-->

Waumini wakimbia Kanisa kupisha bomoabomoa

Waumini wa Kanisa la Freedom Pentecostal Bible Tanzania lililopo Kibamba kwa Mangi wamelikimbia kanisa lao baada ya kukumbwa na bomoabomoa na jana, ibada ya Jumapili ilihudhuriwa na waumini 10 tu.

Kanisa hilo ni miongoni mwa nyumba 30 za ibada zilizokumbwa na bomoabomoa hiyo ili kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya ikiwa ni agizo la Serikali linalotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

Akizungumza jana kanisani kwake, mchungaji wa kanisa hilo, Braun Sikapizye alisema kabla ya kubomolewa lilikuwa na waumini 150 ambao alisema aliwatafuta kwa shida kwa miaka 16.

“Hofu kubwa niliyonayo ni kukimbiwa na washirika wakihofia umbali, maana baada ya kuvunja kanisa letu la awali na kuwekewa alama ya X na Tanroads, tumehama eneo tulipokuwa tukiabudia. Sasa huku tulikohamia waumini hawaji,” alisema.

Alisema awali kanisa lao lilikuwa karibu na barabara, lakini sasa wamehamia ndani zaidi, ambako waumini wanalazimika kutembea umbali wa kilomita tatu kulifikia kanisa jambo alilodai kuwa ni kikwazo kwa waumini wake kufika kanisani.

“Najiona kama napoteza waumini maana huku kuna makanisa mengi, najua wengi watakwenda kusali katika makanisa yaliyojirani, hii ni hasara kwangu na sijui nifanyeje ili kuwarejesha natamani nitafute gari niwapakize wote niwalete kanisani,” alisema.

Mzee wa kanisa hilo, Anthony Simundi alisema umepita mwezi tangu wabomoe kanisa lao na wamekuwa wakisalia nje kabla msamaria mwema kujitolea na kuwapa robo ya kiwanja chake ili wajenge kanisa.

“Hii ni Jumapili ya pili tangu tuanze kuabudia hapa, lakini waumini wamekuwa ni wachahe sana kiasi ambacho kinatishia amani ya kanisa kupoteza waumini,” alisema.

Mmoja wa waumini wa kanisa hilo, Neema Marko alisema idadi ya waumini imepungua, “Wiki iliyopita tumesali waumini 10 wakati kwa kawaida huwa tunasali waumini zaidi ya 50,” alisema.

 

Hali ya Kanisa

Mwanadishi wetu jana alifika katika kanisa hilo na kukuta limejengwa kwa miti na turubai na kufunikwa vitambaa, ukilitazama kwa mbali hutaamini kama ni kanisa unaweza ukafikiri ni kibanda cha wakimbizi.

Aliwakuta waumini saba yaani mchungaji, mzee wa kanisa, watoto wanne na muumini mmoja mtu mzima. Kanisa hilo halina sakafu na limejengwa katikati ya kiwanja ambacho kimezungukwa na vichaka vingi, kwa hali ya kawaida kunaonekana kama shambani.

Upepo ulivuma kwa kasi kiasi ambacho kilisababisha turubai kupiga kelele na kuyumba huku na kule na hata vitambaa na miti iliyojengewa, vilionekana kutaka kung’oka na kupeperushwa na upepo.

Mchungaji wa kanisa hilo alisema alianzisha kanisa lake mwaka 2002 akiwa na waumini watatu. Lilijengwa kwa matope na bati baada ya kupewa eneo na mzee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika (KKKT) wa Kibamba aliyemtaja kwa jina moja la Kessy.

Mchungaji Sikapizye alisema mwaka 2007 walianza ujenzi wa kanisa la kudumu na kulikamilisha mwaka 2012 kwa kuchangisha waumini wake na wadau mbalimbali akiwamo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki ambaye alichangia Sh1 milioni.

Alidai kuwa hata katibu mkuu mstaafu wa CCM, Yusuph Makamba pia alichangia Sh4 milioni katika ujenzi wa kanisa hilo.

Mwaka 2007 wakati wakianzisha ujenzi wa kudumu, alisema wafanyakazi wa Tanroads walifika na kuweka jiwe la mpaka wa barabara ambalo lilionyesha kwamba kanisa hilo lipo ndani ya hifadhi ya barabara jambo ambalo liliwastua waumini na mchungaji huyo.

“Walikuja vijana wakaweka jiwe nilipowauliza wakasema, ‘Mzee sisi tumetumwa na Serikali bwana.’ Sikutaka kuwafuatilia zaidi kwani niliamini mita za barabara ambazo nilizitambua kwa wakati huo zilikuwa 60.”

“Tuliendelea na ujenzi hadi tulipokamilisha, ndipo wakaja kutuwekea alama ya X wakitaka tubomoe, hatukutaka kubishana nao, tulibomoa wenyewe tukawa tunasalia nje lakini baadaye akajitokeza msamaria mwema akatupatia hili eneo unaloliona hapa leo,” alisema.

“Tunaomba Rais wetu atusaidie mchango walau tuweze kujenga tena kanisa, najua kazi ni ngumu sana kuanza tena kuwachangisha waumini ukiangalia, wenyewe hawaonekani,” alisema.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364