Tunda Man Afungukia Wimbo Wake wa ‘Mwanaume Suruali’ na ‘Dume Suruali’ ya Mwana FA
Msanii wa muziki Tunda Man amedai alisitisha kuachia wimbo wake mpya ‘Mwanaume Suruali’ kama alivyowaahidi mashabiki wake baada ya rapper Mwana FA kumfuata na kumweleza kuwa ana wimbo ambao unaitwa ‘Dume Suruali’ na tayari ameshashoot na video yake.
Muimbaji huyo kabla ya kuachia wimbo wake mpya ‘DebeTupu’ toka mwaka 2016 alikuwa anatangaza kuhusu ujio wa wimbo ‘Mwanaume Suruali’.
Akiongea na Bongo5 Alhamisi hii, Tunda Man amedai kuwa kuna watu wa karibu wa Mwana FA ambao walimfuata ili kuandaa utaratibu wa namna ya kuachia nyimbo hizo ambazo zimefanana majina.
“Unajua mimi nilianza kutangaza toka mwaka 2016 kuhusu ujio wa wimbo Mwanaume Suruali, na ndio project ambayo ilitakiwa kutoka kabla ya ‘DebeTupu’,” alisema Tunda Man. “Lakini kabla sijautoa Suka akaja akaniambia Mwana FA ana ngoma kama hii, yaani ina jina kama la wimbo wako mnatakiwa kupeana muda ili kuzipa nafasi ya kufanya vizuri. Tena ananiambia Mwana FA tayari ameshafanya na video, kwa hiyo mimi nikamwachia atoe na mimi nikatoa ‘DebeTupu’,”
Aliongeza, “Wimbo wangu Mwanaume Suruali utatoka kwa sababu tayari nimeshafanya baadhi ya marekebisho kwa sababu baada ya kuusikiliza wimbo wa Mwana FA kuna vitu niliona vinafafa,”
Pia muimbaji huyo amewataka mashabiki wake kuendelea kuusubiria wimbo huo kwani ukifikia muda wake atauachia.
Bongo5