Simu ya JPM Kwa Diamond Inaweza Kuleta Mabadiliko
JAPO sanaa ni utajiri ila kuna baadhi ya wahafidhina bado wanaona ni kitu cha kihuni. Kwao msanii ni muhuni na sanaa ndiyo uhuni wenyewe. Bahati mbaya dhana hii haiko kwa watu wa kawaida ila imesambaa mpaka kwa baadhi ya watu walio madarakani. Na hali inapofika hapa ndiyo wazi unajua kuwa sanaa haiwezi kuendelea.
Mfano mzuri angalia chuo cha sanaa Bagamoyo. Mbali na taasisi ile kuwa chimbuko la sanaa halisi na kichocheo cha utamaduni mzuri wa mtanzania na mwafrika kwa ujumla, ila kiko taabani. Kwanini? Kwa sababu baadhi ya walioshika mpini wanaona sanaa ni uhuni.
Kila wawaonapo wasanii wanaona kama ni watu waliokosa la kufanya na kuamua kuimba ama kuigiza. Ila ahsante sana kwa muheshimiwa Magufuli kumpigia simu Diamond akiwa mubashara kwenye kipindi cha runinga.
Wengi tunamchukulia Magufuli kama mtu wa kazi na ofisini tu. Baadhi ya watu hawaamini kama mheshimiwa ana muda wa kukaa hata dakika kumi kusikiliza nyimbo ama kuangalia filamu fulani.
Kwao ukitaja jina la Rais huyu, picha inayokuja katika akili yao; ni kiongozi fulani mkali, asiyetaka utani na mwenye mipango na maendeleo kupitia zile sekta zinazoonekana rasmi tu.
Ila simu yake kwa Diamond imeonesha kitu tofauti. Siyo tu anapenda sanaa na kuifuatilia, ila pia anajua hata maisha ya wasanii. Kamuuliza kuhusu watoto wake na mengineyo.
Hii hali inatakiwa kuwafanya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na hata wajumbe wa nyumba kumi wajue kuwa wanajukumu la kuifanya sanaa ipae zaidi.
Diamond katika maongezi yake ya wazi na mheshimiwa Magufuli hajatuangusha wadau. Ni kama alijiandaa kuwa ipo siku atapata upenyo wa kuongea na mkuu wa nchi.
Kaongea mengi, kalia mengi na kaomba mengi, Diamond kamaliza yote na sasa kazi imebaki kwa mheshimiwa kutekeleza alichoahidi mbele ya watanzania wengi.
Nimefurahi namna Diamond alivyoongea na mheshimiwa. Hajatuangusha hata kidogo. Wasanii wengine huenda wangebabaika na kushindwa kuwasilisha kilio chao. Wangebaki kujiuma uma na kuongea yasiyohusika. Safi sana Diamond.
Mbali na kuwa na mafanikio makubwa katika muziki ila ameonesha bado ana njaa sana. Safi kabisa. Wakati mwingine unapopata nafasi kama hiyo siyo tu unajiangalia peke yako ila inabidi uongee kwa niaba ya wenzako kama alivyofanya Diamond.
Kwa kuonesha anajali sanaa, JPM anakuwa amefanya mwendelezo wa harakati za sanaa alizofanya Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Kikubwa kilichotokea katika serikali ya awamu hii ni ile hatua ya Mheshimiwa Nape Nnauye (aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo) kuonesha nia ya kutilia mkazo uboreshaji katika Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo.
Bagamoyo ndiyo kitovu cha sanaa katika nchi hii. Mbali na wengi kuweza kufanya kazi ya sanaa kwa umakini kutokana na vipaji vyao ila chuo cha Bagamoyo ndiyo msingi wa kuwaweka katika namna bora zaidi.
Kukiendeleza chuo hiki ni fursa ya wengi kuwa katika ubora mkubwa katika sanaa na hivyo kuongeza pato kubwa la Taifa. Hongera mheshimiwa Nape (aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo). Simu ya Dk. Magufuli kwa Diamond ichochee kuharakisha mfumo bora wa sanaa nchini.
Mtanzania