-->

Wastara, Hili la Ndoa Inabidi Ujifunze!

WASTARA22

KWAKO mwigizaji wa kitambo Bongo Muvi, Wastara Juma. Habari za kazi? Unaendeleaje na shughuli zako za kila siku?
Binafsi namshukuru Mungu. Sijambo. Naendelea kupambana. Nimekukumbuka leo kwa barua, maana kitambo kidogo hatujaonana laivu.

Nakumbuka mara ya mwisho tulikutana nyumbani kwako, Tabata. Tukazungumza mengi, lakini hiyo ilikuwa yapata zaidi ya miaka minne iliyopita.

Dhumuni la barua hii ni kutaka kukueleza kuwa licha ya kuwa una nia njema katika suala la ndoa, lakini safari hii kama yule Mbunge wa Donge-Zanzibar, Sadifa Juma mmeachana kwa kheri basi kuna kitu cha kujifunza hapo.
Nakumbuka wiki iliyopita ulipopigiwa simu na waandishi wa Global Publishers, ulieleza wazi kwamba uliolewa kwa kulazimishwa, haikuwa dhamira yako.

Sasa dada yangu hapo ndipo naona wakati mwingine unapaswa kuwa makini. Unaolewaje na mtu ambaye hujamridhia kutoka moyoni? Kwa nini ukubali kuishi na mtu ambaye pengine hujampenda?
Dada yangu nakujua vizuri katika mapito uliyopitia. Umepambana na mengi sana kwenye ndoa tofauti. Kama ni kujifunza, naamini utakuwa umejifunza vya kutosha na wewe si mtu wa kuyumbishwa na fedha wala anasa nyingine za dunia.

Hukuwa na sababu ya kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye hukumtaka. Kama ulivyosema wiki iliyopita kwamba wewe unampenda mtu kwa hali yoyote,  huna sababu kuingia tena kwenye ndoa ambayo watu wanaweza kukufikiria kwamba ulifuata fedha na si mapenzi ya kweli.

Pia hata inapotokea la kutokea kama juzikati mlivyoanzisha varangati la kuachana, hakuna sababu ya kuanika mambo ya ndani. Wewe ni staa lakini ustaa wako usikubali ukaingia kwenye maisha yenu binafsi hata kama mmegombana.
Kupitia sakata lako na Sadifa, mmewafaidisha watu wengi kwa kuzungumza mambo ya chumbani laivu bila chenga. Watu walikuwa hawayajui mambo ya kurogana, mambo ya ulevi lakini kupitia mabishano yenu, wamepata sinema ya bure.

Najua dada yangu wewe si mtu wa kuzungumza hayo yote, naamini ulipitiwa au labda pengine ni hasira tu. Kumbe suala hilo likupe somo kwamba kuna umuhimu wa wewe kujua staha ya ‘kubakisha’ maneno.
Si kila unaloliwaza linastahili kutamkwa. Angalia heshima yako kubwa uliyojijengea katika jamii. Usikubali iyeyuke kama theluji.
Kama umeamua kuachana kabisa na Sadifa, chukua muda kutafakari na Mungu akikujaalia utampata mtu mwingine wa kukuoa.

Usiwe na papara. Hakika utafanikiwa kama kweli utakuwa makini na kutofanya makosa kama yaliyotokea katika ndoa iliyopita.
Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa.
Mimi kaka yako;
Erick Evarist

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364