Uwoya, Kajala Waingia Vitani
Ubuyu mzito! Mastaa wakubwa kunako Bongo Muvi, Irene Pancras Uwoya ‘mama Krish’ na Kajala Masanja ‘Kay’ wanadaiwa kuingia vitani, kisa mapenzi ya wasanii wa Bongo Fleva, Msami Giovani na Abbott Charles ‘Quick Racka’ Wikienda limeng’atwa sikio.
Chanzo kilicho karibu na wawili hao kilipenyeza ishu kuwa aliyeanza yote ni Uwoya baada ya kumchukua mpenzi wa Kajala ambaye ni kigogo serikalini jambo lililomkera na kulipiza kisasi kwa kumchukua Msami.
“Siku zote Kay (Kajala) si mzungumzaji sana zaidi ya vitendo, sasa baada ya kuona kigogo wake anatoka na Uwoya aliamua kulipiza kwa kutoka na Msami,” kilisema chanzo.
Chanzo hicho kiliendelea kutiririka kuwa baada ya Uwoya kuona Kajala amemchukua Msami alihamishia ‘majeshi’ kwa mpenzi wa zamani wa Kajala, Quick Racka. “Ni mwendo wa kulipiziana tu na unaambiwa kwa sasa wawili hao hawazungumzi yaani ni chui na paka,” kiliweka nukta chanzo hicho.
Ili kuweka ubuyu huo sawa, Wikienda lilimtafuta Msami ambaye alifunguka: “Ni kweli mimi na Kajala tuko karibu na mara ya mwisho alitumika na meneja wangu kunikabidhi gari kama sehemu ya jasho langu na hakuninunulia yeye, lakini hata kama kuna vitu vingine vinaendelea siyo mbaya kwani mimi ni mwanaume na yeye mwanamke.”
Alipotafutwa Quick Racka naye alisema: “Ujue kwanza mimi na Kajala mapenzi yetu yalikuwa ya kishkaji sana yaani naweza kutoka na mtu mwingine na yeye hivyohivyo ila hili la kuhusu kutoka na Uwoya si kweli na haijawahi kutokea.”
Kwa upande wa Uwoya alipotafutwa kulizungumzia hili alionesha hali ya kushangaa kisha akasema: “Duh! Sijawahi kuwa na mazoea na Quick Racka hata siku moja na wala mimi na Kajala hatuna tatizo lolote yaani hatujawahi kugombana.”
Alipotafutwa Kajala alipokea simu lakini hakusikilizana vizuri na mwandishi kutokana na kelele lakini alipopigiwa mara ya pili alipokea na kukaa kimya.
Jitihada ziliendelea kwa kumuandikia ‘waraka’ mrefu wenye madai hayo na kumtumia kwenye simu yake ambapo licha ya meseji kuonesha imemfikia napo hakujibu.
Chanzo:GPL