-->

Wastara: Nilikatwa Mguu, Nikakomaa, Nimefanikiwa

TABATA-Bima Kwenye makutano ya njia nne, ndipo palibadilisha historia ya maisha yake. Anaitwa Wastara Juma Issa Abeid. Ndiyo, ajali mbaya iliyohusisha pikipiki aliyokuwa amepanda yeye na aliyekuwa mumewe, marehemu Juma Kilowoko ‘Sajuki’ na fuso ndiyo ilifungua ukurasa mpya wa maisha yake, simulizi yake inatia hamasa kwa wapambanaji wa maisha, hususan wanawake, twende aya kwa aya.

UMT: Kipi kilianza maishani mwako, uigizaji au biashara?

Wastara: Nilianza na sanaa chini ya Kundi la Mzee Majuto miaka ya nyuma kabla sijaamua kujikita moja kwa moja kwenye biashara, wakati huo nilikuwa naishi Morogoro na familia yangu.

UMT: Kipi kilikutoa kwenye sanaa?

Wastara: Uamuzi. Katika maisha ni muhimu sana kutazama unakokwenda panakufaa au unakwenda tu ilimradi. Niliangalia na kuona ilikuwa lazima nifanye biashara ili nitimize nilichokuwa nakihitaji.

UMT: Ulianza na biashara gani?

Wastara: Bidhaa mbalimbali, kuanzia nguo kuzitoa Congo na Burundi na baadaye nikajikita kwenye biashara ya kununua na kuuza vito vya dhahabu (sonara) ambayo hadi sasa ipo na nilikaa pale kama meneja wa masoko kabla sijarudi tena kwenye filamu.

UMT: Nini kilikurudisha tena kwenye uigizaji?

Wastara: Nilitafutwa na Deogratius Shija akiwa na marehemu mume wangu wakaniambia wana filamu ambayo wangependa sana nishiriki nao, inaitwa Two Brothers, tukaelewana na kuanzia hapo nikajikita zaidi kwenye filamu lakini pia sikuacha biashara zangu, nikawa namlipa Sajuki kiasi fulani cha pesa anifundishe uigizaji zaidi na tukafungua kampuni nikiwa kama mkurugenzi, maana nilikuwa na wazo la kuimba pia lakini sikulitendea haki sana.

UMT: Baada ya kukumbana na ajali na kusababisha kukatwa mguu wako mmoja, matatizo mengi yalijitokeza ikiwemo kufiwa na mumeo miaka michache baadaye, uliweza kusimama, nini siri ya mafanikio?

Wastara: Ni kweli tangu nilipopata ajali matatizo mengi sana yalijitokeza, unajua siku napata ajali ndiyo ilikuwa siku ambayo nilitakiwa nikanunue nguo za harusi, kwa hiyo mipango mingi ilikwama na kifupi nilifunga ndoa muda mfupi baada ya kukatwa mguu lakini haikuchukua muda mrefu mume wangu naye akaanza kuugua, nilihangaika sana na mume wangu nadhani wewe (mwandishi) ni shahidi kwa hili, lakini yote yalipita na sasa maisha yanasonga.

UMT: Nimekuwa nikishuhudia wanawake wengi sana wakikatishwa tamaa na matatizo ya kidunia na kuachana na jitihada za kusaka mafanikio yao, nini neno lako kwa hao?

Wastara: Kwanza, mimi sijioni kama mlemavu na ndiyo maana umeona nimeendelea kuigiza na kushiriki kwenye mikakati mbalimbali ya kimaisha ikiwemo siasa na jamii, kwa hiyo nawasihi waache kulitazama tatizo na badala yake watafute namna au suluhu za matatizo yao kimaisha.

UMT:Kwa sasa unaendelea na biashara?

Wastara: Ndiyo hadi sasa duka la sonara lipo na pia nimejikita kwenye uzalishaji wa video za muziki ambapo nina kampuni ya kurekodi nyimbo yaani audio lakini pia video, ofisi zangu zipo TabataSanene, namshukuru sana Mungu maisha yanasonga.

UMT: Hebu wakumbushe kidogo wadau na wapenzi wa kazi zako, siku ya ajali ilikuwaje?

Wastara: (akikaa kimya kidogo), siku hiyo sikuwa nataka kabisa kupanda pikipiki lakini Sajuki alilazimisha, nikamwambia basi nakubali ili akaniue na yeye akasema ni heri akaniue, kweli bwana kuna jamaa tulikuwa tunaishi naye nikamwambia asizime simu kwani muda siyo mrefu atapigiwa simu aje kuokota maiti, kweli ndiyo tukapata hiyo ajali na yote nabaki nikimshukuru Mungu.

UMT: Hivi karibuni umetoa wimbo wa Wanawake, ukiwahamasisha kupambana na maisha, umeamua kujikita moja kwa moja kwenye eneo la uimbaji na nyimbo zako zitakuwa za aina hiyohiyo au Bongo Fleva za kawaida?

Wastara: Nimeamua kuwatia nguvu wanawake wenzangu kujitambua kwa maana ya uwezo walionao na kupambania ndoto zao, ndiyo maana ukisikiliza wimbo huo na ukatazama video yake, utaona namna ambavyo nimehamasisha wanawake kujituma. Ngoja nikuambie, hii siyo kwa wanawake tu bali ni kwa watu wote kwamba mafanikio huja kwa yeyote mwenye kujituma kwa juhudi kubwa.

UMT: Mwanamke anawezake kuanza biashara ikiwa hana pesa kabisa kwa maana ya mtaji?

Wastara: Hicho ndicho kisingizio kikubwa ambacho wengi hukiweka kwamba hawana mitaji. Muhimu ni kuwa na wazo bora la biashara ambalo unaamini litakuingizia pesa, ukishakua na wazo kisha ukakutana na watu wenye uwezo na unaowaamini hatimaye maisha yako yanabadilika na kutimiza kile ulichokuwa unakihitaji.

UMT: Wastara nikushukuru sana kwa ushirikiano wako.

Wastara: Karibu tena mdogo wangu.

Makala: Brighton Masalu
Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364