-->

Waziri Nape Aelezwa Rose Mhando Alivyo jipu

MSANII wa nyimbo za injili nchini, Rose Mhando, ameshtakiwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, kwa kitendo cha utapeli na kushindwa kutekeleza mkataba wa kuhudhuria na kutumbuiza kwenye Tamasha la Pasaka lililofanyika jijini Mwanza licha ya kulipwa gharama zote alizotaka.

nape3421

Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions inayoongozwa na Alex Msama, ambayo ina mkataba naye imekuwa ikiuza na kuandaa matamasha ya msanii huyo pamoja na tamasha la Pasaka la kila mwaka, alimweleza Waziri Nnauye, mbele ya halaiki ya wananchi alipokuwa mgeni rasmi wa sherehe za tamasha hilo lililofanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Msama alieleza kusikitishwa na kitendo cha Rose Mhando kuingia mitini ilihali akiwa ameingia mkataba na kulipwa gharama zote pamoja na nauli alizodai kabla ya kuanza safari kufika Geita, Mwanza na Kahama kujiunga na wasanii wenzake kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha hilo.

“Mheshimiwa Waziri, Rose Mhando naye amekuwa ni jipu kwa kuwa amefanya utapeli kwa kukubali kulipwa gharama zake zote lakini ameshindwa kuhudhuria na kutumbuiza kama wenzake wakina Solomon Mkubwa, Bonny Mwaitege, Upendo Nkone na wengine uliowashuhudia hapa.

“Hii ni mara ya tatu amekuwa akifanya hivi na mara kwa mara nimekuwa nikimsamehe,” alisema bila kutaja kiasi alichomlipa katika mkataba waliokubaliana ili aweze kufanya onyesho hilo.

Msama pia akatumia fursa hiyo kuwaomba radhi wananchi waliofika katika Uwanja wa CCM Kirumba kwa kutegemea mwimbaji huyo angekuwepo na kutumbuiza na wenzake lakini kilichotokea ni aibu na utapeli wa msanii huyo mkubwa wa nyimbo za injili aliyejizolea umaarufu ndani na nje ya nchi.

“Kuanzia leo mtu yeyote asije akaingizwa mjini na Rose Mhando kwa kuingia naye makubaliano akidhani yupo chini ya Kampuni ya Msama Promotions, kwa kitendo alichoendelea kukifanya naomba kutangaza rasmi kuvunja mkataba wa kufanya kazi na msanii huyo ili kulinda hadhi na heshima ya Kampuni yangu,” alisisitiza Msama.

Msama aliomba wananchi waendelee kuipa sapoti kampuni yake kwa kuwa imekuwa ikirejesha mapato ya viingilio na sadaka katika tamasha hilo kwa jamii hasa kwa watu wasiojiweza, makundi maalumu pamoja na kuendeleza vipaji vya wasanii chipukizi wa nyimbo za injili nchini kote.

Hata hivyo, wadau mbalimbali waliokuwepo katika uzinduzi huo walisikitishwa na kutokutokea kwa mwanamuziki huyo huku wengine wakimlalamikia kuwa na tabia hizo kwa muda mrefu na kufanya bila woga na hofu yoyote.

Mwanamuziki huyo aliwahi kuripotiwa kutuhumiwa kufanya udanganyifu kwa kupokea zaidi ya Sh milioni 3 na kisha kushindwa kufanya onyesho katika tamasha la nyimbo za injili lililoandaliwa mkoani Njombe mwaka jana.

Mkurugenzi wa Kampuni ya The Comfort Gospel Promotions, Seth Sedekia, ndiye alimfungulia kesi hiyo  katika kituo kikuu cha polisi Njombe na akapewa RB namba: NJ/RB/1793/2015.

Kushindwa kutokea kwa mwanamuziki huyo siku hiyo ya Jumapili iliyopita, kuliwafanya mashabiki waliokuwa wamelipa kiingilio cha shilingi 5,000 kila mmoja kuzusha vurugu kubwa kwa mwandaaji huyo wakidai wametapeliwa huku wengine wakionyesha kuchukizwa na kitendo cha mwanamuziki huyo kushindwa kutokea kufanya onyesho hilo.

Mwandaaji wa onyesho hilo, Sedekia alisema amefikia hatua ya kufungua kesi kituo cha polisi kufuatia kumlipa fedha zote shilingi milioni tatu Mhando ambazo alisaini mkataba naye akiwa mjini Dodoma kwa ajili ya kufanya onyesho mjini Njombe. Katika onyesho hilo, Mhando alitarajiwa kushirikiana na msanii wa nyimbo za injili, Happy Kamili kutoka jijini Mbeya ambaye alifika katika tamasha hilo akishirikiana na wasanii wengine kutoka mjini Njombe.

Ofisa Habari wa Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Franco Malimba, alipoulizwa juu ya kuwepo kwa taarifa hizo katika kituo cha polisi, alikiri kuwepo lakini alisema hawezi kulizungumzia kwa sababu halijafika ngazi za juu.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364