-->

Seduce Me, Zilipendwa ni shida mtaani

KWA vijana wa kizazi kipya na mashabiki wa Alikiba na Diamond kuna maneno mawili tu yanayotamba Seduce na Zilipendwa. Seduce ni wimbo mpya wa Kiba unaomaanisha ushawishi na Zilipendwa ni wimbo wa Diamond anaokumbushia mambo ya zamani kwa staili ya kisasa.

KAMA ULIKUWA HUJUI

FRESHI REMIX

NI wimbo wa Fid Q ambao amewashirikisha Diamond na Rayvanny kutoka Wasafi (WCB). Fid Q aliimba Freshi kivyake lakini Diamond na Rayvannu wakashirikiana naye kutoa Freshi Remix.

Wimbo huu ulitoka Agosti 24, siku ya Alhamisi na kufanikiwa kutazamwa na watu 572,296 kwenye You Tube hadi kufikia juzi.

Wimbo huu ulizua maneno kwa baadhi ya mashabiki wa Alikiba kwa kudai staa wao huyo ameimbwa kwani baadhi ya maneno ya Diamond amesikika akiimba: “Ukinichukia sikosi hela hivyo kwangu sio kesi, kunikompea na Cinderella aaah… haiwezi kuwa freshi, Simba kutoka mbuga ya Tandale naona swala wanafosi tuwe saresare viuno vidogo wanataka ya pensi ya Pepe Kalle si walitaka kiti nimewapa hadi kitanda wakalale.”

Haikupita hata siku Alikiba kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akaandika: “The King always be a King. Je, umeshakitandika nilale Malikia wangu wa nguvu?#KingKiba.” Maneno ambayo yanatajwa moja kwa moja na mashabiki kumjibu Diamond. Mashabiki wakaanza kuzozana mitandaoni hadi kufikia hatua wasanii wenzao kujiingiza katika mgogoro huo akiwemo Ommy Diampoz ambaye aliingilia kwa kuposti picha akiwa mama wa Diamond huku akimuongelea maneno machafu, hapo ndipo Ney wa mitego, Steve Nyerere na wengine walipojitokeza kuposti kwa kumsema wagombane wenyewe wasiwahusishwe wazazi.

SEDUCE

Ni ngoma mpya ya Alikiba. Imepishana siku mbili na Fresh Remix. Hadi juzi imeangaliwa na watu mil. 2.7 kwenye Youtube. Umeshika nafasi ya pili Afrika kwa kupata idadi kubwa ya mashabiki ndani ya siku tatu na kuwa wa kwanza kwa Tanzania na Afrika Mashariki kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa mwanamuziki wa Kitanzania.

Kutokana na hayo, pia wimbo huo umekuwa gumzo kwa mashabiki wa Alikiba kwa kuutumia kutuma video fupi huku wakiwa wanaucheza.

Vijembe vikaendelea.

ZILIPENDWA

Ngoma mpya ya Wasafi (WCB), imetoka siku moja baada ya wimbo wa Seduce Me. Hadi kufikia juzi watu milioni 1.9 waliukuwa wameutazama Youtube.

Umewashirikisha wasanii wote wa Wasafi ambao ni Diamond, Rich Mavoko, Harmonize, Queen Darling, Rayvanny, Lavalava na wasanii aliyesajili miezi kadhaa iliyopita kutoka Yamoto Bendi, Maromboso. Vijembe vikazidi kukolea.

TIMU KIBA

Timu za mashabiki wao ambazo nyingine siyo rasmi zimenogesha malumbano kwenye mitandao ya kijamii. Wasanii kadhaa wamejipambanua kama timu Kiba. Baadhi ya wasanii walioonekana kuposti ngoma hiyo ya Kiba mpaka jana ni Wema Sepetu, Lulu na Jokate, Jacqueline Wolper, H.Baba wao walijirekodi vipande vya video wakitembea na kuonyesha maumbo yao huku kwa mbali ikisikika ngoma ya Seduce Me kisha kuzitupia Instagram.

Ingawa habari za ndani zinadai ni mkakati wa kibiashara lakini baadhi ya wasanii wamedai kufanya hivyo kama jambo la kawaida tu.

LULU

“Hapana kwangu sio kampeni, ila nimeupenda huu wimbo wa ‘Seduce Me’ kwa sababu umenivutia sana, na niko hivyo, hata ukiangalia katika peji yangu huwa naposti muziki niliovutiwa nao, ukiangalia hata nyimbo za Injili huwa naposti.

Hakuna sababu maalumu, miye nimeposti nilichovutiwa nacho na siko kitimu mimi.”

WOLPER

“Jamani miye si nimeposti tu kama posti nyingine, kwani kuna tatizo? Miye sichagui wanamuziki wa kuposti kwani kila mwanamuziki akitoa kitu kizuri namsapoti na sijafanya hivyo kwa sababu ya kuwaudhi Wasafi (WCB) sio kweli na watu kwanza wajue sina tatizo na Wasafi kabisa naposti zao nyingi huwa nawapa sapoti “Kuhusu kutoposti Zilipendwa ya Diamond, sina jibu la kujibu kwakweli, maana kumsapoti mtu sio lazima uposti katika mitandao.”

H.BABA

“Muziki ukiwa mzuri una raha yake kuposti, sasa Kiba ametoa kitu kizuri kwa nini nisimpe sapoti mwana? Kiba anaweza na miye naposti vitu vizuri sio vibovu vibovu. Kwanini Diamond sijamposti, sababu sipangiwi cha kuposti aise ndio maana nimeposti kitu ninachokipenda.”

TIMU DIAMOND

Waliomposti Diamond ni Dude na Anti Ezekiel pamoja mastaa wenzie wa Kundi la Wasafi pamoja na Lemutuz. Wengine ni mashabiki wake wa kawaida ingawa hali hiyo haijaonekana kumtisha Diamond ambaye anaonekana kujiamini na kusisitiza kwenye mitandao kwamba yeye ni Simba.

Mwanaspoti

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364