-->

Wababe wa Game Wamerudi!

WASANII wenye uwezo mkubwa katika tasnia ya filamu za Kibongo nchini wamerejea mzigoni. Hapa nawazungumzia Jimmy Mponda ‘J Plus’ na Sebastian Mwanangulo ‘Insp. Seba’.

J Plus a.k.a Jimmy Master na Seba

 

Mseto wa J Plus a.k.a Jimmy Master na Seba ni wa aina yake. Ni wasanii wanaocheza sinema za mapigano na kwa hakika kwa namna wanavyoweza kuwasiliana wanapokuwa nyuma ya kamera, hakuna aliyeweza kuwafunika mpaka sasa kwa upande wa mapigano.

Mastaa hawa wamerejea wakati ambao kuna kelele nyingi za soko la Bongo Muvi kuanguka. Sinema za Kibongo zimepoteza mvuto.

Wasanii wenyewe wa tasnia hiyo wametoa sababu nyingi. Wengine wanasema tatizo ni kurushwa kwa tamthilia za nje huku wakieleza sababu nyingine tofauti na hiyo.

Pamoja na sababu zao lukuki, wanaacha ukweli mmoja muhimu ambao unapigiwa kelele na wadau wa filamu za Kibongo kwa muda mrefu – filamu mbovu.

Filamu mbovu ni mchanganyiko wa vitu vingi kwa pamoja. Hadithi, picha, taa, uongozaji, maeneo ya kurekodia nk. Hata hivyo vyote hivi vimebebwa na vitu viwili vikuu; hadithi na wasanii.

Hadithi za siku hizi si za kuridhisha, lakini pia hata baadhi ya wasanii wanaohusishwa katika sinema za sasa siyo wale wenye weledi na vipawa vya sanaa hii bali ni wale ambao wana lengo la kuuza sura kwa sababu zao binafsi.

Vitu hivyo ndivyo vinavyoelekea kupeleka kaburini filamu zetu. J Plus na Seba walikuwepo kabla ya tamthilia za runingani. Walikuwepo kabla ya filamu za kuuzwa mitaani.

J Plus na mwenzake Seba walikuwepo enzi za majumba ya sinema yalivyokuwa yakitamba kila mkoa. Hawa ni zao na Kundi la Mzimuni Theatre ambalo mkurugenzi wake ni J Plus.

WALIPOTOKA

Mwaka 1995 soko la filamu za Kibongo likiwa hata halina dalili za kushika hatamu nchini, Mzimuni Theatre waliachia sinema yao ya kwanza kabisa ilivyokwenda kwa jina la Shamba Kubwa.

Ni sinema iliyooneshwa katika majumba ya sinema nchi nzima. Binafsi, mwaka huo nilipata bahati ya kushuhudia sinema hiyo katika Ukumbi wa Plaza Cinema, mjini Moshi.

Akizungumzia sinema hiyo, J Plus anasema: “Tulikuwa tukifanya kazi kwa moyo, lengo letu ilikuwa kutoa sinema bora. Tulitaka kuwafikia wasanii wa nje. Kwetu haikuwa fahari kuwaacha akina Van Damme, Check Norris, Rambo na wengineo watambe kwenye ardhi yetu wakati kazi tunaiweza. Tukaamua kutoa hiyo sinema ya kwanza ya  mapigano ya Kiswahili.”

Pamoja na vifaa duni wakati huo, ilikuwa sinema nzuri ya mapigano, yenye hadithi nzuri ya kusisimua. J Plus anapongeza kusema: “Kiukweli ilibamba sana kwenye majumba ya sinema nchini.”

MSISIMKO MWANZO MWISHO

Wakati soko la filamu likianza kushika hatamu nchini, Mzimuni kwa mara nyingine waliingia na kazi iliyowaweka pazuri. Sinema ya Misukosuko. Ni filamu iliyokuwa na zaidi ya sehemu sita na haikuchosha.

Wapenzi wa filamu watakumbuka patashika iliyokuwepo wakati Seba akifanya mauaji katika familia ya J Plus na baadaye kukimbilia Mererani.

J Plus alitinga hadi Mererani na kuanza kumsaka Seba, ambapo alifanikiwa baadaye baada ya kukutanishwa kwenye pambano la ngumi la mtaani.

KILA MMOJA KIVYAKE

Baada ya filamu hiyo, kila mmoja alikaa kivyake kwa muda. Seba alicheza sinema kadhaa bila J Plus na Jimmy Master vivyo hivyo.

Seba alionekana kwenye filamu kama Drugs, Inspekta Seba na nyinginezo wakati J Plus yeye akicheza sinema moja tu, Double J mwaka 2012 ambayo ilikuwa na sehemu tano – akawa kimya hadi alipoibuka na Seba kwenye The Foundation.

Wote kwa pamoja, kila mmoja akiwa kivyake walifanya kazi nzuri zenye viwango vya kuridhisha katika sinema za mapigano nchini.

Hata hivyo bado kiu ya mashabiki ilikuwa ni kwa wababe hawa kukutana katika filamu nyingine kama walivyofanya sasa.

Akizungumza na Leisure ya Swaggaz, J Plus anasema: “Maoni yalikuwa mengi sana kabla ya kufikia uamuzi wa kukutana kwa mara nyingine katika sinema mpya iliyoingia mitaani hivi karibuni. Lakini tuliwafikiria zaidi wapenzi wetu.

“Hatukutaka kujishusha, ilikuwa lazima tufunike Misukosuko na sinema nyingine zote tulizocheza. Tumetumia muda, fedha na vipaji vyetu kwa kadiri ya uwezo wetu ili tufanye kazi nzuri ambayo itazidi kutupaisha kileleni kwenye medani hizi za filamu.”

WAMERUDI

“Hiyo filamu ndiyo The Foundation. Haijaitwa hivyo kwa bahati mbaya. Ni kazi ya nguvu inayodhihirisha nguvu yetu kama wasanii wa ukweli kwenye mapigano,” anasema J Plus.

Tayari filamu ya The Foundation inapatikana mitaani. Kama uliwahi kuona sinema zao zilizopita ukaamini hawatatoa nyingine kuzizidi, utakuwa unakosea sana, The Foundation ni habari nyingine.

“Wapenzi wa sinema zetu na wapenda filamu za Kibongo nawasihi wanunue kazi yetu hii, watakutana na kitu cha tofauti kabisa. The Foundation ni levo nyingine. Hilo litadhihirika iwapo mtu atanunua filamu hiyo na kushuhudia mwenyewe,” anasisitiza J Plus.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364