VIDEO: Wasanii ‘Bongo Movie’ Wako Hatarini – JB
Mkongwe wa filamu Jacob Stephen ‘JB’ amefunguka kwamba wasanii wa filamu wapo hatarini kupotea ikiwa hawataweza kwenda sawa na kipindi ambacho tasnia hiyo inapitia kwa sasa.
JB ametoa tahadhari hiyo huku akikanusha hofu iliyopo kwamba tasnia ya movie imekufa ambapo amedai kuwa kuna wasanii wanaoweza kupotea kwenye ramani na kuja wasanii wapya lakini tasnia itaendelea kubaki palepale hivyo mashabiki wasikate tamaa.
Akiwa anabanwa kwa maswali na mashabiki wake jana kwenye kipindi cha Kikaangoni kinachorushwa kupitia ukurasa wa Facebook ya EATV, JB amewataka wapenzi wa movie kuwa wavumilivu kwa sababu kipindi hiki wanachopitia ni cha hatari na sababu kubwa ni kuwa tasnia hiyo ilipokelewa kwa ushabiki mkubwa kitu ambacho kimechangia kupoteza mvuto kwa haraka.
“Bongo movie ilipokelewa kwa nguvu kubwa sana, na kwa kipindi cha miaka kama sita mfululizo na haikuwahi kufanya marekebisho yoyote. Marekebisho haya ya sasa yanayofanyika ni ya kuboresha kutoka hatua hii tuliyopo kwenda nyingine nzuri zaidi lakini hatua hii siyo nzuri kawani kuna watu watapotea na wataibuka wapya” JB alifafanua.
Hata hivyo JB ameongeza kuwa tasnia hiyo inakabiliwa na upungufu wa waandishi na wasambazaji kitu ambacho hata watu waliopo kwenye sanaa wanahofia na mashabiki kuona kama hadithi ni zile zile.
“Kwenye industry tuna upungufu mkubwa kwa upande wa distributors ambacho hicho ndio kilio cha wasanii wote lakini pia ukiangalia upande wa script writters hatuna kitu ambacho mashabiki wanalalamika na siyo Tanzania pekee hili ni la dunia nzima, kama huamini tazama wamarekani saizi wanatengeneza hadithi za kufikirika inabidi tupate watu wenye utaalamu waje kuwekeza” – aliongeza JB.
Kwa upande mwingine JB amesema tatizo la movie hivi sasa ni la dunia nzima, akimaanisha kuwa wadau wa movie duniani kote ikiwemo Nigeria na Marekani wameishiwa vitu vya kuandika kwa kuwa mambo yaliyowapa umaarufu katika tasnia hiyo yamewachosha wapenz wa movie.
Amesema watu hawapaswi kuihukumu tasnia hiyo hapa Tanzania kwa kuwa hadi sasa ina umri wa miaka sita pekee kwa kuwa imeanza rasmi (kibiashara) mwaka 2010.
Huyu hapa JB akiichambua kwelikweli…