za kuhudumia jamii ili waweze kuona manufaa ya kazi za kujitolea na kushiriki katika masuala ya kijamii ili kuongeza mchango na ushiriki wao katika jamii zao warejeapo nchini mwao.

Jumla ya wanafunzi 800 wa Kitanzania waliofanya vizuri zaidi katika mitihani yao ya Taifa ya Kidato cha Pili walichaguliwa kushiriki katika mchuano wa kupata washiriki katika Programu ya YES. Miongoni mwao, wanafunzi 18 ndio waliochaguliwa kushiriki katika mwaka wa masomo 2016-2017.

Kati ya wanafunzi hao 18, nane wanatoka Zanzibar na 10 wanatoka Tanzania Bara.Kutoka mkoani Arusha, wanafunzi hawa wanatoka katika shule za Canalland, Ilboru, Akeri na Ailanga Lutheran Seminary.  Kutoka mkoa wa Morogoro, wanatoka katika shule za Kilakala, Mgulani, Kola Hill na Mzumbe. Wanafunzi kutoka Zanzibar wanatoka katika shule za Lumumba, Laureate, High View, Glorious, Filter, Trifonia, Konde naVikokotoni.

us33

Afisa Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani dar es Salaam , Jeffrey Ladenson akizungumza na Wanafunzi 18 wa shule za sekondari za Tanzania Bara na Zanzibar waliotoka Tanzania (Photo Courtesy of U.S. Embassy)

Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kilianzisha programu ya YES hapo mwaka 2003 ili kuimarisha maelewano na kujenga madaraja kati ya raia wa Marekani na wale wa mataifa mbalimbali duniani. Nchini Tanzania programu hii inaendeshwa kwa ubia kati ya Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam na asasi isiyo ya Kiserikali ya Kimarekani iitwayo Iowa Resource for International Service (IRIS).  Toka mwaka 2006 jumla ta wanafunzi wa sekondari wa Kitanzania 183 wameshiriki katika programu ya YES.

Kwa taarifa zaidi, tembelea: http://www.yesprograms.org/.

Kwa  taarifa zaidi kuhusu programu nyingine za mabadilishano za viana zinazofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, tafadhali tembelea http://exchanges.state.gov/youth/index.html

Kwa taarifa zaidi kuhusu tukio hili, tafadhali wasiliana kwa barua pepe na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam.

 

 

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364