-->

Wema: Nisipopata Mtoto Nafunga Kizazi

Exclusive! Hapo nyuma kumepita matukio mengi yaliyomhusu staa mwenye jina lake kwenye tasnia ya sinema za Kibongo, Wema Abraham Isac Sepetu, lakini mwenyewe hakuwa tayari kufungua kinywa kutoa ufafanuzi na hisia zake.

Ni kupitia Ijumaa Wikienda ambalo limethubutu kufanya naye mahojiano maalum ambayo ndani yake alifunguka mambo mazito kuhusu maisha yake ya sasa na kuelezea dhamira yake ya kutaka kufunga kizazi endapo safari hii hatajaliwa kupata mtoto baada ya kupata mpenzi mpya.

NYUMBANI UNUNIO

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Wema, Ununio jijini Dar, staa huyo ambaye ni Miss Tanzania 2006/07, aliweka wazi mambo ambayo watu wamekuwa wakiyasema bila mpangilio wala kusikia kauli yake.

UNGANA NA WEMA

Ijumaa Wikienda: Mambo vipi Wema? Ni muda mrefu sana mashabiki wako hawajakusikia. Je, ni kwa nini umeamua kuwa kimya kiasi hicho?

Wema: Sasa hivi nimebadilisha ratiba nzima ya maisha yangu. Kuna vitu ambavyo

nilikuwa ninavifanya zamani, sasa hivi nimepunguza au sifanyi kabisa.

Ijumaa Wikienda: Kama vitu gani?

Wema: Labda kutoka usiku kwenda kwenye kumbi za starehe. Hii ni kwa sababu nilikuwa sioni raha yoyote ya kufanya hivyo.

Ijumaa Wikienda: Kwa nini ulikuwa huoni raha?

Wema: Yaani tangu unaingia ukumbini mpaka mwisho watu wanaomba kupiga picha tu hivyo huwezi kufurahi ulichoendea pale na ukimnyima mtu kupiga naye picha, atasema unaringa.

 Ijumaa Wikienda: Kuna tetesi kuwa ulitolewa posa na ukatakiwa kukaa ndani kusubiri uolewe, je hilo nalizungumziaje?

Wema: Ni kweli nilitolewa posa, lakini baadaye ilirudishwa.

Ijumaa Wikienda: Kwa nini posa iletwe, ipokelewe halafu irudishwe?

Wema: Aliyeleta posa sikuwa ninampenda kutoka moyoni mwangu na wakati posa imeletwa, mchumba wangu ambaye niko naye kwa sasa hivi tulikuwa tumegombana, akanisihi sana nisiipokee kwani hata yeye yuko tayari kunioa.

Ijumaa Wikienda: Kwa hiyo wewe sasa hivi uko tayari kuwa mke wa mtu?

Wema: Bila tatizo lolote kabisa, sasa hivi utoto nimeuweka kando na nimefanya mazoezi ya kutosha ya kuwa mke wa mtu. Ijumaa Wikienda: Vipi kuhusu penzi lako na Idris?

Wema: Halipo tena japokuwa najua kabisa yeye ananipenda.

Ijumaa Wikienda: Je, watoto wale apacha ambao ulimbebea mimba Idris wangekuwepo mngeachana?

Wema: (anainamisha kichwa) tena usinikumbushe watoto wangu, lakini tungeendelea kuheshimiana kama watu ambao tumezaa.

Ijumaa Wikienda: Vipi kuhusu suala lako la kupata mtoto? Ulishalipatia ufumbuzi wa kitaalam na kujua tatizo ni nini?

Wema: Ndiyo na tena safari hii nisipobahatika kupata mtoto hadi ninafikisha umri wa miaka 32 (kwa sasa ana 29), nitafunga kizazi.

Ijumaa Wikienda: Kwa nini ufunge kizazi maana kuna watu wanazaa hata wakiwa na umri wa miaka 40 na  aidi na hata mifano ipo mingi ya watu waliopata watoto uzeeni hasa ukisoma kwenye vitabu vitakatifu?

Wema: Hapana! Mimi sitaki hiyo.

Ijumaa Wikienda: Tukiacha hilo, kuna madai mengi kuwa unatumia dawa za kuongeza makalio na mahipsi, unalizungumziaje hilo?

Wema: Nakumbuka wakati ninashinda kuwa Miss Tanzania, kwenye moja ya magazeti yenu mliniandika kuwa mimi ndiye Miss Tanzania wa kwanza kuwa na kalio, umesahau?

Lakini pia wamuangalie hata mama yangu jamani, unajua kuna wakati watu wanasema hadi nimewadharau.

Ijumaa Wikienda: Mara nyingi unapenda kuishi na wanaume tata (mashoga) nyumbani kwako au hata kuongozana nao, je, ni kwa nini?

Wema: Mimi sijui ni kitu gani lakini ninawapenda sana hao watu na ninafurahi sana kuwa nao maana hata mama alikuwa hapendi kabisa kuona wapo kwangu lakini sasa amewazoea na ninaona nao ni binadamu kama mimi.

Ijumaa Wikienda: Mastaa wengi wamekuwa wakiishi katikati ya mji kama Kinondoni, Sinza, Kijitonyama na kwingineko, kwa nini wewe umeamua kuishi mbali na mji?

Wema: Mimi ninahitaji sana faragha yangu, sasa ukiishi katikati ya mji kila siku watu watakuwa wakiingia na kutoka na hapa nikitoka ninasogea mbali zaidi, sirudi tena katikati ya mji.

Ijumaa Wikienda: Unasogea wapi?

Wema: Kwa sasa ninajenga maeneo ya Mapinga, huko ndiko nitakakoenda kuishi.

Ijumaa Wikienda: Wewe na Martin Kadinda (meneja wa Wema) inaonesha hamko kama mlivyokuwa huko nyuma, je, kuna tatizo lolote?

Wema: Hakuna tatizo, tupo sawa, sema tu mimi nilikuwa kambini karibu miezi miwili, ninafanya kazi yangu ya Filamu ya Heaven Saint lakini hatuna shida.

Ijumaa Wikienda: Wasanii wengi wanalalamika kuwa filamu haziwalipi kwa sasa na soko limeshuka, lakini wewe ndiyo kwanza unaingia kambini, je, nini mtazamo wako?

Wema: Unajua sisi wenyewe ndiyo tunashusha soko la filamu kwa sababu hatutengenezi kitu kilicho bora kwa mashabiki wetu. Mashabiki wanahitaji vitu vya tofauti, lakini hatujui, tumebaki kulalamika tu.

 

Ijumaa Wikienda: Zamani ulikuwa uko bize na mbwa wako, lakini siku hizi mbwa wako hawaonekani kwenye ukurasa wako wa Instagram, vipi uliwauza?

Wema: Hapana! Wapo mpaka sasa, tena Gucci (jina la mmoja wa mbwa wake) amezaa. Sema tu siku hizi nimepunguza mambo ya mitandaoni.

Ijumaa Wikienda: Kuna utofauti gani uliouona tangu umehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ukilinganisha na ulipokuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)?

Wema: Huku naona nina furaha sana. Nipo huru kupita maelezo. Yaani kiukweli sijui kama ipo siku nitarudi nyuma.

Stori: Imelda Mtema | IJUMAA WIKIENDA| Dar

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364