Video 5 Zilizowapa Mkwanja Wasanii Kwa Muda Mfupi
VIDEO zimekuwa chanzo kipya cha mapato kwa wasanii wa Bongo Fleva na sasa hawategemei kuuza audio pekee kama ilivyokuwa hapo awali.
Zamani msanii alitoa video ili kukamilisha utaratibu, lakini sasa imekuwa tofauti kwani msanii anapotoa wimbo analenga kuingiza fedha kwenye audio na video kwa pamoja.
Mtandao wa Youtube ni soko kuu la wasanii kuuza video zao za muziki, kupitia matangazo yanayoonekana kabla ya video kuanza, asilimia flani zinaingia kwenye kibubu cha msanii, kwa kila watazamaji elfu moja wa video basi msanii huyu anatengeneza nusu dola hadi dola moja ya Marekani.
Kwa hiyo kadri video ya muziki inapotazamwa na watu wengi ndiyo hivyo anavyozidi kujipatia fedha. Ndiyo maana siku hizi wasanii wengi wamekuwa wakiwekeza zaidi kwenye video sababu ni soko jipya la kazi za muziki na malipo hayo yapo tu kwa wasanii waliosajiliwa kwani vigezo na masharti huzingatiwa.
Sasa Juma3tata leo tunakusogezea video tano za muziki ambazo zimetoka wiki mbili zilizopita na kwa muda mfupi zimetazamwa mara nyingi zaidi na kufikisha watazamaji zaidi laki 2 hivyo kumuingizia msanii husika mkwanja kwa muda mfupi
Harmonize- Sina
Ni video iliyoachiwa Julai 27 mwaka huu, ndani ya siku saba tayari ilikuwa imefikisha watazamaji milioni 1, inawezekana mafanikio ya wimbo huu yametokana na uwepo wa Mr Nice katika video, akiingiza maisha ya kijana aliyekuwa na fedha nyingi na baada ya matanuzi na starehe mbalimbali akajikuta amekuwa masikini.
Video ya Sina imefanyika hapa hapa Bongo na kuongozwa na Khalfan Khalmadro.
Aslay- Baby
Huu ni wimbo wake wa nne aliouachia mfululizo ndani ya miezi mitatu. Baby ni ngoma nyingine kali ambayo aliiachia Julai 19 mwaka huu na mpaka sasa video yake imetazamwa na watu laki 6.
Video ya Baby imetengenezwa hapa hapa Bongo na kuongozwa na Einxer, mwongozaji ambaye anakuja kwa kasi sana kwenye utengenezaji wa video za Bongo Fleva baada ya kufanya video nyingi za muziki wa Injili.
Rich Mavoko ft Fid Q- Sheri
Baada ya wimbo wao na Harmonize, Show Me kupata mafanikio makubwa, Mavoko ameachia ngoma aliyomshirikisha Fid Q inayoitwa Sheri na video yake imetoka Julai 24 mwaka huu.
Mpaka sasa imetazamwa na watu laki 598,500, ikiwa ni kazi nzuri ya mwangozaji mtanzania, Joowzey.
Joh Makini ft Davido- Kata Leta
Ni kolabo ya tatu ya kimataifa ya rapa Joh Makini, amewahi kufanya wimbo na AKA kutoka Afrika Kusini na Chidima kutoka Nigeria na sasa kwenye Kata Leta amemshirikisha msanii Davido.
Video umefanyika Afrika Kusini na ameitoa Julai 23 mwaka huu ambapo ndani ya siku chache sasa imetazamwa na watu zaidi ya laki 4.
Country Boy ft Mwana Fa- Turn Up
Ni wimbo ambao umejipatia umaarufu katika sehemu mbalimbali za starehe, Turn Up ngoma ambayo imefanikiwa zaidi kutoka kwa msanii, Country Boy akiwa amemshirikisa Mwana Fa.
Video ya Turn Up imetoka Julai 19 mwaka huu na ndani ya siku chache imetazamwa na watu na zaidi ya laki 2. Imefanyika Afrika Kusini na kuongozwa na mtanzania, Hanscana.
Mtanzania