-->

Vera Sidika, Huddah… Bifu Lao Lawapaisha Bongo

MASTAA wa kike wanaochuana vikali katika mitindo nchini Kenya, Vera Sidika ‘Vee Beiby’ na Alhuda Njoroge ‘Huddah’ wanazidi kupata umaarufu Bongo kutokana na bifu lao la muda mrefu sasa.

vera na huddah

Huddah anajulikana kitambo kidogo hapa Bongo, lakini kwa sasa ni kama anampaisha mwenzake Vee Beiby kutokana na bifu lao linalofukuta.

Kwa muda mrefu Huddah amekuwa akimchokonoa Vee Beiby kwa maneno makali kisha baadaye kumuomba msamaha. Huddah alifika mbali zaidi kiasi cha kumsema mwenzake kuwa eti ana ‘ngoma’, lakini baada ya muda anaomba msamaha.

Pamoja na chokochoko zote hizo, Vee Beiby amekuwa mzito kujibu chochote, hadi alipoibuka hivi karibuni katika vyombo vya habari na kueleza kuwa Huddah ana njama za kumzima kistaa.

 

KWANINI BIFU?

Kwa asili Vee Beiby ni mzaliwa wa Mombasa na amekuwa akifanya harakati zake za mitindo akiwa mjini humo lakini baadaye aliamua kuhamia jijini Nairobi, yalipo makazi ya Huddah na hapo ndipo tifu lilipoanzia.

Vee Beiby amepata kueleza kuwa, Huddah hakufurahishwa na ujio wake jijini Nairobi kwa vile aliona kama anamharibia biashara.  Hata hivyo wakati mwingine warembo hao, walikuwa wakipata mialiko ya pamoja katika maonyesho mbalimbali.

Huddah anaonekana amepania kumshusha Vee Beiby kisanii kwa kumzushia mambo ya hovyo kwenye mitandao ya kijamii, lakini kitendo cha Vee Beiby kuwa kimya kinampa karata ya kuzidi kupaa kistaa.

Kupitia bifu hilo, Vee Beiby naye ameanza kupata mashabiki wengi Bongo na Afrika Mashariki kwa jumla, tofauti na nia ya Huddah ya kumshusha.

 

HUDDAH NDANI YA BONGO

Mrembo huyu alichomoza kupitia Shindano la Big Brother Africa The Chase, mwaka 2013. Hata alipotolewa kwenye shindano hilo tayari alikuwa amejitengenezea wigo mpana wa kukamata mashabiki wa Afrika Mashariki.

Tangu hapo kila alichokifanya kiligeuka habari na wengi kuvutiwa nacho. Kabla hajaingia BBA, alikuwa akifanya kazi ya ukatibu muhtasi katika kampuni moja ya ujenzi jijini Nairobi, pia  kutembeza CD mitaani jijini humo kabla ya kujitosa kwenye mashindano ya BBA ambayo yalimtoa jumla.

Umaarufu wake Bongo ulikwenda sambamba na kuwa na urafiki na mastaa wa Bongo kama Diamond Platnumz, Millard Ayo, Harmonize, Diva na vyombo vya habari vilivyomtambulisha vema kwa mashabiki wa Tanzania.

 

VEE BEIBY ATUA BONGO KWA KISHINDO

Vee Beiby ambaye rekodi zinaonyesha kuwa alianza kuonekana kwenye video ya P Unit kama Video Queen katika wimbo uitwao You Guy mwaka 2013, mpaka sasa amefanya video za wasanii mbalimbali Afrika ikiwemo Ebaeno wa msanii K Cee wa Nigeria.

Mrembo huyu ameanza kuchomoza kwa kasi zaidi, kiasi cha wiki mbili zilizopita ambapo amekuwa akipita katika vyombo mbalimbali vya habari vya Tanzania na kuzungumzia namna Huddah anavyomharibia.

 

VEE BEIBY KAMA HUDDAH

Kwa upande mwingine, inaonekana wazi kuwa Vee Beiby ameshtukia dili soko la Tanzania na hivyo kujisogeza kwa nguvu kwa wadau wa hapa +255 – Bongo Dar es Salaam.

Wakati Huddah akiwa amepata umaarufu nchini kwa kujiweka karibu na mastaa na wadau wa Bongo, Vee Beiby naye anaonekana kupitia njia hiyohiyo.

Vee Beiby amemtaja msanii wa Bongo Fleva, Diamond Plantnumz kama msanii anayeimba vizuri na kwamba nyimbo zake zinachezeka, jambo linaloonekana kama njia ya kujiweka karibu naye.

 

BIFU AU KIKI?

Mtindo wa mastaa kutoana kwa kutumia kiki umebamba sana duniani kote kwa sasa. Bado haijajulikana kama Huddah na Vee Beiby wana bifu la kweli au ni janja yao ya kupigana tafu ili waweze kupata soko la Tanzania.

Vyovyote iwavyo, siye twawaachia wenyewe. Vee Beiby, karibu kwenye uwanja wa burudani Bongo.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364