-->

Ukweli Kuhusu Ndoa ya Uwoya, Dogo Janja

SASA ni wazi kuwa sanaa yetu hapa Bongo haiwezi kwenda bila kiki. Ni kiki kila kukicha. Lesso utasikia msanii huyu kafanya vile, kesho mwingine ameibuka na lake. Ni kama wanashindana.

Imeonekana kama kazi kutolewa bila kianzio cha kiki huenda isiwe na matokeo mazuri sokoni. Hata hivyo kwa upande wangu, napingana na hilo.

Naamini katika kazi bora, yenye viwango kuanzia kwenye utunzi, utayarishaji, utangazaji na hatimaye usambazaji. Ikiwa kazi itatayarishwa na kukosekana hayo, hata ikiwa na kiki kubwa kiasi gani haiwezi kufurukuta.

Habari ya mjini bado ni ndoa ya wasanii Dogo Janja (Bongo Fleva) na Irene Uwoya (mwigizaji). Wenyewe wakizungumza na vyombo mbalimbali vya habari nchini wamethibitisha kuwa ni kweli wamefunga ndoa.

Akizungumza na redio moja ya burudani jijini Dar es Salaam juzi, Uwoya alisema kuwa yupo ndani baada ya kufunga ndoa na mwanamume wa maisha yake na kwamba hawezi kuzungumza chochote kwa vile yupo kwenye arobaini baada ya kufunga ndoa.

Wiki iliyopita nilieleza namna ndoa hiyo ilivyo na utata na kwa namna gani inavyoonekana dhahiri kuwa ni kiki isiyo na kificho. Pamoja na kwamba wawili hao (Dogo Janja na Uwoya) wameendelea kusisitiza kuwa wamefunga ndoa, msimamo wa mwandishi wa makala haya ni kwamba wasanii hao hawajafunga ndoa, bali ni kiki.

NI KAZI YA TIP TOP CONNECTION

Haihitaji akili nyingi kugundua kwamba kuna project inayoandaliwa na Tip Top Connection. Miongoni mwa picha za ndoa zinazosambaa mitandaoni, ipo inayoowaonyesha baadhi ya memba wa Tip Top wakiwa na kiongozi wao Babu Tale.

Memba wanaaonekana kwenye picha hiyo mbali na Tale ni pamoja na Kassim Mganga, Madee na Keisha.

Uchunguzi wa Swaggaz unathibitisha kuwa, hakuna shaka kwamba kinachoendelea ni kiki lakini pia unaeleza kuwa ni kazi kati ya wasanii Dogo Janja au Keisha.

Chanzo chetu cha ndani kinaeleza kuwa, kuna project ya Kesha ipo njiani inakuja. Kikiomba hifadhi ya jina lake gazeni, chanzo hicho kilisema kwamba, uongozi wa Tip Top uliumiza kichwa namna ya kumrudisha Keisha kwenye game, ndipo wakaafikiana kutumia kiki hiyo.

“Keisha ana kazi inarekodiwa… hiyo ni stori iliyo ndani ya wimbo wake mpya ambao video yake kuna hiyo harusi ya Dogo Janja na Uwoya. Kiukweli hakuna ndoa, lakini ni kazi inafanyika.

“Na kweli wamefanikiwa kuwaaminisha watu hilo. Lakini pia nasikia itakuwa ni project mbili kwa pamoja, yaani video ya Keisha na filamu ya Dogo Janja na Uwoya. Hiyo ndiyo siri ninayokumegea,” alieleza rafiki huyo wa karibu na wasanii hao.

NI PIERE SIYO ABDULAZIZ

Kitu kingine kinachoonyesha kuwa ni kiki ya wazi ni pale ambapo walisahau hata jina waliloandika kwenye kadi iliyopostiwa na Uwoya kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika kadi hiyo, inaonyesha kuwa jina la mwanaume aliyetarajia kufunga naye ndoa ni Yousouf Enow Piere, wakati sasa anasema amefunga ndoa na Dogo Janja ambaye jina lake halisi ni Abdulaziz Chende.

WAFIKIRIE ZAIDI

Kiki kwenye sanaa haizuiwi na hasa kwa wasanii wakubwa kama wao, lakini kwa kawaida haipaswi kuwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyo kwenye kiki hii. Uwoya na Dogo Janja wanajaribu kucheza na akili za mashabiki kiasi cha kusimamisha kila kitu na kufuatiliwa ndoa yao hiyo.

Ni kweli kwamba, kwa sasa hakuna kiki kubwa kama hiyo tangu mfululizo wa kiki ulipoanza, kiasi cha kuwafanya watu wabishane sana kuhusu uwepo au kutokuwepo kwa ndoa hiyo.

Kuendelea kuchelewa kutoa kazi iliyokusudiwa kunaweza kuharibu maana ya utangulizi wa kiki hiyo. Kwa namna ubishani ulivyo mkali mitaani, kila mmoja akiwa na msimamo wake, huenda shangwe isiwe kubwa watakapotoa kazi yao kwa kuchelewa.

Tukio la kiki limekuwa kubwa zaidi ya project yenyewe inayotarajiwa.

USHAURI WA BURE

Hakuna shaka yoyote kuhusu uwezo wa wasanii hao. Dogo Janja yupo juu kisanii, kadhalika Irene Uwoya hajawahi kuchuja tangu alipotoka na filamu ya kwanza kabisa iitwayo Division of Love.

Ili waendelee kulinda heshima yao na mapenzi mema ya wadau kwenye sanaa yao, waachie hiyo kazi. Tayari tukio la kiki ni kubwa zaidi ya kazi yenyewe, hivyo basi kuzidi kuchelewa ni kuiandalia sura mbaya project waliyotumia nguvu kubwa kuitangaza kwa mtindo wa kiki.

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364