Zari Kuishi Kwenye Nyumba ya Ivan Au Diamond?
KAMATI ya watu wanne walioteuliwa kushughulikia namna ambavyo mali za marehemu Ivan Ssemwanga zitasimamiwa, imempa mpenzi wa mkali wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Zari Hassan, moja ya nyumba za marehemu huyo iliyopo nchini Afrika Kusini ili aishi na watoto wake.
Kwa mjibu wa mtandao wa Kenya moja, kamati hiyo iliwajumuisha Ritah Ssemwanga (dada wa Ivan), George Ssemwanga Pinto (kaka wa Ivan), Lawrence Kiyingi Muyanja maarufu King Lawrence (rafiki mkubwa wa Ivan) ambaye pia ni kiongozi wa kundi la matajiri wanaojiita (Rich Gang) na Zari Hassan (mke wa Ivan).
Kwa pamoja kamati hiyo imekubaliana kwamba licha ya kumpa Zari nyumba hiyo, pia imempa madaraka ya kusimamia chuo cha Ivan cha Brooklyn, kilichopo Afrika Kusini.
Pia Zari ameamliwa kuishi na watoto wake katika moja ya nyumba za Ivan zilizopo Afrika Kusini na nyingine itapangishwa ili kusaidia familia hiyo kiuchumi, huku kamati hiyo ikiendelea na usimamizi wa jumla hadi watoto hao watakapofikia umri wa kujitambua wa miaka 18.
Kutokana na hilo, Zari ameondoka Uganda na kuelekea Afrika Kusini, ingawa bado haijajulikana kama ataishi katika moja ya nyumba za Ivan huko Pretoria, Afrika Kusini au ataishi na watoto wake kwenye nyumba ya mpenzi wake, Diamond Platnumz, aliyonunua jijini Johannesburg.
Mtanzania